• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
GWIJI WA WIKI: Bethwel Wanjala

GWIJI WA WIKI: Bethwel Wanjala

NA CHRIS ADUNGO

KUTANA na mwanahabari Bethwel Wanjala anayelenga pia kuwa mwandishi na mhariri stadi wa vitabu ili abadilishe sura ya ujifunzaji na ufundishaji wa Kiswahili katika ngazi na viwango tofauti kimataifa.

“Kiswahili kilinibishia milango nikiwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Nilikariri mashairi na kuwakilisha shule yangu katika mashindano ya tarafa. Kuwasilisha mbele ya wanafunzi kulinishajiisha. Matokeo yangu masomoni yaliimarika nikawa miongoni mwa wanafunzi bora.”

MAISHA YAKE YA AWALI

Wanjala alizaliwa yapata miaka 24 iliyopita katika kijiji cha Sango, eneo la Kiminini, Kaunti ya Trans-Nzoia. Ndiye wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto watano wa Bw Reuben Kunani na Bi Dianah Mmali.

Alianza safari ya elimu katika chekechea ya Sisako, Moi’s Bridge, Kaunti ya Uasin Gishu (2004) kabla ya kujiunga na shule ya msingi ya Kaptien, Kitale (2005-2008) kisha Mosoriot, Trans-Nzoia (2009-2013).

Alisomea katika shule za upili za Kaptien (2014), ACK St Joseph’s Kibagenge, Kitale (2015) na Salvation Army Sirakaru, Bungoma (2016-2017). Alijiunga baadaye na Chuo cha Kiufundi cha Kenya Institute of Professional Studies (KIPS), Nairobi kusomea uanahabari na mawasiliano ya umma mnamo 2018.

Mwanahabari wa TMP Radio mjini Eldoret, Bethwel Wanjala. PICHA | CHRIS ADUNGO

Utangazaji ni kipaji kilichoanza kujikuza ndani ya Wanjala katika umri mdogo. Alitia azma ya kupalilia talanta hiyo chini ya uelekezi wa Bw Bernard Muyekho na Bw Haron Wanjala waliomfundisha katika shule ya upili.

“Nilikuwa na mazoea ya kusikiliza redio na kutangaza mpira kwa kuwaiga baadhi ya wanahabari wazoefu. Ukubwa wa uwezo wangu katika Kiswahili ulinichochea kujitosa katika taaluma ya uanahabari,” anatanguliza.

“Walimu walinipa jukwaa la kusoma makala na habari za matukio mbalimbali gwarideni. Ujasiri huo ulinoa zaidi kipaji changu cha ulumbi, nikawa mwepesi wa kukisarifu Kiswahili,” anasema.

Akiwa KIPS, Wanjala alipata fursa ya kutia sauti kwenye matangazo mbalimbali yaliyopeperushwa redioni na runingani kwa ajili ya kukivumisha chuo hicho. Picha alizopigwa akiwa nyanjani zilitiwa pia katika mabango makubwa yaliyotumiwa kutangaza KIPS jijini Nairobi.

Mnamo Oktoba 2020, baadhi ya makala aliyoandika na picha alizopiga kwa uelekezi wa mwanahabari Wairimu Gitahi wa shirika la habari la BBC zilimshindia tuzo ya kimataifa ya Mediatwenty Productions (M20Production).

Wanjala aliajiriwa na kituo cha Radio Safari, Kitale mnamo Februari 2021 kuwa msomaji wa taarifa na mtayarishaji wa makala.

Ilikuwa hadi Disemba 2011 ambapo alijiunga na TMP Radio Afrika mjini Eldoret kuwa mhariri wa taarifa za Kiswahili na mwendeshaji wa kipindi ‘Johari ya Lugha’ ambacho hupeperushwa hewani kila Jumamosi asubuhi.

You can share this post!

Presha kwa Raila

Thika Queens yajinolea CECAFA

T L