• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
GWIJI WA WIKI: Kelsy Kerubo

GWIJI WA WIKI: Kelsy Kerubo

Na CHRIS ADUNGO

KELSY Kerubo ni miongoni mwa wasanii wa humu nchini wanaoinukia vyema katika tasnia ya muziki.

Upekee wake ulingoni ni upevu wa masimulizi na wepesi wa kuita maneno ya sifa kila anapojikuta katika majukwaa ya kumtukuza Mungu.

Japo ana ndoto ya kuwa mwanahabari, kipaji cha uanamuziki kilianza kumtambalia katika umri mdogo mno. Shule za msingi alizosomea zilimpa fursa nyingi za kuwa ngoi katika mashindano ya ngazi na viwango tofauti.

Alitamba kwa urahisi kutokana na ujuzi wa kuremba maneno ya Kiswahili kwa ufundi wa kuajabiwa. Kipawa cha ulumbi kilimfanya maarufu miongoni mwa wanafunzi wenzake na akawa tegemeo la makundi ya uimbaji na uigizaji yaliyoburudisha waumini kanisani na kutumbuiza wageni shuleni.

Hata hivyo, alianza kujikuza zaidi kimuziki mnamo Mei 2020 aliposhirikiana na marafiki tisa kuunda kundi la Msanii Music Group lililoanza kufyatua nyimbo za Kiadventista (SDA) zikirekodiwa na mwasisi wa Msanii Records, Joe Nyamongo.

‘Peke Yangu Sitaweza’, ‘Asubuhi Njema’, ‘Atawale’ na ‘Kristo wa Msalaba’ ni miongoni mwa nyimbo maarufu za kundi hili lililoanzishwa na waimbaji Waadventista wa Sabato pekee kabla ya kufungulia milango waumini wa madhehebu mengine. Sasa lina takriban waimbaji 30 wanaojivunia kuchomoa zaidi ya vibao 100.

Japo Kelsy angali mwanachama wa Msanii Music, alianza kutoa nyimbo zake binafsi mnamo 2021. ‘Huru Kwa Pendo’ ni kibao alichokiachilia Machi 2021, mwezi mmoja baada ya Cherub Media kumrekodia ‘Asante’.

Vibao hivyo vilimchochea kutoa ‘Nafsi Yangu’ kabla ya kuachilia ‘Atatenda’ – wimbo uliomkweza juu zaidi katika ngazi ya muziki wa injili akiwa mwimbaji wa kujitegemea.

Kelsy aliungana na msanii Lilian Kirui kutoa kibao ‘Mungu Wa Ishara’ mnamo Agosti 2021 kabla ya kushirikiana na Charlotte Ochieng kusuka wimbo ‘Yesu Wa Huruma’ walioachilia Aprili 2022.

Mbali na wimbo ‘Nina Haja Na Wewe’ aliocharaza mwishoni mwa Oktoba 2022, kazi yake nyingine maarufu zaidi ni ‘Nitie Nguvu’. ‘Haujachelewa’, ‘Barua Yangu’ na ‘Hayafichiki’ ni baadhi ya nyimbo nyinginezo ambazo amezisana kwa Kiswahili.

Kubwa zaidi katika matamanio yake ni kuendelea kuachilia kazi zinazokubalika kimataifa huku akitambua, kukuza na kulea vipaji vya wanamuziki chipukizi.

Mbali na kuhifadhi nyimbo zake katika albamu mbili mwakani, anapania pia kushirikiana na Mercy Masika na Christina Shusho kutumia uimbaji kueneza Ukristo, kukuza maadili na kuipa jamii mwelekeo. Hawa ni miongoni mwa wasanii waliomchochea zaidi kujitosa katika tasnia ya muziki.

Mwimbaji Kelsy Kerubo wakati wa mahojiano. PICHA | CHRIS ADUNGO

Kelsy alizaliwa 1999 katika mtaa wa Sinai, Mukuru Kwa Njenga, Kaunti ya Nairobi. Ndiye mwanambee katika familia ya watoto watano wa Bi Esther Mwango na Bw Henry Okerosi.

Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Jobenpha, Sinai (2004–2009) kabla ya kuhamia shule ya msingi ya Tonga Omonuri, Nyamira (2010 –2011).

Alifanya KCPE kwa mara ya pili mnamo 2013 katika shule ya msingi ya Nyamecheo, Kaunti ya Kisii baada ya kutofaulu vyema katika jaribio la kwanza katika shule ya msingi ya Luminary Academy, Sinai, mnamo 2012.

Alijiunga na Matuu HGM Memorial Girls High, Machakos (2014 –2015) kabla ya kuhamia shule ya upili ya Nyakoiba, Kisii (2016 –2017). Kwa sasa anasomea saikolojia na soshiolojia katika Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU).

  • Tags

You can share this post!

Ripoti yaonyesha wanaume nchini Kenya wanaogopa kuoa

RIWAYA: Kielelezo cha swali la dondoo na namna ya kulijibu...

T L