• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Ripoti yaonyesha wanaume nchini Kenya wanaogopa kuoa

Ripoti yaonyesha wanaume nchini Kenya wanaogopa kuoa

NA MARY WANGARI

IDADI ya wanaume wanaokwepa kuoa humu nchini ni ya juu kuliko wanawake wanaojiepusha na maisha ya ndoa, ripoti mpya imefichua.

Ripoti ya tathmini ya sensa ya 2019 iliyotolewa Jumatano, Novemba 2, 2022, na Shirika la Takwimu Nchini (KNBS), inaonyesha kuwa idadi ya wanaume wanaozeeka bila kuoa iko juu kuliko wanawake ambao hawajaolewa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi ya wanaume wanaochelewa kuoa pia imekuwa ikiongezeka tangu miaka ya 1980s.

Katika miaka ya 1980s, kwa mfano, wastani wa umri wa wanaume kuoa humu nchini ulikuwa miaka 25 na sasa wastani ni umri wa miaka 29, kwa mujibu wa ripoti.

Wastani wa umri wa wanawake kuolewa miaka ya 1980s humu nchini ulikuwa miaka 21 lakini sasa umeongezeka hadi umri wa miaka 25.

Ongezeko la wanaume wanaokwepa au kuchelewa kuoa huenda linasababishwa na hali ngumu ya uchumi, itikadi za kidini, masomo na maamuzi ya kibinafsi.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa idadi kubwa ya wanaume hukimbilia kuoa tena mke anapofariki au kutalikiana na mke.

Hiyo inathibitishwa na idadi kubwa ya wanawake ambao walisema kuwa walikuwa wajane au walitalikiana na waume zao wakati wa sensa ya 2019.

Asilimia 7 ya wanawake walisema kuwa walikuwa wajane huku asilimia moja pekee ya wanaume wakisema kuwa walifiwa na wake zao.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa wanawake wengi wanajiepusha kupata watoto wengi ikilinganishwa na miaka iliyotangulia.

Kwa sasa, wanawake wengi wanapata jumla ya watoto watatu pekee ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita ambapo wanawake walikuwa wanapata hadi watoto saba.

Aidha, wanawake sasa wanakawia kabla ya kupata watoto ikilinganishwa na hapo zamani.

Hii inadhihirishwa katika utafiti huo ambapo wanawake wengi wanapata kifungua mimba wakiwa na umri wa miaka 25 ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita ambapo safari ya uzazi ilikuwa inaanza mapema katika umri wa miaka 20 pekee.

Isitoshe, wanawake wengi wa mijini hukimbilia kuolewa tena baada ya kufiwa, kuachana au kutalikiana na waume.

Hii ni kinyume na wenzao vijijini wanaoamua kukimu familia zao kivyao baada ya kutengana au kufiwa na waume.

Kulingana na sensa iliyopita, idadi kubwa ya wanawake mashinani walifichua kuwa wao ndio vichwa vya familia zao ikilinganishwa na wale wa mijini.

  • Tags

You can share this post!

Aliyeghushi cheti cha digrii kupata kazi benki ashtakiwa

GWIJI WA WIKI: Kelsy Kerubo

T L