• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
El Nino yaangamiza watu 4 Wajir mafuriko yakilemea kaunti nzima

El Nino yaangamiza watu 4 Wajir mafuriko yakilemea kaunti nzima

NA SAMMY WAWERU

VIONGOZI kutoka Kaskazini mwa Kenya wanaomba msaada wa dharura kuokoa jamii zinazoishi eneo hilo kame (ASAL) kufuatia athari za mvua ya El Nino inayoendelea kushuhudiwa maeneo mbalimbali nchini.

Kulingana na viongozi hao, takriban theluthi mbili (2/3) ya Kaunti ya Wajir imeathirika vibaya kutokana na mvua kubwa inayonyesha.

Barabara zinazoelekea Kaskazini mwa Kenya hazipitiki (zimekatika), Wajir ikitajwa kuharibika pakubwa.

Akizungumza na vyombo vya habari mnamo Jumatatu, Oktoba 20, 2023, katika Uwanja wa Ndege wa Wilson, Jijini Nairobi wakati akiruhusu shehena ya dawa kwenda Wajir, Gavana wa Kaunti hiyo Ahmed Abdullahi alionya kuwa eneo hilo linakabiliwa na changamoto za kibinadamu.

“Hali ni mbaya; sehemu zote ya Wajir, kwa mfano, zimejaa maji,” Bw Abdullahi alilalamika, akifichua kwamba kaunti hiyo imeandikisha visa vinne vya watu waliopoteza maisha kutokana na mvua kubwa.

Gavana wa Wajir Bw Ahmed Abdullahi akizungumza katika Uwanja wa Ndege wa Wilson, Jijini Nairobi mnamo Jumatatu, Novemba 20, 2023. PICHA|SAMMY WAWERU

“Hali tunayoshuhudia si mzaha. Barabara zote zinazoelekea Wajir zimekatika, na watu wetu wanahangaika kutokana na njaa na ukosefu wa mahitaji muhimu ya kimsingi,” alisema bosi huyo wa kaunti.

Kupitia msaada wa Bluebird Aviation, kampuni ya ndege ya kikanda iliyo na makao yake jijini Nairobi, Gavana Abdullahi aliongoza kutuma shehena ya dawa za tani 24 kutokana na hali ya hatari kiafya inayokodolea macho kaunti yake.

Dawa hizo zilinunuliwa na Serikali ya Kaunti ya Wajir kutoka kwa Mamlaka ya Usambazaji Dawa Nchini (KEMSA), na hivyo kulazimu uongozi wa kaunti kujihami kwa mipango ya dharura ili kusaidia kukabiliana na uwezekano wa mlipuko wa magonjwa yanayosababishwa na mafuriko.

Dawa (ndani ya ndege) zilizonunuliwa na Serikali ya Kaunti ya Wajir kusaidia kuimarisha matibabu endapo magonjwa ya maji yatalipuka. PICHA|SAMMY WAWERU

Bw Abdullahi alidokeza kwamba hospitali na vituo vya afya Wajir vinaelekea kuishiwa na vifaa vya matibabu.

“Matrela yanayobeba dawa tulizonunua kama kaunti kutoka KEMSA yamekwama kwa muda wa wiki mbili zilizopita barabarani. Hospitali zetu zinaishiwa na dawa, na tumelazimika kutumia usafiri wa anga kuangazia dharura iliyopo,” Gavana huyo alielezea.

Dawa zilizokwama njiani kwa sababu ya miundomsingi duni na mbovu ya barabara ni tani 57, na tani 67 zaidi ziko kwenye maghala ya KEMSA.

“Jimbo la Kaskazini mwa Kenya linalemewa na mafuriko kutoka Ethiopia na eneo la Kati, hivyo basi hali ni mbaya sana. Miji imesheheni maji, hivyo kufanya hali iwe mbaya zaidi,” Bw Abdullahi alifahamisha.

Barabara zilizoathiriwa kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha ni Nairobi-Isiolo, Nairobi-Garissa, na Garissa-Wajir-Mandera.

Wakati wa kutuma sheheni ya dawa katika kaunti yake kwa kutumia ndege, Gavana huyo wa Wajir alikuwa ameandamana na wabunge kutoka Kaskazini mwa Kenya, akiwemo Bw Abass Sheikh, Seneta wa Kaunti, Bi Fatuma Jehow, Mbunge Mwakilishi wa Wanawake, Mbunge wa Eldas Aden Keynan, Hussein Barre (Tarbaj), Farah Yussuf Mohamed wa Wajir Magharibi, miongoni mwa wengine.

Wakinyooshea kidole cha lawama Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu Nchini (KeNHA) kwa kile walichokitaja kama “kutelekeza barabara za eneo hilo”, wabunge hao walilaumu serikali kuu kwa kutosaidia Kaskazini mwa Kenya kupunguza athari hasi za El Nino.

Ndege iliyosafirisha dawa kuelekea Wajir kutokana na hali mbovu ya barabara kwa sababu ya athari za El Nino. PICHA|SAMMY WAWERU

“Barabara kuelekea eneo hilo imekatikia Modogashe, na kwa hivyo jaribio lolote kutuma kitu kwa njia ya barabara litakuwa halina manufaa sasa. Tunaiomba serikali kuu itoe msaada na kusaidia watu wa eneo letu,” Dkt Keynan aliiomba.

Kabla ya kubisha hodi kwa El Nino, Baraza la Magavana (CoG) kupitia Mwenyekiti wake, Anne Waiguru (Gavana wa Kirinyaga), lilikuwa limeomba Serikali ya Kitaifa kutenga kima cha Sh15 bilioni kwa ajili ya maandalizi kupunguza na kukabiliana na athari za El Nino.

Hata hivyo, kulingana na Gavana wa Wajir Bw Abdullahi, fedha hizo hazijatolewa.

Mkuu huyo wa kaunti aliambia wanahabari kwamba Wajir kwa sasa inashirikiana na Kikosi cha Majeshi ya Ulinzi wa Kenya (KDF) kusambaza kwa kutumia ndege chakula na bidhaa zingine muhimu za kimsingi, kwa ushirikiano na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya, ambalo limetoa misaada ya chakula kwa wakazi walioathirika.

Mnamo Jumanne, Novemba 21, 2o23, Serikali ya Kaunti ya Wajir itaanza kutuma misaada ya chakula kutoka Nairobi.

Viongozi wa Kaskazini mwa Kenya wameonya kwamba ikiwa hatua za dharura hazitachukuliwa, magonjwa yanayosambazwa na maji, ukosefu wa chakula, na mahitaji muhimu ya binadamu yataanza kuathiri wakazi hivi karibuni.

Kulingana na Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa ya Kenya, huenda El Nino ikaendelea hadi Januari mwaka ujao, 2024.

Awali, Rais William Ruto alikuwa amepuuzilia mbali uwezekano wa mvua kubwa, akikosoa Idara ya Hali ya Hewa kwa alichodai ni “kutoa onyo lisilo la kweli”.

  • Tags

You can share this post!

Bei za mafuta, umeme kupanda tena mswada mpya ukipitishwa

Kanisa lafungisha ndoa za pamoja kusaidia kupunguza tabia...

T L