• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Utamkumbuka Samidoh na nini akistaafu?

Utamkumbuka Samidoh na nini akistaafu?

NA MWANGI MUIRURI

WAPENZI wa sanaa na burudani Mlima Kenya na kote nchini bila shaka wanafurahia muziki wa Samuel Muchoki almaarufu Samidoh ambaye kando na muziki, ni afisa wa polisi.

“Utamkumbuka kwa sifa ya muziki, Mkenya, sarakasi zake tele za kimapenzi au taaluma yake ya kuwa afisa wa polisi?” auliza mwenyekiti wa Shirika la utafiti la Ustawishaji Mila na desturi za Mugikuyu Mzee Kamande Gitu, 75.

Mwaka wa 2050 Bw Samidoh, Mungu akimjalia afya na uhai, atakuwa na umri wa miaka 61 ambapo tayari atakuwa amestaafu kutoka huduma ya polisi nchini.

Samidoh alikuwa amepiga hatua kubwa katika taaluma ya muziki ambapo hata wenyeji Mlima Kenya walikuwa wameanza kumkumbatia kama ‘Mfalme’ wa mtindo wa ‘Mugithi’.

“Kufikia mwaka wa 2018, Samidoh alikuwa akionekana kuwa asiye na ushindani katika kutwaa taji la aliyefanikiwa zaidi ya wote kwa nyakati zote (G.O.A.T) katika kupiga muziki wa Mugithi,” asema Mzee Joseph Kaguthi ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa kwa miaka mingi.

Bw Kaguthi alisema kwamba kuanzia mwaka wa 2021 Bw Samidoh alianza kujulikana kwa ueledi wa kimapenzi na uigizaji mwingi wa baadhi ya wapenzi wake.

Bw Kaguthi anasema kuwa kati ya sifa zote ambazo Samidoh anahusishwa nazo, “hakuna iliyo haramu na zote ni za kujivunia”.

Mnamo Januari 5, 2023, Samidoh aliandika kwa ukurasa wake wa Facebook kwamba “huu mwaka utakuwa wa kutengeneza pesa, mwili na siku za baadaye. Jina  walishakuharibia kitambo”.

Katika mitandao ya kijamii, Samidoh huzua mijadala mikali, nyingi ikiwa kuhusu masuala ya mapenzi huku bidii aliyokuwa nayo ya kuachilia ngoma kalikali na ambazo hukumbatiwa Mlima Kenya kama Wimbo wa Taifa imemtoka.

Sarakasi nyingi zake za kimapenzi huhusu bibi yake wa kwanza Bi Eddie Nderitu dhidi ya Seneta maalum Bi Karen Nyamú huku ucheshi mitandaoni ukichipuza huyu na yule bila kutoa ushahidi wa kina, yeye akikosa kuwakubali au kuwakana.

Mfadhili wa Mashabiki wa Kituo cha redio cha Inooro Bw Muriithi Kang’ara aliambia Taifa Leo kwamba “huwezi ukamlaumu Bw Samidoh kwa kuwa sanasana ngoma zake huwa za kupigia debe mapenzi kati ya wanaume na wanawake na huo ni wito uko katika nafsi yake”.

Alisema kwamba “kilicho katika nafsi ni lazima kikae kikikuramba polepole na ndio sababu unapata mapenzi yakimwandama Samidoh katika kila kona ya uhai wake”.

Masaibu ya Samidoh katika ulingo wa mapenzi yamefanya Naibu Rais Rigathi Gachagua kumshauri kwa ucheshi kwamba “kwanza nenda kwa wazee wakushauri jinsi wanaume wanavyokaa na wanawake wao pasipo sarakasi.”

“Unatuaibisha hadi ng’ambo na huenda kama serikali tukupige marufuku ya kusafiri nchi za nje hadi utupe ushahidi kwamba utadhibiti watu wako,” aliwahi kusema Bw Gachagua.

Lakini Bw Kaguthi anamtetea Bw Samidoh kwa msingi kwamba “yeye na mimi ni wazawa wa Kaunti ya Nyandarua na hakuna cha aibu Samidoh hufanya ikizingatiwa kwamba yeye ni msanii katika sekta ya burudani na ambapo lazima apendwe na mashabiki sambamba na wanawake”.

Anasema kinachohitajika kutoka kwa Samidoh ni busara ya kubaini mbivu na mbichi, kutofautisha kati ya kupendwa na kutumiwa visivyo na wanaomstawisha dhidi ya wanaomwangamiza.

“Samidoh atakumbukwa kwa hayo yote mnayodadisi na pia mengine mengi ambayo hamna uwezo wa kutabiri,” akasema Bw Kaguthi.

  • Tags

You can share this post!

Seneti yashauri magavana jinsi huduma za maji zinavyoweza...

Soka: Green Commandos waapa kurejesha heshima yao

T L