• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 6:50 AM
KIKOLEZO: Utamu wa chai si rangi!

KIKOLEZO: Utamu wa chai si rangi!

Na THOMAS MATIKO

KATIKA kipindi hiki kigumu cha corona mastaa wengi nchini hasa waliokuwa kwenye ndoa na mahusiano, wamejikuta katika vipindi vigumu.

Ingawaje wengi wao wameamua kutofunguka ukweli uliochangia ndoa na mahusiano yao kuvunjika, msoto umetajwa kama chanzo.

DADDY OWEN

Sakata ya mwanamuziki wa injili Daddy Owen kutorokwa na mke wake wa miaka minne Farida Wambui ilichipuka Januari 2021.

Madai ni kuwa Farida alikutana na tajiri mmoja anayeishi Gilgil na ndiye alimshawishi kuachana na jamaa ambaye kipindi hicho alikuwa akipitia ugumu kifedha.

Hadi leo, Daddy Owen amechagua kutozungumzia sababu kamili za kuachwa kwenye mataa na mwanamke aliyemwita mke kwa miaka minne.

Ila stori za vijiweni zinadai kuwa, corona ilipokatiza njia zake za kuingiza mtaji, ndipo mtoto wa watu aliona hatavumilia shida baada ya tajiri kujitokeza na kupita naye.

KELVIN ‘SHANIQWA’ MUNGAI

Kuna kipindi Shaniqwa alikuwa ndiye habari za mjini.

Stesheni kibao zilimpa dili ya kupeperusha komedi yake iliyowabamba wengi enzi hiyo ambayo sio zamani sana.Lakini taratibu jamaa alitoweka kwenye rada.

Sasa kafunguka na kusema kuwa, baada ya kupoteza kazi alipochujwa kwenye kipindi cha TV alichokuwa akiigiza, mke wake naye akamtoka.

Anakiri kushindwa kuendelea kutoa pesa za matumizi alipopoteza kazi na hapo ndipo alianza kuziona kucha za mkewe.

“Mke wangu alianza kunichepukia. Ikawa sasa ananiachia mtoto, yeye anakwenda kuhanya. Nakumbuka kuna siku tumelala njaa wakati kwenye Mpesa alikuwa na Sh8,000,” kafunguka.

Alipokuja kugundua anavyochezwa, jamaa aligeukia ulevi wa kupindukia. Hata hivyo anawashukuru marafiki zake wachekeshaji Desagu na Jalang’o kwa kuweza kumsapoti kifedha kwa miezi kadhaa.

DJ CREME DE LA CREME

Vyuma vilipokaza na shoo kupungua mapema mwaka huu 2021, DJ Creme aliyekuwa ameishi Nairobi kwa miaka 17, aliamua kuihamisha familia yake hadi kijijini kwao Kericho.

DJ Creme aliondoka na mkewe pamoja na watoto wao wawili na kwenda kuanzisha maisha ya ukulima. Julai 2021 baada ya kuwa na mkewe kwa miaka 14, jamaa alitibua kuwa wameachana.

Hivi majuzi alikiri kuwa ni kweli wametengena ila akasisitiza hawakuachana kwa sababu ya msoto na kwamba ni kutokana na tofauti ya kimitazamo kuhusu maisha.

DJ Creme anasisitiza kuwa alikutana na mkewe akiwa hana chochote hivyo msoto si chanzo cha wao kutengana.

Hata hivyo wanazengo mitandaoni wanahisi suala la mkwanja litakuwa limechangia ikizingatiwa kuwa alianza kwa kuhamishia familia kijijini na kisha miezi michache baadaye, wakaachana kwani nchi bado ilikuwa kwenye ‘lockdown’.

MEJJA KHADIJA

Baada ya kudumu kwenye ndoa kwa miaka mitano, siku moja Mejja alirejea nyumbani kwake Thika na kumkuta mkewe hayupo.

Hawakuwa wamegombana na wala hakukuwa na tatizo. Alipojaribu kumpigia simu akitaka kufahamu aliko, mke wake alimtumia ujumbe akimtakia kila la kheri.

Aidha alimshauri kuendelea na maisha yake bila ya kumuwaza.

Tukio hilo lilitokea Disemba 2020.

Baadaye Mejja alifunguka na kudai kuwa kwa muda mrefu walikuwa na mzozo kuhusu mustakabala wa maisha yao.

Mke wake alikuwa na ari ya kwenda majuu kusaka ajira huku yeye akiwa anapinga.

Inawezekana ishu hiyo ya riziki ilichangia pakubwa ndoa yao kuvunjika.

You can share this post!

Ghulamu mtukutu apiganisha wazazi

Wafugaji sasa walia kupunjwa na serikali

T L