• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 7:50 AM
Ulinzi Starlets watandika Vihiga Queens na kutetea ubingwa wa kombe la wanawake la Super

Ulinzi Starlets watandika Vihiga Queens na kutetea ubingwa wa kombe la wanawake la Super

NA TOTO AREGE

ULINZI Starlets wametetea kombe la wanawake la Super baada ya kuwabwaga Vihiga Queens 2-0 katika fainali mnamo Jumamosi uwanjani Kenya Utalii College jijini Nairobi.

Fainali ya kombe hilo ilikutanisha mabingwa wa kombe la Super ambao ni Ulinzi na mabingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Shirikisho la Soka nchini (FKF-WPL) Vihiga.

Wanajeshi hao sasa wametwaa kombe hilo kwa mara ya pili.

Katika makala ya kwanza mwaka 2021, walishinda kombe hilo baada ya kuinyorosha Thika Queens ambayo sasa ni Kenya Police Bullets kupitia penalti ambapo walizoa ushindi wa 11-10 katika uwanja uo huo.

Jumamosi, Ulinzi wameonyesha ubabe wao kwa mara nyingine ambapo wamepata bao la kwanza katika dakika ya 40 kupitia mshambulizi Joy Kinglady baada ya kuunganisha pasi ya kiungo matata Cindy Ngairah na kuwafanya kuongoza kipindi cha kwanza.

Kabla ya kipindi cha pili kun’goa nanga, Vihiga walifanya mabadiliko mawili kwa mpigo kuimarisha mashambulizi. Mshambulizi Bertha Omitta na Claudia Kadenge waliingia kuchukua nafasi ya Tumaini Waliaula na Maureen Ater mtawalia.

Mabadaliko hayo ya kocha Boniface Nyamuhnyamu hayakuzaa matunda kwani kunako dakika ya 58, Ulinzi walipata bao la pili kupitia winga Mercy Airo.

Ulinzi walienda nyumbani na Kombe na medali kwa hisani ya Shirikisho la Soka nchini (FKF).

Waziri wa Michezo Ababu Namwamba ambaye alikuwepo uwanjani kutazama mechi hiyo, ametuza kila timu Sh50,000.

Katika mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Shirikisho la Soka nchini (FKF-WPL) msimu wa 2023/24 wikendi ijayo, timu hizo mbili zitakutana ugani Mumias Sports Complex.

Akizungumza baada ya mechi hiyo, kocha wa Ulinzi Joseph Wambua alisema ushindi huo unawapa motisha warembo hao wanapojiandaa kwa msimu mpya.

  • Tags

You can share this post!

Sammy G avuna matunda ya ‘challenge’ Guardian...

Kenya Power yawarai wawekezaji wa kibinafsi kuisaidia...

T L