• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 2:00 PM
IEBC: Ruto ataka Rais azime polisi

IEBC: Ruto ataka Rais azime polisi

STANLEY NGOTHO NA CHARLES WASONGA

NAIBU wa Rais, William Ruto sasa anamlilia Rais Uhuru Kenyatta akimtaka kuhakikisha uchaguzi wa Agosti 9 unakuwa huru na wa haki.

Dkt Ruto jana Jumamosi alimtaka Rais kuingilia kati na kuonya maafisa wa polisi dhidi ya ‘kutatiza’ maandalizi yanayofanywa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Kiongozi huyo wa Kenya Kwanza aliyekuwa akizungumza katika maeneo ya Namanga na Kitengela, Kaunti ya Kajiado, alidai serikali inatumia maafisa wa usalama kuvuruga maandalizi ya uchaguzi kwa lengo la kumfaa mpinzani wake mkuu, Raila Odinga wa Azimio la Umoja One Kenya.

“Bw Rais, hata kama wewe ni mwenyekiti wa Azimio, ni wajibu wako kufanikisha uchaguzi wa haki. Bw Rais usiruhusu polisi watumiwe kuvuruga uchaguzi. Usikubali nchi iharibikie mikononi mwako,” alisema Dkt Ruto.

Alionya kuwa kuna hatari ya kuahirishwa kwa uchaguzi iwapo maafisa wa polisi wataendelea kuhangaisha tume ya IEBC.

“(Rais) tafadhali ruhusu uchaguzi huru na haki ufanyike ilivyopangwa,” akasema Dkt Ruto.

Naibu Rais alidai kuwa kuna ushirikiano kati ya serikali na viongozi wa Azimio kuipiga vita IEBC na mwenyekiti wa tume hiyo Bw Wafula Chebukati, ‘baada yao kugundua kuwa watapoteza uchaguzi Agosti 9’.

“Washindani wetu wamegundua kuwa tutawashinda. Hii ndio maana wameanzisha vita na IEBC ili uchaguzi uahirishwe. Wakenya wako tayari kwa uchaguzi. Wapinzani wetu wajue hawashindani na IEBC bali wanashinda na sisi,” Dkt Ruto akaongeza, akishikilia kuwa Kenya Kwanza ina imani kubwa na IEBC.

Hii ni mara ya pili kwa Dkt Ruto kuonekana kuashiria kuwa huenda Rais Kenyatta akatumia mamlaka yake kumnyima ushindi.

Mnamo Machi 2022, alipokuwa katika eneo la Gatundu, Kaunti ya Kiambu, ambapo ni nyumbani kwa Rais Kenyatta, Naibu wa Rais alimtaka kiongozi wa nchi ‘kutomkata’ kwa kutumia kisu alichomsaidia kupata.

“Nina ujumbe ambao ninataka kuwapa nyinyi (wakazi wa Gatundu) mwende kumwambia rafiki yangu Rais Uhuru Kenyatta. Nendeni mkamwambie kwamba hata kama ameamua kuunga mkono Kitendawili (Raila), ninamsihi kwa unyenyekevu asitumie kisu nilichomsaidia kupata kunikata,” alisema Dkt Ruto.

Naibu Rais alisema hayo wakati malumbano yamechacha kati ya IEBC na polisi kuhusiana na kukamatwa kwa watu watatu, waliopatikana na vifaa vya uchaguzi katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Alhamisi.

Watatu hao, akiwemo raia wa Venezuela, walinaswa Alhamisi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi baada ya kuwasili kutoka London.

Bw Chebukati alitaja hatua ya polisi kuwakamata Bw Comarco Gregoria (raia wa Venezuela) na maafisa wawili wa kitengo cha teknolojia katika IEBC, kama njama ya “kuhangaisha maafisa wetu bila sababu”.

“Kukamatwa na kuzuiliwa kwa maafisa hao ambao ni maafisa wa kampuni ya Smartmatic International B.V iliyopewa kandarasi ya kuweka na kusimamia vifaa vya teknolojia kunaweza kulemaza maandalizi ya uchaguzi,” akaeleza kwenye taarifa.

  • Tags

You can share this post!

Apu zinazoongoza wakulima na wafugaji katika shughuli zao

WANTO WARUI: Mishahara ya walimu wa daraja la chini...

T L