• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
BONGO LA BIASHARA: Jinsi video, picha zilivyomsukuma kuingilia uchoraji

BONGO LA BIASHARA: Jinsi video, picha zilivyomsukuma kuingilia uchoraji

Na SAMMY WAWERU

MAPEMA Januari 2021, video ya Jane Nyambura aliyelalamikia kuhujumiwa na kampuni moja ya Kichina iliyopewa zabuni kuchimba bwawa la Karimenu, Gatundu Kaskazini, Kaunti ya Kiambu, ilisambaa mitandaoni.

Ilizua ucheshi kutokana na alivyoelezea masaibu yake baada ya kuondolewa kwenye ardhi yake ili kuruhusu ujenzi wa bwawa kuendelea, ila hakufidiwa.

Japo masimulizi yake kwenye video hiyo yanazua utani, ana ujumbe: “Kutafuta haki”.

Joseph Njoroge Maina ni mchoraji hodari na kupitia kipaji chake, alichora picha ya Nyambura, akinyooshea kidole cha lawama kampuni inayodaiwa kumhujumu nyanya huyo.

Aliipakia kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii chini ya nembo yake, Josey Arts, asijue hatua hiyo ingegeuka kuwa jukwaa la nyanya kupata haki na pia kuvumisha talanta yake ya uchoraji.

Kulingana na Maina, chini ya saa chache, picha ile ilisambaa mitandaoni mithili ya moto unavyochoma nyasi nyikani, akaanza kupokea simu za kongole.

“Sikujua watumizi wa mitandao wataichukulia kwa uzito. Wengi walinipigia simu kunipongeza na pia kutaka kujua iwapo ninaweza kuwachora,” anaelezea msanii huyo.

Msambao wa picha hiyo ukageuka kuwa fursa ya biashara yake ya sanaa kuinuka.

Licha ya kuwa alichora nyanya huyo kwa sababu video ilizua utani, ‘lugha’ ya uchoraji aliyotumia iliashiria nyanya mwenye hasira na kwa hakika angetaka haki kutendeka.

Maina anafichua kwamba alipata fursa ya kumtembelea Nyambura na hadithi yake ni ya kuhuzunisha, mahangaiko aliyopitia baada ya kuondolewa katika shamba lake.

“Nilimtunuku picha yake, hatua ambayo ilimfurahisha akanifungulia moyo kuna nuru gizani, serikali iliahidi kumfidia,” anasema.

Ni picha iliyochangia kupata wateja, akidokeza kwamba kwa sasa kila wiki hakosi kuhudumia wateja watano. Hali kadhalika, imekuwa jukwaa la kuonyesha umahiri wake katika uchoraji.

Isitoshe, Maina anadokeza kusambaa kwa picha hiyo kumevutia idadi kubwa ya wanafunzi wanaotaka kunolewa talanta katika uchoraji.

Akiwa mzaliwa wa kijiji cha Marumi, Kigumo, Kaunti ya Murang’a, Maina anaiambia Akilimali kuwa alitambua ana kipaji cha uchoraji hata kabla ya kujiunga na chekechea. Ari hiyo aliipiga jeki kwa kutazama michoro kwenye magazeti na majarida.

Anasema historia ya ufanisi wake katika sanaa si kamilifu bila kutaja baba yake, Mzee Francis Maina, anayemsifia kwa kuwa nguzo kuu.

“Baba pia alipenda kuchora, alikuwa kielelezo na alinitia motisha,” anasema.

Katika shule ya msingi, Maina alitegemewa pakubwa na wanafunzi wenzake kuwachorea picha walizopewa kama kazi ya ziada. Alikuwa hodari wa kuchora pia ramani. Kilele cha upalizi wa talanta yake kilikuwa katika Shue ya Upili ya Karega, alikosomea.

“Nilikuwa nikiomba walimu magazeti. Walidhani shabaha yangu ilikuwa kunoa ufasaha katika Kiswahili na Kiingereza ila nililenga kurasa za vibonzo, nilizokuwa nikikata na kuchora upya,” anafafanua, akiongeza kuwa magazeti ya Taifa Leo na Daily Nation yalimfaa na kumuinua pakubwa.

Anataja magwiji Gado, John Nyagah, Stano na marehmu E. Gitahi (Juha Kalulu) kuwa chanzo cha ubunifu wake wa kuajabiwa.

