• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 9:11 AM
FATAKI: Vipodozi haviongezi wala kupunguza ubongo wa mtu kichwani

FATAKI: Vipodozi haviongezi wala kupunguza ubongo wa mtu kichwani

Na PAULINE ONGAJI

HIVI majuzi nilijiunga na kikundi fulani kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.

Ili kujitambulisha, kila mwanachama aliyekuwa akijiunga, alilazimika kuchapisha picha yake kwenye ukurasa wa kikundi hicho mtandaoni.

Ni wito ambao ulisababisha mabibi kwa madume kujikakamua na kutuma picha zao wakipendeza ajabu. Lakini kaka mmoja alionekana kukerwa hasa na mabinti.

“Hata mnapoendelea kuchapisha picha kuonyesha maumbo yenu ya kupendeza na sura zenu nzuri, hakikisheni kwamba sifa hizi mnaziambatanisha na tabia njema, maadili na werevu,” aliwaambia mabinti.

Ni kauli niliyokubaliana nayo kabisa kwani ni muhimu kujinoa kimaadili na kiakili, sambamba na urembo. Alinikera tu kwa kuegemea upande mmoja, mabinti pekee.

Pia akina kaka walikuwa wakichapisha picha zao za kupendeza na hakuna hata mmoja niliyoona ikiwa imeambatanishwa na tabia njema, maadili au werevu. Pili, kwa nini watu wanapenda kulinganisha maadili, vile vile werevu na urembo? Nani alisema mwanamke mrembo hawezi kuwa mwerevu na mwenye tabia njema?

Nimekutana na mabinti wengi visura wenye maadili na werevu ajabu, na pia nimekutana na vipusa wengi ambao kwa viwango vya kawaida hawawezi orodheshwa miongoni mwa mabinti warembo, lakini pia wana tabia njema na maadili ya viwango vya juu.

Hii yanikumbusha kuhusu chapisho la kaka mmoja mtandaoni aliyeonekana kuendeleza dhana kwamba mabinti wanaojipodoa hawana akili.

Vipodozi haviongezi wala kupunguza ubongo wa mtu kichwani. Ikiwa wewe ni bwege, ujipodoe au la, hakuna litakalobadilisha ukweli huo. Ikiwa wewe ni mwerevu, ujipodoe au usalie vivyo hivyo, hakuna linalobadili ukweli huo.

Kwa hivyo haupaswi kumlaumu binti aliyejikakamua kujinoa kiakili na pia kimwonekano, kisha umtunuku ambaye hajatia bidii kuuchangamsha ubongo wake, eti tu kwa sababu hajipodoi.

Mbali na hayo, watu wanapaswa kukumbuka sio kila mtu anayevutiwa na mwenziwe tu kwa sababu ya werevu wake. Kuna madume wanaokanganywa na kiuno na kifua hata ikiwa ubongo ni mdogo kuliko wa kuku. Sawa na jinsi kuna mabinti wanaopagawishwa na kifua kipana na misuli iliyochomoza kwenye ngozi, hata kama kichwa kimejaa uji.

Na kuna baadhi ya madume wanaopaswa kukoma kuwekea wanawake vikwazo vya mapenzi eti sababu wanajipodoa, wana nywele na kucha za kubandika.Wanapaswa kujifunza kutoka kwa baadhi ya mabinti. Kuna mengi ya wanaume yasiyoridhisha lakini wanawake wao wanayavumilia bila kulalamika.

  • Tags

You can share this post!

MWANAMUME KAMILI: Karibu kijiweni tuwakemee wanaotafuta...

UMBEA: Unaweza chagua kutopendwa ila kumbuka huishi...