• Nairobi
  • Last Updated April 15th, 2024 2:58 PM
Vijana waonywa kuhusu ‘beach parties’ Malindi Ukimwi ukienea

Vijana waonywa kuhusu ‘beach parties’ Malindi Ukimwi ukienea

NA MAUREEN ONGALA

SHIRIKA la vijana la Dream Youth Achievers Organisation (DAYO) limeshirikiana na serikali ya Kaunti ya Kilifi kutoa hamasisho kuhusu Ukimwi, harakati hizi zikipelekwa shuleni na maeneo mengine ya umma katika eneobunge la Malindi.

Mradi huo ambao pia unafanywa kwa ushirikiano wa Aids Healthcare Foundation (AHF) unaujulikana kama Youth for HIV Prevention unatia zingatio kwa maswala mawili muhimu, kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi haswa miongoni mwa vijana na namna ya kupunguza makali kwa wanaoishi na HIV.

Mkurugenzi Mkuu wa DAYO Bw Seif Jira alisema kuwa waliamua kufanya mradi huo katika eneobunge la Malindi kufuatia ripoti ya utafiti uliofanywa na kuonyesha kuwa maeneo ya ufuo katika ukanda wa Pwani yanaongoza katika maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

“Sababu kubwa ya idadi kubwa ya maambukizi katika ufuo wa Bahari imetokana na ukweli kwamba maeneo haya yako na mambo mengi mabaya yanoendelea, ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya na pia watu wengi kujistarehesha na watalii bila kujali ili kupata pesa,” akasema.

Alisema kuwa wanafunzi katika shule za upili watahusishwa moja kwa moja katika harakati za kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

“Tayari tumetambua shule kumi kutoka Shakahola katika eneobunge la Magarini hadi Gede katika eneobunge la Malindi na tumewachagua vijana ambao ni wakazi wa maeneo hayo ili waweze kuenda huko na kuwachorea wanafunzi hao taswira kamili. Pia tuna walimu kumi ambao tumewapa mafunzo kuhusu Ukimwi ili waweze kutembea nafi katika safari hii,” akasema.

DAYO inalenga wanafunzi 30 ambao ni viongozi katika kila shule na ambao watapeana mafunzo kwa wanafunzi wengine katika madarasa yao tofauti.

Wanafunzi wa Shule ya Upili ya Ngala Memorial katika eneobunge la Malindi wakipata hamasisho kama njia mojawapo ya kukabiliana na kuenea kwa Ukimwi. Hamasisho lilifanya kupitia mradi wa Youth for HIV Prevention (Y4P) mnamo Ijumaa, Septemba 1, 2023. PICHA | MAUREEN ONGALA

Alisema kuwa tayari wameanza vikao vyao na wanafunzi katika shule hizo kuwapa mafunzo.

“Jambo kubwa ni kuwa tunaangalia ni jinsi gani tutakavyoendeleza mradi huu kikamilifu ili kutimiza malengo yetu katika kuwafikia vijana wengi na ujumbe na pia kujulisha jamii kuwa ugonjwa wa Ukimwi bado ni donda sugu katika jamii,” akasema.

Kulingana na Bw Jira, wengi katika jamii wameanza kusahau kuwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi yanasambaa na kusema kuwa vijana katika ya miaka 25 hadi 30 ndio ambao wanaendelea kuathirika pakubwa.

“Hili ni kundi ambalo ni rahisi sana kupata virusi vya ukimwi kwa sababu ni watu ambao wako wako kwa ndoa na wanajisahau sana kuwa huenda mwenzake ana mpango wa kando na ni rahisi kuleta virusi nyumbani,” akisema.

Alisema kuwa wanaweka kipaumbele kwa upimaji wa Virusi Vya Ukimwi (VVU) ili kuafikia ajenda yao ya matibabu.

Aidha wanalenga kuwasaidia waathiriwa na fedha za kununua chakula ili kuboresha lishe huku wakiwahimiza kumeza dawa ili kupunguza makali ya virusi hivyo.

Familia 10 zitafaidika na Sh5000 kila mwezi za kununua chakula.

“Tuna imani kuwa mradi huu utanufaisha watu wengi na kupunguza maaumbukizi ya VVU katika eneobunge la Malindi,” akasema.

Kulingana na twakimu za kila baada ya miezi mitatu kutoka katika hospitali ya Malindi, kati ya Januari hadi Machi inaonyesha kuwa kuna haja ya juhudi kabambe kufanywa ili kuhakisha vijana wanatumia dawa za kupunguza makali, ARVs, ipasavyo.

Ripoti ilionyesha kuwa hospitali hiyo ilirekodi asilimia 25 pekee ya wanaopokea ARVs miongoni mwa vijana wenye umri wa miaka 15 na 24.

Idadi hii ni ya chini kwa hospitali hiyo inayolenga kuwapa asilimia 95 ya vijana wanaoishi na virusi vya ugonjwa huo ARVs.

Kati ya watu 236,549 wanaoishi katika eneobunge la Malindi, takriban 7,341 wameathirika na virusi vya Ukimwi.

