• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Corona ilivyofumbua macho kampuni ya macadamia 

Corona ilivyofumbua macho kampuni ya macadamia 

NA SAMMY WAWERU

JANGA la Covid-19 lilipolipuka mwaka wa 2020, shughuli na biashara nyingi ziliathirika kufuatia sheria na mikakati iliyowekwa kudhibiti maenezi zaidi.

Amri ya ama kuingia au kutoka kaunti zilizotajwa kuwa katika hatari ya maambukizi na huduma za usafirishaji mizigo ng’ambo kwa ndege kusitikishwa kwa muda, sekta ya kilimo ilikadiria hasara kubwa.

Ni gonjwa la kimataifa lililofumbua wengi macho, mtandao wa uzalishaji na usambazaji chakula nchini ukitathmini mifumo ya uongezaji thamani.

Wish Kenya Ltd ni kampuni inayokusanya zao la macadamia kutoka kwa wakulima, na kuyatafutia masoko nje ya nchi na haikusazwa na mjeledi wa virusi vya corona.

Kulingana na Philomena Nduku, afisa msaidizi kitengo cha mauzo na soko, anasema kampuni hiyo yenye kiwanda eneo la Thika, Kaunti ya Kiambu mwaka uliopita ilianza kuongeza thamani njugu za zao hilo.

“Tumekuwa kwenye biashara ya macadamia tangu 2010, na corona ilipoingia tukaathirika. Hivyo basi hatukuwa na budi ila kusaka mbinu mbadala kuendeleza utendakazi, ambapo tulikumbatia ukamuaji mafuta,” Nduku adokeza.

Afisa huyo anasema hali ilikuwa ngumu, kiasi cha mazao kuozea kwenye maghala.

Utengenezaji mafuta, ni mwanya anaotaja kuwa na faida tele ikizingatiwa kuwa mafuta wanayorina yanatumika kwenye mapishi, kuchoma nyama, uokaji keki na kiungio cha saladi.

Purity Makena akielezea kuhusu mafuta ya njugu za macadamia. PICHA | SAMMY WAWERU

Wanapopokea mazao, hukagua kiwango cha unyevuunyevu wa maji kwenye njugu, Nduku akisisitiza sharti yawe huru dhidi ya magonjwa, wadudu na chembechembe hatari za aflatoxin.

Yanapoafikia vigezo vilivyowekwa na kampuni hiyo, hukaushwa kwa nguvu za umeme na kutolewa maganda.

Mashine maalumu aina ya compresser, inatumika kukama mafuta ikiwemo hatua kadha kuyasafisha na kuyachuja.

Akiyasifiia kusheheni virutubisho, Nduku anasema yanawekwa na kupakiwa kwenye chupa za glasi.

“Yanadumu muda wa miaka miwili,” aelezea, akisema uhalisia huo unawezesha mfanyabiashara kutafuta soko bila presha.

Huku wanunuzi wakuu wakiwa maduka ya jumla Kiambu na Nairobi, kipimo cha mililita 100 kinagharimu Sh145, 250 Sh450, 500 Sh800 na 750 Sh1, 200.

Philomena Nduku akihudumia mteja aliyetaka kujua manufaa ya mafuta ya macadamia. PICHA | SAMMY WAWERU

Afisa huyo anaambia Akilimali kwamba, hivi karibuni wanapania kuzindua kipimo cha lita moja.

“Lita 20 tunapima kupitia oda.”

Maganda ya macadamia yanatumika kama kuni.

Isitoshe, masalia ya njugu baada ya kukama mafuta ni malighafi kutengeneza chakula cha mifugo.

  • Tags

You can share this post!

MITAMBO: Mtambo muhimu wa kupulizia mimea dawa mashambani

Wahofia unyakuzi ardhi ujenzi wa bandari ukianza

T L