• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Biashara za uchuuzi wa dawa za mende na panya mitaani kufungwa  

Biashara za uchuuzi wa dawa za mende na panya mitaani kufungwa  

NA SAMMY WAWERU 

BODI ya Kudhibiti Kemikali Nchini ndiyo PCPB imetangaza kwamba biashara za wachuuzi wa dawa za mende na panya mitaani zitafungwa. 

Hatua hiyo, kulingana na Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi, Fredrick Muchiri, hatua hiyo inatokana na kukithiri kwa visa vya dawa hatari na zenye zinazouzwa kiholela.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo Dijitali, Bw Muchiri alikiri kuwepo nchini kwa kemikali ambazo hazijaidhinishwa.

Baadhi, zinaingia Kenya kupitia mipaka ya mataifa jirani.

“Kwa sasa, tunashughulikia mikakati kukomesha uuzaji na uchuuzaji wa dawa za mende na panya mitaani,” akasema Afisa huyo.

Huku wachuuzi wakikosa kulengwa moja kwa moja na mpango huo, Bw Muchiri alisema PCPB inalenga kiini cha dawa hizo – wanaowauzia.

“Tunalenga chanzo chake, dawa zinakotoka. Tukiangazia hilo, dawa hizo hazitawahi kuonekana mitaani tena,” alielezea.

“Mchuuzi anaweza akakuuzia chochote, ila sasa umewadia wakati kukomesha uuzaji wa kemikali kiholela. Lazima kuwe na mpangilio.”

Aidha, kufanikisha oparesheni hiyo, Muchiri alisema PCPB itashirikiana na Idara ya Ujasusi (NIS) na ile ya Upelelezi wa Uhalifu na Jinai (DCI) kukabiliana na mtandao wa wafanyabiashara wahuni wanaouza kemikali kinyume na sheria.

Tangazo hilo limejiri siku chache baada ya Shirika moja lisilo la Kiserikali Nchini kufichua kuhusu kuwepo kwa kemikali hatari hasa za kilimo.

Dawa hizo za shambani kukabiliana na wadudu na magonjwa ya mimea, zinatumika nchini licha ya kupigwa marufuku.

Katika kikao cha awali na waandishi wa habari, kilichoandaliwa na kampuni ya aak-Grow ambayo imeshirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kenyatta (KNH) kuzindua upya kituo cha kupokea visa vya watu kunywa sumu au kuathirika, ilibainika kwamba wakulima wanatumia kemikali zilizopigwa marufuku kukuza chakula.

Kirinyaga ilitajwa kama mojawapo ya kaunti zilizoathirika pakubwa, wakulima wakisusia kufichua dawa hizo.

Mitaa mingi nchini, hasa maeneo ya mijini wachuuzi wa dawa za mende na panya wanaendeleza biashara bila kudhibitiwa.

Hatua hiyo inaibua hatari kuhusu usalama wa watu kiafya haswa wanaozinunua, zingine zikitajwa kuwa bandia na hatari.

  • Tags

You can share this post!

Ezekiel Odero aonya watu dhidi ya kusherehekea siku maalum...

Eneo Nakuru ambapo baa ni nyingi kuliko makanisa

T L