• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 5:55 AM
BAHARI YA MAPENZI: Je, inafaa mke kushika hatamu nyumbani?

BAHARI YA MAPENZI: Je, inafaa mke kushika hatamu nyumbani?

SIZARINA HAMISI Na BENSON MATHEKA

HIVI karibuni nilipata nafasi ya kuzungumza na kijana ambaye anatarajia kufunga ndoa hivi karibuni. Swali langu kubwa kwake lilihusu jambo lililomvutia kwa mkewe mtarajiwa.

Yule kijana akanieleza kwamba pamoja na kwamba mkewe anavutia, anampenda na ni msomi ila jambo kubwa lililomvutia ni uwezo wake wa kujitegemea, kuishi nyumbani kwake, kujipangia majukumu muhimu katika maisha yake na hata kununua mahitaji ya msingi.

Nikamwuliza itakuwaje pale watakapoanza kuishi pamoja na iwapo anayo matarajio mkewe aendelee kutekeleza yale aliyokuwa akitekeleza kabla ya kufunga ndoa.

Ndiposa kijana akanijibu kwamba hayo ndio matarajio yake na zaidi.

Nikatambua kwamba baadhi ya wanaume wa kisasa, wanashindwa kutambua jukumu lao kubwa kama viongozi wa familia.

Kwamba sasa hivi kigezo kikubwa cha msichana kuolewa na kijana ni kuwa na uwezo wa kutafuta pesa, kutimiza majukumu kadha katika maisha na mengine ambayo awali yalikuwa ni ya mume.

Hali ya maisha imebadilika na siku hizi familia nyingi zimekuwa zikiongozwa na mke badala ya mume. Majukumu ya wanawake katika kazi na shughuli za kiuchumi yameongezeka, hali ambayo imepelekea baadhi ya wanaume kupunguza bidii katika wajibu wao wa kushika hatamu ya kuongoza na kuhudumia familia.

Akiwa binti, kawaida mwanamke huwa na wito wa kuangalia wazazi wake. Anapokuwa mke, anatarajiwa kumhudumia mumewe, kumtayarishia chakula, mavazi na mahitaji mengineyo na anapokuwa mama anakuwa na wajibu wa kushughulikia mahitaji ya watoto ikiwemo kuhakikisha wanapata elimu ipasavyo.

Lakini anapoingia kazini, anawajibika kuwa mwadilifu, mwenye nidhamu na mfanyakazi mzuri.

Katika jamii, mwanamke anatarajiwa ashiriki katika shughuli za kijamii na wakati mwingine kujitolea katika shughuli hizi. Kwa upande wa wanaume, kawaida jukumu lao kubwa ni kutunza familia na kukidhi mahitaji muhimu.

Hali ilivyo hivi sasa majukumu haya mara nyingi yanawahusisha wote, kwamba mume na mke inabidi kusaidiana katika kuhakikisha familia inakidhi mahitaji yake.

Kwa maana kwamba kuna utaratibu wa kugawana majukumu ambao wakati mwingine husababisha mmoja katika ndoa kuregarega ama kutelekeza jukumu lake na kumuachia mwingine sehemu kubwa ya majukumu.

Katika enzi hizi kusafisha nyumba, kuosha nguo na hata kupika sio kazi ya mwanamke pekee. Wakati mwingine kulingana na majukumu, wanaume wamekuwa wanasaidia. Halikadhalika wanawake pia hawana budi kusaidia waume zao pale inapobidi na wanapokuwa na uwezo wa kufanya hivyo. Ndoa na kuishi pamoja imekuwa ni kusaidiana.

Katika yote, tunaweza kusema mwanamume imara, anayehusiana vyema na nafsi yake, anayejitambua na kuelewa wajibu wake, hatishwi na uimara wala mafanikio ya mwanamke. Anapokuwa imara, huwa na uwezo wa kulipa gharama za kuhusiana na mwanamke yeyote, bila kujali mafanikio aliyonayo.