Idara ya afya ililenga kuwa wagonjwa 6,974 wangeanza matibabu yao.

Wagonjwa 6,225 walistahili kuwa wanameza ARVs na 6,294 kurekodi kupungua kwa makali ya virusi vya Ukimwi.

Hata hivyo, kati ya wagonjwa 6,974 waliolengwa, hospitali hiyo iliwafikia wagonjwa 5,841 (asilimia 84).

Wagonjwa 5,481 kati ya 6,625 (asilimia 88) walianza kumeza ARVs na 6294 (asilimia 70) walishuhudia kupungua kwa makali ya Ukimwi.

Mbali na hayo, wagonjwa 1,134 kati ya 6,984 wanaostahili kuanza matibabu haijulikani waliko.

Pia wagonjwa 784 ya wanaostahili kumeza ARVs hawajulikani walipo na wagonjwa 1,892 ambao wanastahili kuwa wamepunguza makali ya virusi pia hawaonekani.

Bi Prudence Kombe, muuguzi katika hospitali ya Malindi, alisema kuwa eneobunge hilo bado linang’ang’ana kuhakisha vijana wengi waluoathiriwa na virusi vya ukimwi wanajitokeza kumeza dawa ili kupunguza makali ya virusi.

“Kulingana na twakimu zetu, bado hatujafika pale tunapostahili kuwa katika kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi miongoni mwa vijana. Tunalenga kufikia asilimia 95 lakini kwa sasa tuko katika asilimia 25,” akasema.

Kulingana na Bi Kombe, ambaye pia anasimamia kitengo cha maswala ya dhuluma za kijinsia katika hospitali hiyo, alisema kuwa kutofikia lengo lao la asilimia 95 kumesababishwa na changamoto nyingi ambazo zinawakumba vijana.

“Inaaminika kwamba eneo ambalo wakazi wamepokea matibabu ya virusi vya Ukimwi kwa muda mrefu, kunakuwa na hali ya virusi kutosikia dawa lakini tunakisia tu na itakuwa vizuri iwapo kutafanyika utafiti katika jamii kubainisha hilo,” akasema.

Aliongeza kusema kuwa changamoto nyingine ni kuwa huenda vijana wengi hawamezi dawa zao kama inavyohitajika kulingana na maagizo ya daktari.

“Vijana wengi hawamezi dawa kwa mfulululzo kwa sababu pengine kijana hataki tu kufuatia hali anayopitia ama starehe zake kama kunywa pombe zinavuruga mpango mzima,” akasema.

Bi Kombe aliendelea kusema kuwa imani potovu katika jamii imechangia pia kwani wagonjwa wamekuwa wakishawishiwa kuenda kwa wahubiri kutafuta uponyaji ama hata kutumia mitishamba.

Pia, vijana wengi wanasusia kuenda katika vikao vya kuzungumziwa na wataalam kuhusu namna ya kujikinga.

Hata hivyo, alisema kuwa vijana wengine wanaishi mbali na vituo vya afya na baadhi hukosa nauli kuendea ARVs.

“Japo mashinani tuko na vituo vya kupata ARVs , bado kuna vijana wengine ambao wanatoka mbali zaidi na hawachukui dawa kwa wakati unaohitajika na iwapo atakosa kama wiki moja ama mbili itaathiri pakubwa kinga mwilini,” akasema.

Alimalizia kusema kuwa unyanyapaa pia ni changamoto kubwa miongoni mwa vijana na wengi hawajakuwa tayari kusema wazi hali yao na hawataki kuchukua ARVs katika vituo vya afya karibu nao na husafiri mbali kwa sababu ya kuogopa kujulikana. Hili linafanya hawamezi dawa hizo kwa wakati unaofaa.

Bi Kombe alisema kuwa ushirikiano na mashirika ya kijamii na yale yasio ya kiserikali ni hatua moja wa kusaidia kutatua changamoto hizo miongoni mwa vijana na kuwasaidia kupata ARVs kwa wakati unaofaa.

Shujaa wa vijana kwenye maswala ya Ukimwi katika Kaunti ya Kilifi Bi Rehema Nyamvula, alisema kuwa inasikitisha kuona kuwa idadi kubwa ya vijana hawajajitokeza kupimwa na kumeza ARVs.

Alisema changamoto hiyo inatokana na ukosefu wa hamasa ya kutosha, ukosefu wa njia bora ya mawasiliano kutoka kwa idara ya afya ambayo imechangia vijana wengi kutoelewa.

Alitoa wito kwa serikali ya kaunti kuweka vituo vingi mashinani kuwahudumia vijana kwa heshima ili kuwavutia kwa wingi.

Aliwahimiza vijana kujitokeza kwa wingi na kuwahimiza wenzao kupimwa na pia kumeza ARVs.

DAYO wanafanya kazi katika kaunti tano nchini ikiwemo Kilifi, Mombasa, Nairobi, Kisumu, na Kwale.

  • Tags

You can share this post!

Bei ya unga wa mahindi Mlima Kenya yapungua hadi Sh15...

Sakaja ataka deni kubwa la NMS lichunguzwe

T L