• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 6:55 PM
Sammy G avuna matunda ya ‘challenge’ Guardian Angel akikubali kolabo

Sammy G avuna matunda ya ‘challenge’ Guardian Angel akikubali kolabo

NA LABAAN SHABAAN

KIJANA Sammy G K mwenye hamu na kiu ya kukua katika tasnia ya burudani ameanza kuona matunda ya kufanya challenge ya wimbo wa ‘Nimependa‘ wa wasanii Deus Derick na Guardian Angel.

Kijana akiwa na vidude vya masikioni alifanya majaribio ya kuimba wimbo huo, bila kujua hatua hiyo ingemkatia tiketi ya kukutana na wasanii hao anaowaonea fahari.

Mwanafunzi huyo wa Kidato cha Nne alipiga challenge katika jukwaa la mtangazaji wa matukio ya burudani Presenter Kai na video hiyo ikasambaa kwenye majukwaa ya mtandaoni kama moto wa jangwani.

Kwa muda mfupi zaidi ikawafikia Derick na Guardian.

“Niliona video hii sana na nilitumiwa na watu wengi sana hata nikajaribu kupuuza,” Guardian alisema akiongeza kuwa watu walipozidi kumshinikiza, akawa hana budi ila kukutana na kijana Sammy G ili amsaidie kuimarika kimuziki.

Bingwa wa nyimbo za injili Guardian Angel aliyeamini kuwa Sammy G atakuwa mwimbaji maarufu baada ya kupigwa jeki naye, amemsihi mvulana huyo kuwa mnyenyekevu na mcha Mungu ili azidi kuinuka katika tasnia ya muziki.

Deus Derick naye alimrai Sammy G asisahau alikotoka kwa sababu ya kupata umaarufu, akisisitiza umuhimu wa mihimili iliyomshikilia katika sekta ya muziki.

“Pia mimi Guardian Angel alinisaidia na hadi sasa sijamsahau. Na ninakumbuka tulipoachia kolabo naye ya wimbo ‘Nimependa’ iliishia kuwa hiti moja kali na kiukweli hilo linafanya niwe na furaha sana,” akasema Derick katika kikao cha kurekodi remix ya kolabo hiyo.

Walipokuwa wanapiga gumzo kabla ya kuingia studioni Guardian Angel alikiri kuwa nyimbo zake za kwanza zilirekodiwa bila malipo na alikuwa tayari kumpa sapoti chipukizi Sammy G kwa kufadhili kurekodi kolabo naye pamoja na video.

Challenge ya kibao ‘Nimependa’ ilivuna ufuasi wa mamia ya maelfu mitandaoni huku watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii wakisambaza video hadi ikamfikia Guardian Angel ambaye sasa majazi ya jina lake yakipata maana kamili ambapo sasa anakuwa malaika kwa Sammy G.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi mrembo Patricia Muthoni alivyoongeza ladha kwenye...

Ulinzi Starlets watandika Vihiga Queens na kutetea ubingwa...

T L