• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:55 AM
Msanii aliyeonja kifungo bila hatia aendeleza mahamasisho ya amani

Msanii aliyeonja kifungo bila hatia aendeleza mahamasisho ya amani

NA LABAAN SHABAAN

KILA anapofurahia uhuru wake, yeye huMshukuru Mwenyezi Mungu na kumuomba hekima asije akajipata tena rumande ama kufungwa gerezani.

Anasema alionja kifungo licha ya kwamba hakuwa na hatia yoyote.

“Hakika jela si pahala  pazuri. Kula, kulala na kurauka ni mapema. Nyuma ya kuta hizi nimejifunza mengi. Maisha yalikuwa magumu ya kushambuliwa na kunguni na wadudu huku siku nazo zikiganda bila kusonga katika mazingira magumu ya rumande,” hii kauli yake inatokana na kipande cha mmojawapo wa nyimbo ambazo ametunga msanii John Kasyula almaarufu Kaploti Mwenyewe.

Kaploti Mwenyewe ni mwimbaji wa nyimbo za kizazi kipya ambaye aliselelea miaka mitano katika jela yenye ulinzi mkali ya Kamiti na ile ya Industrial Area.

Anasimulia kwa huzuni jinsi alivyoona miaka mitano ya maisha yake ikigeuzwa muda aliopoteza kwa sababu alitupwa ndani kwa tuhuma za mauaji.

“Nilijikuta gerezani kutokana na tukio ambapo niliwakuta wezi wakimwibia mkazi wa Kayole usiku nje ya duka langu la biashara jijini Nairobi. Niliona wanaharibu sifa ya eneo la biashara yangu,” anaeleza Kaploti Mwenyewe akidokeza ulikuwa usiku wa manane akitoka kutumbuiza kwenye maeneo ya burudani.

Akaongeza: “Kisa changu kinaelezwa na msemo mtego wa panya huingia waliomo na wasiokuwemo. Nilijaribu kuwazuia majambazi wasifanye uhalifu huo kwa mwathiriwa huyo… kumbe nilijitia motoni.”

Msanii huyo anaambia Taifa Leo kuwa mwathiriwa aliyeshambuliwa na kuibiwa alidungwa kisu na baadaye akaaga dunia wakati akitibiwa hospitalini.

Anakumbuka kuwa polisi waliokuwa wanashika doria waliwafumania na kuwakamata wote wanne na kuwaweka korokoroni.

“Ni mimi peke yake ambaye nilifikishwa mahakamani na baadaye kufungwa jela. Wahalifu wale walihonga maafisa wa polisi na kuachiliwa huru,” anafunguka.

Anasema hakuwa na wakili.

“Naamini ningekuwa na wakili ningesaidika sana ila umaskini na kukosa hela vilichangia mimi kutopata haki. Hali hii, huwakumba sana vijana wa vitongoji duni jijini kwa sababu haki katika mahakama ni adimu sana kwao kwa kutojua sheria,” anaongeza.

Maisha ya jela na muziki

Kaploti Mwenyewe alifanya kesi akiwa rumande kwa miaka mitano baada ya kushindwa kujitetea na kukosa ufahamu wa mchakato wa kupata haki lakini baada ya kukosekana ushahidi kwamba alikuwa mhalifu, aliachiliwa huru mwaka 2017.

Kwa mujibu wa msanii huyu, familia yake iliyoishi maisha ya uchochole ilijawa na majonzi na hapo ndipo baba yake aliwezwa na kuwa mlevi kupindukia.

Akiwa nondoni saa za jioni Kaploti Mwenyewe alikuwa anatumbuiza wafungwa wenzake kwa muziki ambapo walitumia vijiko na ndoo kama ala za muziki.

“Mashairi na muziki ninaotunga huwa ni ya uhalisia wa maisha tunayoishi. Msukumo wangu ni kuhamasisha jamii na kuwa kioo cha jamii,” anasema.

Tangu milango ya gereza imuone mgongo, msanii huyu amekuwa akizuru takriban magereza na shule 200 kwa mwaka kupitia mpango wake wa ‘Mfungwa ni Binadamu Initiative’.

Msanii John Kasyula almaarufu Kaploti Mwenyewe apozi kupigwa picha alipozuru gereza la Kamiti kuzungumza na wafungwa. PICHA | LABAAN SHABAAN

Katika mpango huo, anashirikisha mtangazaji King Kafu ambaye pia aliwahi kufungwa jela kwa kosa la ujambazi.

Wao hutumia mradi huu kutoa mafunzo ya maisha kwa wafungwa pamoja na kukuza talanta zao.

Mmoja wa waliorekebisha tabia akizoa taka mtaani Kayole baada ya kuhamasishwa na msanii John Kasyula almaarufu Kaploti Mwenyewe. PICHA | LABAAN SHABAAN

“Kuna kundi kubwa la wapigaji ngeta wa zamani ambao leo hii ni wema na wanajihusisha na uzoaji taka Kayole,” anasema.

“Kuna kundi la vijana waliacha uhalifu kupitia kazi yangu na leo ni waigizaji,” akaongeza.

Msanii John Kasyula almaarufu Kaploti Mwenyewe akiwa na afisa wa gereza baada ya kuhamasisha wafungwa katika Gereza la Kamiti. PICHA | LABAAN SHABAAN

Ili angaa kujikimu kimaisha, Kaploti Mwenyewe hushirikiana na mashirika mbalimbali kufadhili mipango hii magerezani, shuleni na katika mitaa.

Kadhalika, kazi yake ya usanii pia humtegea hela kwa sababu anapoimba katika hafla mbalimbali, hulipwa.

Msanii John Kasyula almaarufu Kaploti Mwenyewe akiwapa motisha wanafunzi wa shule mojawapo ya msingi jijini Nairobi. PICHA | LABAAN SHABAAN
  • Tags

You can share this post!

Msizungumze na wanahabari bila idhini, Sakaja aonya maafisa...

Krismasi: Wafugaji kuku waripoti kuongezeka kwa visa vya...

T L