• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 9:50 AM
BAHARI YA MAPENZI: Tabia za wazazi hufuata watoto wao hata katika ndoa

BAHARI YA MAPENZI: Tabia za wazazi hufuata watoto wao hata katika ndoa

NA BENSON MATHEKA

MSEMO kwamba mtoto wa simba ni simba unaweza kuwa na tafsiri nyingi kwa muktadha unaotumiwa.

Katika masuala ya mahusiano ya mapenzi unaafiki kwamba mtu anaweza kuiga tabia za wazazi au mmoja wa wazazi wake.

Ni kawaida kusikia mtu akisema au akisemwa kuwa ana hulka za mama au baba yake au akitaja aliyojifunza kutoka kwa wazazi au mmoja wa wazazi wake akiwa mdogo.

Hii ina maana kwamba tabia ambazo mtu hushuhudia kwa wazazi katika utoto wake huwa zinachangia uhusiano wake wa kimapenzi utakavyokuwa akiwa mtu mzima.

Mwanadada anayekua akiona mama yake akimheshimu na kumthamini baba yake anaweza kuwa na ndoa thabiti kuliko anayekua akishuhudia mama yake akidharau baba yake.

Ni rahisi kwa mwanamume anayekua katika mazingira ambayo wazazi wake hugombana na kupigana kuiga tabia hizo na kufanya maisha ya ndoa kuwa jehanamu kwa mkewe.

Hali ni sawa kwa mtu aliyekua akiona baba yake akimuacha mama yake kwa upweke kwenda kulewa hadi usiku wa manane au kushiriki michepuko kwa siku kadhaa.

Ni jambo lisilopingika kwamba tabia za wazazi zimefanya watu kuchukia ndoa. Unasikia mwanadada akisema hawezi kuolewa ili asipitie aliyoona mama yake akipitia katika mikono ya baba yake.

Unaweza pia kusikia mwanamume akisema alichukia ndoa kwa sababu ya aliyoshuhudia mama yake akimtendea babake. Hii ni mifano tu ya yale ambayo watoto huweza kuiga kutoka kwa wazazi.

Kuna chanzo cha hali hiyo ambacho huenda hawakifahamu na wanapokifahamu huwa ni katika mazingira yasiyopendeza na ambayo huchangia mtizamo wao kuhusu ndoa.

Viwango vya uhusiano vya wazazi huchangia pakubwa mtizamo wa watoto wao kuhusu taasisi hii muhimu kwa uendelevu wa maisha ya binadamu.

Wazazi wanaoonyeshana upendo wa hali ya juu huwa wanajenga msingi sawa kwa watoto wao kwa kuwa nao huwa wanaiga na kukumbatia tabia zao.

Ni rahisi kwa mwananume kukubali kupeleka mkewe likizo iwapo babake alikuwa akifanyia mama yake hivyo kinyume na aliyekuwa akisikia babake akinguruma na kuambia mama yake kwamba kufanya hivyo ni kuharibu pesa.

Ni rahisi pia kwa mtu aliyekua akishuhudia wazazi wake wakiandamana kwenda kazini kufanya hivyo katika ndoa yake.

Hivyo basi, ni muhimu kwa mtu kudadisi aliyopitia mchumba wake katika utoto wake kabla ya kukata kauli kuingia katika ndoa.

Inaweza kuchukua muda kwa kuwa sio rahisi mtu kufunguka kuhusu tabia za wazazi wake mapema katika uhusiano wa kimapenzi.

Kuna wanaofanya hivyo wakisifu wanachodhani wazazi walikuwa na tabia chanya kwao lakini mtazamo wao unaishia kuwa hasi kwa uhusiano wao na wapenzi wao.

Hata hivyo, mtu anapofunguka, huwa anatoa nafasi ya kujua maoni ya mpenzi wake kuhusu aliyojifunza kutoka kwa wazazi wake.

Ndoa huwa ni kati ya watu wawili ambao wanaweza kusaidiana kupiga teke hulka hasi walizojifunza kutoka kwa wazazi wao na kujengea watoto wao msingi bora wa uhusiano wa kimapenzi.

Hii haiwezi kufanyika mtu akishikilia kuwa hawezi kuacha aliyojifunza au kufunzwa na mzazi wake.

  • Tags

You can share this post!

‘Maandamano yetu si ya fujo’

Wandani wa Ruto walia kuachwa nje ya teuzi mbalimbali...

T L