• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 7:52 PM
Analenga kuibuka msanii mahiri nchini pia kuanzisha brandi yake

Analenga kuibuka msanii mahiri nchini pia kuanzisha brandi yake

Na JOHN KIMWERE

MGAAGAA na upwa hali wali mkavu,’ ni methali inayohimiza wanadamu kamwe kutovunjika moyo kwenye jitihada za kufukuzia malengo fulani maishani mwao.

Aidha ni methali inayothibitishwa na wengi wanaozidi kuchangamkia shughuli mbali mbali katika harakati za kusaka riziki. Miongoni mwao ni mwana dada Clarice Apiyo Etori ambaye ni mwigizaji, mchoraji na mwana mitindo.

”Maisha ya sasa kamwe sio mteremko inabidi kila mmoja atumie talanta alizotunukiwa na Maulana,” alisema na kuongeza kuwa anajivunia chochote ambacho hufanya ili kuweka mkate mezani.

Msanii huyu hutumia penseli kuchora picha za wateja wake wakiwamo wasanii na wananchi wa kawaida ambazo hulipisha kati ya Sh2,500 hadi Sh25000. ”Kwa uchoraji nimepania kumiliki studio yangu ili kutoa nafasi kwa wachoraji wanaokuja kupalilia vipaji vyao,” akasema.

Clarice Apiyo Etori mwigizaji, mwana mitindo na mchoraji…Picha/JOHN KIMWERE

UIGIZAJI

Katika tansia ya uigizaji binti huyu analenga kuibuka msanii mahiri nchini pia kuanzisha brandi yake ili kupata nafasi ya kukuza waigizaji wanaokuja. Anajivunia kushiriki filamu kadhaa tangia ajitose kwenye masuala ya maigizo.

Ameshiriki kipindi cha Zora na Varshita zilizopeperushwa kupitia Citizen TV na Maisha Magic Plus. Filamu hizo zilizalishwa na Jiffy Pictures na Moonbeam mtawalia. Pia anajivunia kushiriki kipindi cha Perfect Match ambacho hupeperushwa kupitia Ebru TV.

”Maisha ni mzunguko maana tangia utotoni mwangu nilidhamiria kuhitimu kuwa wakili lakini hali sio hali elimu ilinipiga chenga,” anasema na kuongeza kamwe hajutii kwa kutotimiza azma hiyo.

Kisura huyu anasema analenga kutinga upeo wa mwigizaji wa Kenya Sarah Hassan ambaye ndiye muhusika mkuu kwenye kipindi cha Zora. Ndani miaka mitano ijayo anatamani sana kuwa ameiva na jina lake kutambulika kote nchini na dunia nzima. Pia anatamani sana kuwa amefikia hadhi ya kufanya kazi na wana maigizo nyota Afrika kwa jumla.

NOLLYWOOD

Wakenya wengi wanapenda kutazama filamu za Kinigeria (Nollywood) kuliko kazi za wenzao wa humu nchini. Dada huyu anasema wasanii wa Kinigeria wana vifaa vya nguvu ambavyo hufanya kazi ya kupenda na wasimamizi wao wamebobea zaidi pia hushirikiana vizuri. ”Kwetu hali ni tofauti maana mara nyingi hukosana kutokana na mambo ambayo haifai,” akasema.

Anadokeza kuwa serikali haipaswi kudharau wasanii chipukizi bali inastahili kuanzisha mikakati kabambe kuwasaidia kutimiza maazimio yao. Aidha anasema hata wasanii waliowatangulia walianzia chini kama wao.

Baadhi ya picha ambazo amewahi kuchora za kati ya wasanii tofauti katika sekta la uigizaji….Picha/JOHN KIMWERE

PANDASHUKA

Anasema sekta ya maigizo imejaa changamoto kibao ikiwamo waliowatangulia kuonyesha mapendeleo kwa wenzao wanaofahamiana. ”Bila kuongeza chumvi wasanii chipukizi hupitia mengi ikiwamo kasumba ya ubaguzi,” alinena.

MAWAIDHA

Ingawa hajapiga hatua kubwa katika masuala ya uigizaji kamwe sio mchoyo wa mawaidha. Anashikilia kuwa licha ya changamoto ambazo hupitia wajitume kiume pia wasife moyo wala wasikubali maprodusa kuwashusha hadhi.

Anawahimiza kuwa ni muhimu kuwa na malengo ya wanayopania kutimiza. Kadhalika anasema wanapaswa kuwa wabunifu ili kuwapiku wenzao wakati wa majaribio ya kutafuta ajira.

KANUNI

Msanii huyu aliyetua duniani mwaka 1999 anasema amejiwekea kanuni kadhaa ili kuhakikisha anatimiza malengo yake katika usanii. Baadhi yazo ikiwa:Kujiamini, kupuuzia chuki za wenzake, kuheshimu mbinu na masharti ya uigizaji, kuheshimu waliowatangulia katika sekta hii, kufanya utafiti ili kujifunza zaidi masuala mapya katika usanii, kukubali anapofeli na nyakati zote kumtumainia Mungu.

Kuhusu mahusiano ya kimapenzi anasema kamwe hawezi kuweka katika kaburi la sahau wakati fulani aliwahi kulia alipogundua mpenzi wake alikuwa akimchezea karata dhidi ya mwana dada mwingine. Anadokeza kuwa yupo singo hadi atakapompata mwanaume anayempenda alivyo pia bila kubagua shughuli anazopiga ili kujikimu kimaisha.

You can share this post!

Washukiwa watatu wa wizi wa simu wakamatwa na simu 9 siku...

Trailblazers yapania kutinga fainali za Klabu Bingwa Afrika...

T L