Baada ya kufanya Mtihani wa kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) na kufuzu, Maina alitamani kusomea uandishi wa habari. Hata hivyo, alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) kusomea taaluma ya ualimu (Historia na Dini). Mnamo 2010, akiwa Mwaka wa Pili, alifufua na kuendeleza ari yake katika sanaa.

“Nikiwa katika Mwaka wa Tatu, niligeuza talanta yangu kuwa biashara. Nilikuwa nachora na kuuza picha moja kwa Sh5,” anaelezea.

Anasema alianza kwa penseli, kifutio na karatasi, vifaa vilivyomgharimu mtaji wa Sh50 pekee. Alifanya tafiti za kina mitandaoni na kwenye magazeti, baadaye akaimarika na kukumbatia uchoraji kwa kutumia rangi na brashi. Anadokeza, ilimgharimu Sh4,000 kununua vifaa vilivyotakikana, pesa hizo zikiwa sehemu ya mkopo wa HELB.

Hata baada ya kufuzu chuoni mnamo 2013 na kuajiriwa na serikali miaka miwili baadaye, chini ya Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC), Maina aliendeleza uchoraji.

Katika shule alizofunza kama vile South Tetu Girls (Nyeri) na Shule ya Upili ya Ituru, Gatundu Kusini, alizindua makundi ya sanaa kwa nia ya kunoa wanafunzi.

Mnamo 2018, Maina aliamua kujiuzulu TSC, akajiunga na Riara Group of Schools kufunza sanaa. Hatua ya kujiuzulu anasema haikuwa rahisi, kwa kile anataja kama kupokea upinzani mkali.

Baada ya Kenya kuthibitisha kuwa mwenyeji wa janga la Covid-19 Machi 2020, miezi michache iliyofuata Joseph alifanya uamuzi mwingine kujiuzulu Shule za Riara kuzamia uchoraji kikamilifu.

Kijiji cha Matangi-ini, Kimbo-Ruiru, Kaunti ya Kiambu, karakana ya mwanasanaa huyu ni bayana amepiga hatua nyingi mbele kimaendeleo.

Jitihada zake zimemuwezesha kuchora picha za mawaziri, Prof Margaret Kobia (Jinsia) na James Macharia (Uchukuzi), mbunge maalum na Katibu Mkuu wa KNUT, Wilson Sossion, Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Murang’a, Sabina Chege na mwandishi mashuhuri wa vitabu Prof. Ngugi Wa Thiong’o, ambao wamezinunua.

Pia amechora picha ya Rais mpya wa Amerika, Joe Biden na ambayo imemfanya kuangaziwa na zaidi ya vyombo kumi vya habari ughaibuni.

Msanii huyu anasema anaendelea kupokea maombi chungu nzima kutoa mafunzo ya uchoraji, ambapo hutoza ada kuanzia Sh1, 000.

“Changamoto iliyoko ni kwamba karakana yangu ni ndogo mno kwa shughuli hiyo. Ninaomba serikali na wahisani-wadauhusika kujitolea tushirikiane kuimarisha sekta ya sanaa, ni kiwanda chenye uwezo kubuni mamia, maelfu na hata mamilioni ya ajira kwa vijana,” Joseph anahimiza.

Sekta ya uchoraji nchini kwa kiasi fulani imeonekana kupuuzwa, na kulingana na Edward Gikaria ambaye pia ni mchoraji hodari hamasisho kuipiga jeki inahitajika.

“Kuna vipaji wengi sana wenye talanta ya uchoraji, ila hawana uwezo kifedha wala jukwaa kujiendeleza, serikali ifanye hima kuwainua,” Gikaria anashauri.

Mwaka uliopita, Joseph anasema alikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi alionoa makali kuchora.

Huku akiendelea kupokea wateja, Sikukuu ya wapendanao inayoadhimishwa Februari 14 kila mwaka ikibisha hodi, msanii huyu ambaye ni baba wa watoto wawili anasema analenga kupokea zaidi ya wateja 10 kila juma.

You can share this post!

AKILIMALI: Aliacha mahindi ili kula ndizi kwa kijiko

AKILIMALI: Jinsi teknolojia inavyopunguza gharama ya kukuza...