• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Uhuru akwepa kumsalimia Dkt Ruto kwa mkono bungeni

Uhuru akwepa kumsalimia Dkt Ruto kwa mkono bungeni

NA CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kwa mara ya kwanza tangu Desemba 12, 2021 walionekana pamoja hadharani.

Wawili hao walikutana walipofika katika majengo ya bunge, Nairobi kutizama mwili wa rais wa zamani marehemu Mwai Kibaki.

Hata hivyo, hawakusalimiana kwa mikono bali wakainama na kuonyeshana ishara ya mikono.

Rais Kenyatta na Dkt Ruto, ambao zamani walikuwa wandani wa karibu, sasa wamegeuka kuwa maadui wa kisiasa. Hii ni baada ya Rais Kenyatta kutangaza waziwazi kwamba hatamuunga mkono naibu wake kuwa mrithi wake atakapostaafu mnamo Agosti mwaka huu.

Badala yake kiongozi wa taifa ameamua kumuunga mkono kiongozi wa upinzani wa Raila Odinga kuwa mrithi wake, hatua ambayo inaenda kinyume na ahadi aliyotoa mnamo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2013.

Kando na Dkt Ruto, Rais Kenyatta pia alikwepa kuwasilia kwa mikono Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na mwenzake wa Seneti Kenneth Lusaka ambao wamemkaidi na kuamua kuunga mkono Dkt Ruto kwenye kinyang’anyiro cha urais.

Hata hivyo, Rais Kenyatta alimsaliamia kwa mikono kingozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na viongozi wengine wa ngazi za juu serikali waliofika katika majengo ya bunge kutoa heshima zao za mwisho kwa Hayati Kibaki.

Dkt Ruto ametangazwa kuwa mgombea urais chini ya mwavuli wa muungano wa Kenya Kwanza. Muungano huo unashirikisha jumla ya vyama 12.

Vyama vikuu katika muungano huo ni United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Dkt Ruto, Amani National Congress (ANC) cha Musalia Mudavadi na Ford Kenya kinachoongozwa na Moses Wetang’ula.

Mwili wa Hayati Kibaki uliwasili katika majengo ya bunge na ulibebwa kwa gari la jeshi ukisindikizwa na wanajeshi wa vyeo vya juu.

Wananchi watapata fursa ya kutizama mwili huo na kutoa heshima zao za mwisho kwa kipindi cha siku tatu, hadi Jumatano.

Serikali imetangaza Ijumaa kuwa Siku ya Mapumziko kutoa nafasi kwa Wakenya kuhudhuria ibada ya kitaifa ya wafu kwa heshima ya Hayati Kibaki.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Kibaki ndiye ‘Musa’ aliyekomboa...

DKT FLO: Harufu mdomoni licha ya kupiga mswaki

T L