• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 9:50 AM
Trailblazers yapania kutinga fainali za Klabu Bingwa Afrika (CAVB) mwaka ujao

Trailblazers yapania kutinga fainali za Klabu Bingwa Afrika (CAVB) mwaka ujao

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wanaume ya Trailblazers ndio mwanzo inashiriki mechi za ligi kuu ya voliboli nchini lakini inaonekana inalenga makubwa.

Endapo itaendeleza mtindo huo bila shaka itatikisa wakali wa mchezo huo nchini ikiwamo Kenya General Service Unit (GSU), Kenya Prisons, Jeshi la Ulinzi (KDF) na Halmashauri ya Bandari ya Kenya (KPA) kati ya zingine.

Trailblazers inanolewa na kocha, Geoffrey Omondi aliyekuwa mkufunzi wa Co-operative Bank pia aliyewahi kufunza timu ya taifa. Kocha huyo anasema ”Ingawa hatujakaa vizuri tumepania kupambana mwanzo mwisho kuhakikisha tunajikatia tiketi ya kushiriki fainali za ngarambe ya muhula huu ili kupata nafasi kuwania tiketi ya kufuzu kushiriki kipute cha Klabu Bingwa Afrika (CAVB) mwaka ujao.”

Kikosi hicho chini ya nahodha, James Mutero tayari kinajivunia kushinda mechi mbili kati ya tatu ambazo kimeshiriki. Ukishuhudia mechi ya wachezaji hao bila shaka utagundua kuwa wamepania kujiunga na wapinzani wakuu kwenye fani hiyo nchini.

”Kwenye mechi ambazo tumeshiriki nimeridhishwa na mchezo wa wachezaji wangu,” kocha huyo alisema. Kwenye mechi za raundi ya nne zilizopigiwa ugani Nyayo Stadium, Nairobi (Ijumaa) wanaume hao walishusha mchezo safi dhidi ya Administration Police (AP Kenya) ambapo walibeba ushindi mtamu wa alama tatu muhimu waliposajili seti 3-0 (25-16, 25-22, 25-12) kinyume na matarajio ya wengi.

Wachezaji wa Trailblazers (kulia) wakicheza na wapinzani wao Administration Police (AP Kenya) kwenye mechi za voliboli ya ligi kuu ugani Nyayo Stadium, Nairobi. Trailblazers ilishinda kwa seti 3-0…Picha/JOHN KIMWERE

Kwenye mechi za kipute hicho kesho Jumapili (18.04.2022) wanaume hao wataingia dimbani kumenyana na Western Prisons. Kocha huyo anatoa wito kwa wachezaji wake kuwa makini zaidi dhidi ya wapinzani hao waliovuruga KDF kabla ya kuzimwa kwa seti 3-0 (25-12,25-21, 25-22, 25-15).

Kwenye matokeo mengine: Prisons Kenya ilicharaza Prisons Nairobi kwa seti 3-0, Prisons Nyanza iliangusha Maafande wa Kenya Army kwa seti 3-0 nayo Prisons Mombasa ilikung’utwa seti 3-0 na Equity Bank. Nayo Kenya Forest Service (KFS) iliandikisha ushindi wa seti 3-0 mbele ya Rift Valley Prison.

Wachezaji wa Trailblazers wanaokuja kivingine…Picha/JOHN KIMWERE

You can share this post!

Analenga kuibuka msanii mahiri nchini pia kuanzisha brandi...

Dereva Kimathi atarajia Croatia Rally

T L