• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
MITAMBO: Mtambo muhimu wa kupulizia mimea dawa mashambani

MITAMBO: Mtambo muhimu wa kupulizia mimea dawa mashambani

NA RICHARD MAOSI

MIFUMO ya kisasa inayotumika kupulizia mimea dawa huangazia maswala muhimu kama vile hali ya anga, dozi sahihi, aina ya magonjwa pamoja na njia sahihi kupulizia dawa hiyo.

Kutozingatia baadhi ya hatua hitajika, huenda kukazua matatizo zaidi kwa mimea.

Kwa mfano matawi ya mimea yanaweza kubadili rangi, na kupata ukungu wa poda nyeupe, hali ambayo husababisha ukuaji kudumaa.

Hivyo, ni muhimu kukabiliana na tatizo hilo haraka iwezekanavyo kwa kutumia dozi sahihi ya viua kuvu vya kemikali ambavyo wakati wote huwa ndio suluhu ya mwisho kwa mkulima.

Sharon Kiangi ambaye anasimamia shughuli ya upulizaji dawa eneo la Naivasha, anasema ukuaji wa teknolojia ya kilimo, pia umejumuisha masuala ya upuliziaji mimea dawa.

Kulingana na Kiangi hii itawasaidia wakulima kukabiliana na magonjwa kwa wakati unaofaa.

Anaeleza Akilimali kuhusu manufaa ya kutumia mtambo wa boom sprayer ambao mara nyingi hukokotwa kwa trekta kutoka na hali kuwa huwa umewekewa programu ya kilimo.

Boom sprayer humsaidia mkulima kutambua lita za dawa ambazo atahitaji kupulizia mimea yake kila msimu katika kila ekari, hali ambayo humsaidia kuweka hesabu za kubaini ikiwa anatengeneza faida ama hasara, hasa kipindi hiki ambapo pembejeo za kilimo zimepanda.

Mtambo unaoweza kuwasaidia wakujlima wakati wa kupulizia mimea yao dawa. PICHA | RICHARD MAOSI

Anasema ni njia ambayo huchangia upandaji wa mimea kwa kutunza ikolojia kwa kuangamiza wadudu na vimelea sugu vya bakteria.

Upuliziaji sahihi wa dawa pia husaidia mimea kuwa stahimilivu na kuhifadhi udongo ikizingatiwa kuwa kiwango cha dawa kwenye mtambo wa boom sprayer huwa kimeratibiwa, wala mkulima hawezi kupulizia mimea yake dawa nyingi kupita kiasi.

“Boom sprayer hurahisisha kazi na kuokoa muda wa kupulizia dawa shambani kwa njia inayostahili,” anasema.

“Programu kwenye boom sprayer humsaidia mkulima kutambua iwapo mimea yake ina uhaba wa madini fulani kama vile calcium, phosphorus au patassium,” anaeleza.

Kwa sababu hiyo, mkulima anaweza kuwa katika nafasi nzuri ya kukusanya ujumbe, kuhifadhi data na hatimaye kutafuta mapendekezo ya jinsi ya kuboresha kilimo.

Aina hii ya mtambo hutumika kwenye mashamba makubwa miongoni mwa wakulima ambao wanaendesha kilimo biashara cha matunda na mboga.

Ni mtambo ambao hukokotwa na trekta na sehemu kubwa kubeba mabomba ya kuhifadhi dawa kulingana na mahitaji ya mimea.

Kiangi anaongezea kuwa mtambo huu ni wa manufaa kwa misimu yote ya upanzi, hususan kwa maharagwe, sukumawiki na kabeji ambazo huchukuwa muda wa miezi mitatu hivi kukomaa.

You can share this post!

Wanavyogeuza taka kuwafaidi kimaisha

Corona ilivyofumbua macho kampuni ya macadamia 

T L