Ikiwa hivyo, hatapata shida kuelewa kuwa silaha pekee inayofaa ‘kumtawala’ mwanamke yeyote ikiwa ni pamoja na yule mwenye mafanikio, ni kumpenda kwa bidii na kumthamini kuliko chochote.

[email protected]

WAKATI wa harusi, wanandoa huwa wanaapiana kulindana kwa hali yoyote hadi kifo kiwatenganishe. Sijawahi kusikia kiapo cha ndoa kisichohusisha maneno haya.

Maneno mengine katika ndoa ni kuwa wawili wanapoungana kuwa kitu kimoja katika ndoa, huwa wanakuwa kitu kimoja kumaanisha kuwa kila mmoja, mume na mke, anafaa kuchukulia mwenzake kama sehemu yake na kusaidiana kwa kila hali.

Kusaidiana kunamaanisha kuwa mume na mke wanafaa kutekeleza majukumu muhimu ya ndoa kwa ushirikiano na kwa kuwa wao ni kitu kimoja, hakuna jukumu la mume na mke katika maisha yao. Nimesikia watu wengi wakikariri hili hasa wanawake wanapowataka waume zao kuwajibika kwa kuwasaidia katika kazi za nyumbani.

Ni haki yao kufanya hivyo kwa kuwa ni sehemu ya kiapo cha ndoa. Hata hivyo, hata mume akiingia jikoni kusaidia kupika au kupiga deki, hakuna kinachoweza kubadilisha nafasi yake ya kuwa kiongozi wa familia.

Kuna wanawake wanaomini kuwa faida ya mume ni wakati ana uwezo wa kukidhi mahitaji ya familia na wengi wamewaacha wanapopungukiwa na uwezo wa kifedha.

Katika karne hii ambayo dunia inakumbatia usawa wa jinsia, wanawake wanafaa kubadilisha mawazo na kushika hatamu za kukidhi mahitaji ya familia au kuzisimamia iwapo waume zao wameghafilika.

Kasumba ya baadhi ya wanawake kwamba hawawezi kulisha mwanamume mwenye ndevu asiye kaka yao wa kuzaliwa inatokana na imani ya zama za kale wakati mababu hawakuwa wameelimika.

Ningetaka kufafanua kuwa kushika hatamu za kukidhi mahitaji ya familia hakupatii mke kibali cha kumdharau mumewe.

Wanafaa kufahamu kwamba kufanya hivyo sio hisani kwa mume mbali ni kutekeleza mojawapo wa majukumu yao katika ndoa na kiapo cha ndoa.

Wanawake wamekuwa wakipigania usawa wa jinsia na hawawezi kujitenga na uwajibikaji kikamilifu katika ndoa zao. Nimeona wengi wasio na waume ambao wana familia zinazonawiri wakikosoa dhana kwamba mwanamke hawezi au hafai kuendesha familia.

Kuna wanawake waliobahatika kupata mali kuliko kaka zao au waliosoma ambao wamekuwa wakisimamia shughuli za familia wanazotoka. Je, inamaanisha mwanamke akifanikiwa kuliko kaka zake atelekeze familia yake kwa kuwa ni mwanamke?

Wanaume wanaozuia dada zao kukohoa katika familia, wanaishi karne za mababu wao na wanafaa kukubali ukweli wa maisha ya kizazi cha sasa. Na hapa narudia kusema kuwa wanawake wanapojaliwa kuwa na usemi katika familia hawafai kudharau kaka zao. Heshima sio utumwa.

Waume nao wanafaa kuwaheshimu wake zao wanapowajibikia jukumu hili na kuwaunga mkono kwa kuwa msingi wa ndoa ni kushauriana na kusaidiana. Ajabu ni kwamba msingi huu huwa unazikwa kwenye kaburi la sahau punde tu baada ya wanandoa kubadilisha viapo vya ndoa.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Utaratibu uliofuatwa kabla ya kutangaza kifo cha Malkia...

Uswahilini sihami, niende wapi na ndo nimeshafika!

T L