• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 2:59 PM
Wafugaji sasa walia kupunjwa na serikali

Wafugaji sasa walia kupunjwa na serikali

Na STEPHEN ODUOR

WAFUGAJI katika Kaunti ya Tana River, wamelalamika wakisema kuna masharti makali yaliyoekwa na serikali katika mpango wa kununua mifugo wanaoathiriwa na ukame.

Wafugaji hao wamesema kuwa, ni vigumu kutimiza masharti ya kiwanda cha kitaifa cha nyama (KMC) kwani karibu mifugo wote wamepunguza uzani.

KMC ilikuwa imetoa hitaji, ng’ombe wasiwe chini ya kilo 150 ndipo serikali iwanunue ili kuepushia wafugaji hasara.

“Haitakuwa rahisi. Nimepoteza ng’ombe zaidi ya 20 kwa ukame na yule mzito zaidi niliyebakisha ana uzani wa kilo 138,” akasema Abdirahman Bile, mmoja wa wafugaji.

Alisema ingawa serikali ya kaunti ilikuwa imeingilia kati kuwapa misaada ya lishe ya mifugo, msaada huo haukutosha na sasa amelazimika kuuza kondoo ili akatafute lishe ya ng’ombe kwingine.

Kulingana naye, kama kweli serikali imejitolea kusaidia wafugaji, itakuwa vyema sharti hilo la uzani liangaziwe upya.

Serikali ilikuwa imenuia kununua ng’ombe 788 katika Kaunti ya Tana River chini ya mpango huo wa kuepushia wafugaji hasara wakati wa ukame.

Wafugaji kutoka kaunti ndogo tatu walitarajiwa kuuza ng’ombe 250 kila kaunti ndogo.

Mpango huo unaendelezwa katika kaunti nyingine nchini ambapo kuna idadi kubwa ya wafugaji lakini malalamishi sawa na hayo yamekuwa yakitolewa.

Kamishna wa Kaunti ya Tana River, Bw Mbogai Rioba, alikiri mpango huo haujashika kasi eneo hilo kwa sababu wafugaji bado wanajitahidi kutimiza masharti yanayotakikana.

Kulingana naye, ni wafugaji wawili pekee katika kaunti hiyo ambao wamefanikiwa kuuzia KMC mifugo wao baada ya kutimiza masharti.

“Sisi hatuamui kuhusu masharti. Huwa tunayapokea kutoka kwa KMC kisha tuwasilishe kwa wafugaji, lakini tuna imani wengine wengi watatimiza masharti hayo siku za usoni,” akasema.

Mfugaji mwingine, Bw Ibrahim Salat, alisema uzani unaohitajika kwao si haki na unasababisha matatizo kwa wafugaji ambao tayari wamepoteza mifugo wengi kwa ukame.

Bw Salat alisema wanahisi kama serikali inawakejeli wafugaji kwani walitarajia kusaidiwa ilhali wanaona ni kama serikali inafanyia biashara mahangaiko yao.

“Inamaanisha kuwa, kama ng’ombe wetu hawafitimizi masharti yanayohitajika, serikali itaenda kununua kwingine na ng’ombe wetu wataachwa waangamie,” akasema.

Zaidi ya hayo, walilalamikia bei ya KMC na kusema ni ya chini mno ilhali wanalazimishwa kupeana ng’ombe walionawiri.

KMC imenuia kununua kila ng’ombe kwa Sh20,000 bei ambayo wafugaji wanasema ni chini ya ile ambayo huwa wanauza mifugo wao wakati kunapokuwa na janga.

Wamehimiza serikali ipunguze masharti yake na iongeze bei ya kununua mifugo kwa manufaa ya wananchi.

You can share this post!

KIKOLEZO: Utamu wa chai si rangi!

‘Mageuzi’ Kemsa yapata pingamizi

T L