• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 8:50 AM
Bei ya unga wa mahindi Mlima Kenya yapungua hadi Sh15 kipimo cha kilo mbili

Bei ya unga wa mahindi Mlima Kenya yapungua hadi Sh15 kipimo cha kilo mbili

NA MWANGI MUIRURI 

FAMILIA nyingi katika Kaunti ya Murang’a kwa sasa zinachukulia hadithi za bei ghali ya unga kama hekaya za abunuwasi kwa kuwa kwao, unga kilo mbili ni Sh15 pekee.

Kuanguka kwa bei hiyo kutoka Sh250 hivi majuzi, ni kufuatia mavuno tele ya mahindi ambapo kwa sasa mahindi ya kusagwa unga wa kilo mbili ni Sh15.

“Bei hiyo ni ya unga ulio bora zaidi ambao haujatolewa maganda yanayopendekezwa na wataalamu wa lishe kuwa bora kwa afya kinyume na ule wa madukani,” anasema Bi Eunice Njeri kutoka Kijiji cha Kabuta.

Bi Eunice Njeri akiwa na mwaandishi wa habari Bw Kahara Kairia akisema jinsi bei ya unga imeshuka kupitia msimu mzuri wa mahindi. PICHA|MWANGI MUIRURI

Bw John Gathee ambaye ni baba wa watoto wanne anasema kwamba presha ya maisha imemwondokea kwa sasa.

“Awamu ile mbaya zaidi ya kuhitajika Sh300 kwa siku ili watoto wangu wapate lishe imenikoma. Nilikuwa nikinunua unga kwa Sh250 halafu sukuma, mafuta, nyanya na kitunguu vyote vinachota Sh50,” akasema.

Bw Gathee alisema kwamba kwa sasa anahitaji Sh100 pekee ili familia yake ipate mlo wa ugali na nyama.

“Nyama ya Sh50 ikichemshwa na maji vikombe vinne, kisha uongeze sukuma ya Sh20 na nyanya ya Sh5 na kitunguu cha Sh10 kwangu watu wanakula kama Ikulu,” akasema, akiongeza kwamba nyama haihitaji mafuta ya dukani kwa kuwa nyama yenyewe ndiyo mafuta.

Bw John Gathee asimulua Mwaandishi wa habari, Kahara Kairia jinsi unga wa ugali kipimo cha kilo mbili umeshuka hadi Sh15. PICHA|MWANGI MUIRURI

Wakati mambo hayako shwari na nyama ikose, Sh15 za unga hazitakosa na pia Sh20 za mboga pamoja na zingine Sh30 za nyanya, kitunguu na mafuta.

Anasema kwamba mambo yakizidisha makali na atembee kwa wauzaji supu na mutura, anaweza kununua supu vikombe vinne kwa Sh20 na ugali kwake iteremke kana kwamba yeye ndiye alikuwa amechinja.

Bi Jane Kabura kutoka kijiji cha Kamaguta aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba maisha kwake yameimarika kwa kuwa alivuna takriban kilo 1, 200 za mahindi.

“Kwa kuwa ni mimi peke yangu kwa boma langu, nimepata hata fursa ya kusaidia wanyonge kujipa lishe ya ugali kwa bei nafuu,” akasema.

Bi Jane Kabura asema ni Mungu tu bei ya unga imeshuka kupitia mavuno tele ya mahindi. PICHA|MWANGI MUIRURI

Bi Kabura alisema kwamba akimpa mnyonge wa Mungu muumba kilo mbili za mahindi, kisha naye akagharamie kusaga “maisha yanasonga mbele”.

Alisema kwamba miaka miwili iliyopita, maisha yalikuwa ya kusikitisha huku jamii ikikosa hata uwezo wa kusaidiana kupunguza makali ya njaa.

Alielezea, Mungu hawezi akatubebesha mzigo mkubwa unaoweza kutuua hasa ule wa njaa.

Alisema kwamba maombi yake kwa sasa ni wakulima wa eneo hilo wasiingie katika mtego wa kuuza kiholela mahindi waliyovuna.

“Naomba tu tusiwe wa kusahau kama ngiri tulikotolewa na Mungu. Tuhifadhi haya mahindi kwa kila aina ya mbinu, ili unga kwetu uzidi kuwa Sh15 kwa kilo mbili na ikiwa serikali itapunguza bei ya mafuta, bei hiyo iteremke hadi Sh10,” akasema.

Wizi wa mahindi

Bw Patrick Mwaura 50, anasema kwamba kuna baadhi ya walevi wa eneo hilo ambao wanauza mahindi ili wapate pesa za kuburudika.

Bw Patrick Mburu 50, adai kuna walevi wanauza mahindi ili wapate pesa za kununua sigara na kubugia pombe. PICHA|MWANGI MUIRURI

“Ni hali ya majonzi kuona baadhi ya wanaume walevi wakiiba mahindi kutoka kwa maghala yao na kujitokeza nayo mtaani wakiyachuuza kwa bei ya kutupa ili wapate pesa za kuvuta sigara na kubugia pombe. Vilevile, kuna wanawake wanaouza mahindi ili wapate pesa za kununua mkate. Acheni tutumie akili tusimkasirishe Mungu,” akasema.

Akifurahia kushuka kwa bei ya unga kutoka Sh270 pakiti ya kilo mbili hadi Sh15 ule wa kusaga mashinani, Bw Mburu anahimiza kila Mkenya hasa walio maeneo yanayozalisha mahindi wazidi kumtumainia Mungu na wajifunze kuyahifadhi kwa sababu ya siku za usoni.

Isitoshe, mkulima huyo anawahimiza kuendelea kukaza kamba kuyakuza kwa wingi.

 

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Harusi yetu tuliita watu 50 pekee, si uchoyo, ni vile...

Vijana waonywa kuhusu ‘beach parties’ Malindi Ukimwi...

T L