• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
DKT FLO: Harufu mdomoni licha ya kupiga mswaki

DKT FLO: Harufu mdomoni licha ya kupiga mswaki

Mpendwa Daktari,

Nina tatizo la harufu mbaya mdomoni japo mimi hupiga mswaki mara mbili kwa siku. Tatizo hili limenikosesha raha kiasi cha kwamba nina wasiwasi kila nikiwa mbele ya watu. Nifanyeje kukabiliana na tatizo hili?

Harry, Nairobi

Mpendwa Harry,

Tatizo la harufu mbaya mdomoni au halitosis, laweza sababishwa na bakteria mdomoni. Yaweza kuwa pia kutokana na maradhi ya ufizi au masalio ya chakula mdomoni.

Unapaswa kupiga mswaki na kuondoa masalio cha chakula kwa kutumia uzi maalum wa hariri (floss) kila baada ya kula angaa mara mbili kwa siku, na pia usugue ulimi wakati huu. Pia unaweza tumia dawa maalum ya mdomoni kwa kusukuta kila baada ya kusugua meno.

Pia, unashauriwa kukaguliwa na daktari wa meno ili yasafishwe na uchafu uondolewe kwani uchafu huu huchangia meno kuoza na kuleta harufu mbaya mdomoni.Mdomo pia kukauka huchangia shida hii kwa sababu mate husaidia kusafisha chembe chembe za chakula na bakteria.

Wakati wa usingizi, shughuli za kuzalisha mate hupungua na hivyo kuwezesha bakteria kuongezeka. Hii ndio husababisha harufu mbaya mdomoni wakati asubuhi. Ili kukabiliana na tatizo hili, mbali na kusugua meno asubuhi, unapaswa kula chakula pia wakati huu.

Huenda ukakumbwa na tatizo la harufu mbaya mdomoni hata baada ya kupiga mswaki, endapo hutakula. Njaa ya muda mrefu na kufunga pia vyaweza sababisha tatizo hili.

Chakula unachokula pia huchangia tatizo la harufu mbaya mdomoni. Kwa mfano, baadhi ya vyakula kama vile vitunguu na vitunguu saumu, baadhi ya viungo na samaki. Kwa hivyo punguza vyakula vya aina hii.

Pia, kula vyakula vyenye viwango vya chini vya wanga, kwa mfano wakati wa mfungo, yaweza sababisha mwili kuvunja vunja mafuta mwilini na hivyo kusababisha uzalishaji wa kemikali aina ya ketones, ambazo husababisha harufu inayokaribiana na ile ya matunda unapopumua.

Kunywa maji kwa wingi; angaa lita mbili kwa siku na ule mboga na matunda kwa wingi.Matatizo mengine ya kiafya ambayo yaweza changia tatizo hili ni pamoja na sinusitis, maambukizi ya kila mara ya koo, mabonge ya kooni (tonsil stones), kiungulia na maambukizi ya tumbo, kisukari, matatizo ya ini au figo.

Sababu nyingine ni kuvuta sigara, kunywa pombe kwa wingi na mabadiliko ya kihomoni. Iwapo sababi zozote hizi zinasabbaisha harufu mbaya, kabiliana na kiini chenyewe.

  • Tags

You can share this post!

Uhuru akwepa kumsalimia Dkt Ruto kwa mkono bungeni

Boresha Afya: Kukaza misuli ya mwili

T L