• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Gachagua awataka viongozi wa kidini kukoma kushinikiza Rais kusaka maridhiano na Raila Odinga

Gachagua awataka viongozi wa kidini kukoma kushinikiza Rais kusaka maridhiano na Raila Odinga

NA SAMMY WAWERU

NAIBU wa Rais Rigathi Gachagua amewataka viongozi wa kidini nchini na jamii ya kimataifa kukoma kushinikiza Rais William Ruto kusaka maridhiano kati yake na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga. 

Akimtaja Bw Odinga, ambaye ni kinara wa muungano wa Azimio la Umoja, kama ‘mhalifu’ alisema serikali ya Kenya Kwanza haina nafasi ya wahalifu kushirikishwa kwenye uongozi. 

“Kwa muda mrefu, huyo Mzee wa maandamano (akimaanisha Raila Odinga) amekuwa akitumia fujo kutafuta uongozi. Huo ni uhalifu, ambapo kumeshuhudiwa vifo, uharibifu wa mali na biashara. 

“Ombi langu ni viongozi wa kidini na jamii ya kimataifa muache kushinikiza Rais atafute salamu za maridhiano na mhalifu. Hilo hatutakubali,” Bw Gachagua alisema. 

Akikashifu maandamano yanayoandaliwa na Azimio maeneo tofauti nchini, naibu rais alisema ghasia na fujo zinazoshuhudiwa zinakandamiza na kulemaza uchumi. 

Upinzani umeratibu maandamano ya siku tatu kila wiki, waandamanaji wakikabiliana vikali na maafisa wa polisi. 

“Raila Odinga ajue njia ya kipekee kupata uongozi, ni kupitia debe – kushiriki uchaguzi, na kuchaguliwa na Wakenya,” alisema. 

Serikali imeharamisha maandamano hayo, visa kadha vya maafa – watu waliopigwa risasi na askari na kufariki vikiripotiwa na wengine kuuguza majeraha mabaya. 

Azimio inashinikiza serikali kushusha gharama ya maisha, kupinga Sheria ya Fedha 2023 inayopendekeza nyongeza ya ushuru, miongoni mwa matakwa mengine.

  • Tags

You can share this post!

Waandamanaji 82 Nakuru waendelea kuzuiliwa na polisi

Machimbo hatari Soy yaliyoangamiza watoto wawili

T L