• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 5:15 PM
Machimbo hatari Soy yaliyoangamiza watoto wawili

Machimbo hatari Soy yaliyoangamiza watoto wawili

NA TITUS OMINDE

WAKAZI wa kijiji cha Soy, Kaunti Ndogo ya Soy wanaitaka Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) kushurutisha Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi kufunika machimbo yote yaliyoachwa wazi, kutokana na hatari yanayoibua.

Wakaazi hao waliojawa na hasira wanadai kuwa machimbo hayo yamekuwa mahandaki ya kuua watoto wao mbali na kuwa ngome ya kusambaza Malaria kwa kukuza mbu wanaoeneza maradhi hayo hatari msimu wa mvua.

“Chini ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita tumepoteza watoto wawili baada ya kuzama kwenye mitaro iliyoachwa na kampuni ya ujenzi. NEMA inafaa kuchukua hatua na kulazimisha mwanakandarasi anayehusika kufunika mashimo haya,” akasema Bw Paul Kemoi.

Bw Kemoi ambaye shamba lake ni miongoni mwa mashamba yaliyoathirika, alisema kuwa alikuwa amekubaliana na kampuni hiyo kuziba na kujaza mashimo hatari, lakini wahandisi wa kampuni hiyo walitoweka baada ya kukamilisha ujenzi wa barabara.

Alielezea hofu msimu wa mvua unapokaribia wakazi huwa na wasiwasi kuhusu usalama wa watoto wao na hata watu wazima.

“Watoto wawili wa mmoja wetu walizama kwenye moja ya mitaro hii miaka miwili iliyopita. Licha ya wito wetu kwa viongozi kupitia NEMA hakuna kilichofanyika kuokoa hali hiyo,” alisema Bw Kemoi.

Alilalamikia NEMA kuendelea kusalia kimya, licha ya watu kutumbukia kwenye mahandaki yaliyoachwa.

“Nyumba zetu zimevamiwa na mbu wanaoendelea kuzaana kwenye mashimo. Visa vya ugonjwa wa Malaria vinazidi kuongezeka,” Margret Cherono aliwaambia wanahabari walipozuru eneo hilo.

“Kama wazazi wa watoto wadogo tunahofia usalama wa watoto wetu wanaocheza karibu na machimbo haya ya wazi,” akaongeza Bi Cherono.

Samson Rono, ambaye alipoteza watoto wake wawili baada ya kuzama kwenye shimo moja la machimbo hayo, anaitaka serikali kupokonya leseni wanakandarasi wote wanaoshindwa kuziba mashimo baada ya ujenzi wa barabara.

“Inasikitisha kuwa nimepoteza watoto wangu wawili kutokana na uzembe wa mwanakandarasi ambaye ameshindwa kufunika mitaro baada ya kuchimba nyenzo za ujenzi. Ni lazima serikali ipige marufuku wanakandarasi kama hao kufanya kazi nchini Kenya.”

Bw Cherono alijuta kwamba jaribio lake la kuishtaki kampuni hiyo ili kumlipa fidia limegonga mwamba.

Mifugo pia wameathirika kutokana na mahandaki hayo.

Veronicah Teroroi amepoteza ng’ombe wake wa maziwa baada ya kuzama kwenye timbo moja mtaani humo.

“Ng’ombe wangu wa pekee wa maziwa alizama kwenye timbo hili. Kilio changu ni kwa serikali kuingilia kati kuziba machimbo haya wazi ili kuzuia watu na mifugo kupoteza maisha,” akasema Bi Tororei.

Mkurugenzi wa NEMA Kaunti ya Uasin Gishu, Solomon Kihiu alisema afisi yake imepokea malalamishi hayo na suala hilo linashughulikiwa.

Bw Kihiu alionya kwamba wanakandarasi wanaoacha mabwawa wazi baada ya kuchimba nyenzo za ujenzi watanyimwa leseni na NEMA.

Alisema mwanakandarasi wa kimataifa anayetajwa kuhusika hajapewa cheti cha kukamilisha ujenzi wake hivyo basi ni sharti afunike matimbo hayo.

 

  • Tags

You can share this post!

Gachagua awataka viongozi wa kidini kukoma kushinikiza Rais...

Maandamano: Maina Kairu, mwenyekiti wa Azimio Nakuru...

T L