• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:50 AM
BAHARI YA MAPENZI: Mdada pia ana haki ya kumrushia chali mistari

BAHARI YA MAPENZI: Mdada pia ana haki ya kumrushia chali mistari

NA BENSON MATHEKA

KUNA kanuni isiyopatikana katika vitabu vya sheria na pengine vya kidini kwamba ni mwanamume anayepaswa kurushia mwanamke mistari ya mapenzi.

Kanuni hii hasa miongoni mwa jamii nyingi za kiafrika, imefanya wanawake kusononeka kwa kubeba hisia za mapenzi kuhusu wanaume huku wakiogopa kuwarushia chambo.

Dhana ambayo imejikita kwa miaka mingi ni kwamba mwanamke anayetongoza mwanamume anachukuliwa kuwa amepotoka kimaadili. Wasio na hekima ya kupima maneno huwa wanasema kwamba wanawake kama hao ni makahaba.

Hii imenyima wanawake haki yao ya kuelezea wanaume wakiwapenda na kutamani burudani kutoka kwao. Lakini ni dhana ambayo haina mashiko iliyonuiwa kuwanyima wanawake haki ya kueleza hisia zao za kimapenzi kwa wanaume.

Ni dhana iliyonuiwa kuwadhalilisha waonekane duni kuliko wanaume. Wawe viumbe wasio na sauti katika masuala ya mapenzi. Mwanamke ana hisia za kimapenzi kama mwanamume na ana haki ya kuelezea mwanamume yeyote anavyohisi kumhusu.

Hakuna makosa na hawafai kuogopa kufanya hivyo kwa kuhofia jinsi jamii itawachukulia. Hisia za mapenzi ni za mtu binafsi na sio za jamii.

Hakuna haja ya mwanadada kuteseka akiogopa kumweleza mwanamume kwamba anampenda na angetaka amkate kiu kwa kumlisha uroda.
Ingawa ulimwengu umebadilika, wanawake wengi wanaotongoza wanaume huwa wanafanya hivyo wakiwa tayari kwa lolote.

Ni hali ambayo inawaandama hata katika ndoa huku baadhi wakiogopa kudai haki yao ya tendo la ndoa kutoka kwa wanaume hao ili wasiwachukulie vibaya.

Unapata mwanamke aliye katika ndoa akiumia kwa kutamani burudani lakini anasubiri hadi mumewe atakapotamani uroda ili akate kiu. Huu ni utumwa wa mapenzi ambao wanawake wanapaswa kuupiga teke katika mawazo yao, wajivike ujasiri na kudai haki yao kutoka kwa wanaume wao.

Nao wanaume ambao wangali na kasumba ya kuchukulia wanawake kama vyombo vyao ya ngono wanapaswa kustaarabika na kukubali kwamba akina dada wana mili na hisia kama zao zinazohitaji kushughulikiwa na ni wao wanaojua vyema mili yao na wanapohitaji kushughulikiwa.

Uhusiano unaojengwa kwa msingi wa kutamaniana na kushughulikiana huwa na upekee wake kwa kuwa hakuna anayehisi kutothminiwa na kupuuzwa.

Kwa hakika, mwanamume aliye na mpenzi anayemtongoza anafaa kujivuna kwa kuwa na mchumba anayetambua maana halisi ya uhusiano wa kimapenzi ambao unahusisha watu wawili wanaopaswa kuburudishana na kuridhishana.

Kitu ambacho wanaume wasiochangamkia tabia ya akina dada ya kuwatongoza hawafahamu ni kwamba huwa wanawasukuma mbali na kuweka pengo kati yao linaloweza kupanuka na hatimaye kusambaratisha uhusiano.

Hii ni kwa sababu mwanamke huwa anashuku mpenzi asiyemchangamkia anapomhitaji au kuhisi kutothaminiwa. Mapenzi hayawezi kuhusisha mtu mmoja na kwa hivyo, kila mhusika katika uhusiano anapaswa kuwa na haki ya kutamani burudani kutoka kwa mwenzake bila vizingiti na hofu.

Hili halipaswi kuwa tatizo iwapo wapenzi wanawasiliana vyema kwa kuwa palipo na mawasiliano, kila kitu huwa ni mteremko. Palipo na mawasiliano, mume huwa anajua wakati mke anahitaji haki yake na pia mke anajua wakati mume anahitaji kudekezwa. Hii ndiyo raha ya uhusiano thabiti wa mapenzi, kutongozana.

  • Tags

You can share this post!

PENZI LA KIJANJA: Urembo ni bonasi, gharimikia uhusiano

Majangili wazua hofu bila kujali wanajeshi

T L