• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
HII IMEENDA: Mtimkaji Mary Moraa atoka sokoni

HII IMEENDA: Mtimkaji Mary Moraa atoka sokoni

NA AYUMBA AYODI

HAKUJUA kile ambacho kilikuwa kikimsuburi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) baada ya kuwasili kutoka Prefontaine Classic Diamond League, Oregon, Marekani mnamo Jumanne usiku.

Alipokuwa akisubiri pamoja na wenzake apite katika eneo la kutoa mizigo uwanjani humo, mpenzi wake naye alikuwa amejihami akimsubiri ili awasilishe posa eneo la kuondoka JKIA.

Wakati ambapo wasafiri wengine waliruhusiwa waondoke eneo la kuondoa mizigo, watimkaji wengine wa hapa nchini, walizuiwa kuondoka. Kulikuwa na shida kidogo na kila mmoja wao alikuwa akiujiuliza ni kitu gani kinafanyika.

Mwanaume ambaye alikuwa afike akiwa na pete naye hakuwa amewasili na mpango wote ambao ulikuwa umewekwa kwa siri, ungeporomoka iwapo wangeondoka. Mwishowe Richard Lagat aliachilia pumzi baada ya kuletewa pete.

Ni watu wachache ndio walifahamu kile ambacho Lagat alikuwa akilenga. Moraa na watimkaji wengine waliporuhusiwa waondoke, alimpata Lagat akiwa amepiga magoti akiwa na pete mkononi akiwa tayari kumvisha.

Hivyo, ndivyo Moraa, bingwa wa mbio za mita 800 kwenye Jumuiya ya Madola aliondoka ‘sokoni’ badala ya kumridhia Lagat awe mchumba wake. Kando na pete, Lagat alikuwa na bango lililoandikwa ‘Utakubali nikuoe?’

Bw Richard Lagat akimposa mwanariadha Mary Moraa. PICHA | CHRIS OMOLLO

Moraa ambaye pia ni bingwa 2022 Diamond League alikubali posa hiyo na baada ya kuvalishwa pete, walikumbatia huku wanahabari na wakimbiaji wengine wakipiga vifijo na nderemo.

 “Maneno hayawezi yakaeleza jinsi ambavyo ninahisi kwa sasa. Nimefurahi mno na huu utakuwa usiku wenye furaha riboribo,” akasema.

“Wale ambao walikuwa wananimezea mate wafahamu kuwa sasa nimeenda. Kwa kweli sikutarajia haya na nilifikiria ni mapokezi ya kawaida tu. Nimefurahi,” akaongeza.

Lagat ambaye ni kocha wa voliboli na aliyewahi kuchezea kikosi cha GSU, alisema walikutana na Moraa mnamo 2021 na mapenzi kati yao yakaanza. Walikutana wakati wa kufuzu kwa majeshi katika kambi ya Embakasi.

“Nimefurahi alisema ndio. Ni msichana mzuri, mrembo na anayependa sana kusakata densi,” akasema Lagat, akiwa amefurahi kuwa hakuangushwa.

Lagat ambaye anatoka Kapsabet, Kaunti ya Nandi alimiminia sifa mpenzi wake kutokana na jinsi alivyotamba msimu huu na kusema ana matarajio ataendelea kufanikiwa.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi waachwa gizani kwa saa 4 Al-Shabaab wakiharibu mnara...

Watunzaji makaburi ya Lang’ata wagoma

T L