• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Jinsi wazungu weusi wanavyotesa ‘ushago’

Jinsi wazungu weusi wanavyotesa ‘ushago’

NA MWANGI MUIRURI

BAADHI ya wenyeji waliozoea maisha ya mashambani wameshikilia kuwa ni mwiko kwao kuanika kijivazi cha ndani kwa kamba kionekane hadharani na watu pale nyumbani.

Ni malalamishi ambayo wanavijiji wameweka wazi kuhusu hali halisi mashinani wakipiga stori na wakiwa kwenye mahojiano na vituo vya redio vya lugha ya Gikuyu.

Wamedai kuwa msimu huu wa Krismasi, wanadada wengi waliosafiri kutoka mijini kula Krismasi ushago, wana ujasiri wa kuanika kile kijivazi cha ndani kwa kamba nje penye hata wazee wanapitia.

“Haya ni maajabu kwa sababu huku vijijini kile kijivazi cha ndani ni cha kisiri na huanikwa mbali na umma. Binafsi mimi ninaanika ndani ya nyumba sehemu yenye joto na wakati mwingine ninaficha kwa kutumia shuka,” akasema Bi Lucia Mbogo.

Alisema kwamba sababu nyingine ya kuanika kiujanja ni kwamba ukianika pahala wazi, wezi hupita na kijivazi hicho muhimu.

Hata hivyo, vituo vya redio kwenye mijadala mikali vimeambiwa kwamba wageni kutoka mijini wanabeba chupi zao hadharani sawa na jinsi ambavyo wanakijiji hubeba vitambaa vya kupangusia pua wanapokuwa na mafua au kwa usafi wa aina nyingine.

Shida nyingine mashinani msimu huu, ni wanadada kuvaa nguo kwa njia ambayo chupi inajitokeza nyuma kwa kiuno na pia kuvaa nguo za kubana kiasi kwamba wanaume wa mashinani wanageuka kuingiwa na pepo wa kuwafanya wawamezee mate kupindukia.

“Hata wanaume wengine wa mijini wanavaa kama wanawake. Wamesuka nywele na kutoboa masikio huku wengine hata wakituomba marinda wavalie ili wajipige picha na video waweke kwa mitandao ya kijamii,” akalia Bi Susan Kariuki.

Cha kuwatia wasiwasi kabisa, Bw Wanjohi wa Nyeri akateta kupitia Coro FM, ni jinsi ambavyo baadhi ya wanawake kutoka mijini wanawafungulia roho wanaume walioko mashinani, nao wanaume wa mijini waliojaajaa ‘ushago’ wakitupa chambo kuwanasa wanawake wa vijijini.

Kuna mwenye duka aliyejitambulisha kama David Kairia aliyeshauri kwamba “ambieni hawa wazungu weusi kwamba huku mashambani tunauza mipira ya kondomu kwa heshima ya kuiweka siri”.

“Nimewasikia vijana wa kiume wanafika dukani na kwa sauti za juu kukiwa na wateja wengine wakiwa wazee, wanapayuka wakiagiza kondomu,” akasema Bw Kairia.

Alisema kwamba inabidi mwenye duka aseme hana hata ikiwa iko.

Tabia nyingine za hao wa mijini ni zile za kukumbatiana hadharani hasa wake na wanaume ikizingatiwa kuwa hizo huwa tu ni salamu kanisani zikikubalika sanasana kati ya jinsia ya kike.

“Lakini hawa wanakumbatia kila mtu na wanatujongea kwa njia za kututoa jasho. Msichana aliyekomaa viungo anakurukia ukiwa mwanamume na anajifinya kwa mwili wako eti ni salamu kiasi cha akikuachilia umechanganyikiwa na kuwa mdhaifu kwa magoti,” akalalama mchangiaji mwingine mwingine kutoka Gatanga.

Tabia nyingine ni hao wa vijiji kukataa kutoka nje kuenda haja ndogo na kubwa kwa choo za kuchimbwa mbali na nyumba.

“Wanakataa kwenda nje wakiamua kujisaidia kwa karai na ndoo… Halafu wanataka sisi wa vijijini tuende tukamwage uchafu huo eti wanaogopa giza huku mashambani. Wanakataa tuzime taa usiku tukilala eti wanaogopa na wanajua gharama ya mafuta taa imepanda,” akalalamika mwingine.

Aidha, wengine wanateta kwamba watu wa mijini hasa vijana wa kiume, wako na tabia za kulia ovyoovyo pasipo kujua kwamba mashinani machozi ya mwanamume hufichwa kama bangi.

“Unapata mwanamume mkubwa amepigiwa simu na watu anaita beib kwa simu na unapata anaangua kilio eti ni mapenzi…huku vitu kama hivyo havikubaliki,” akateta Mzee Mwaura Wa Ngigi akipiga simu kutoka Mai Mahiu.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Wasioamini Mungu wakubaliana na Papa kubariki mashoga

Ndindi Nyoro asuta Jubilee kwa kutishia kumng’oa Ruto

T L