• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
HADITHI FUPI: Usawiri wa wahusika katika hadithi ‘Sabina’

HADITHI FUPI: Usawiri wa wahusika katika hadithi ‘Sabina’

LEO baadhi ya wahusika katika hadithi fupi ya Sabina iliyotungwa na Winnie Nyaruri Ogenche.

WAHUSIKA

Sabina Manoti, Nyaboke, Ombati, Yunuke, binamuze Sabina akiwemo Mike na mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Utubora.

MANDHARI

Nyumbani kwao Ombati na Yunuke na shuleni.

MTIRIRIKO

Sabina alikuwa mwana wa pekee wa Nyaboke aliyempata akiwa mwanafunzi wa kidato cha pili, mimba iliyokatiza masomo yake.

Alikanwa na baba mzazi akalelewa na mamake. Alijiunga na shule ya msingi ya Utubora. Alikuwa wembe masomoni akawa anaibuka wa kwanza katika mitihani yake.

Maisha yake yaliingiwa na shaka alipofika darasa la nne. Nyaboke aliugua na hatimaye kuaga dunia kutokana na uwele usioeleweka uliofasiriwa na wanajamii kuwa ulitokana na ushirikina. Sabina akaenda kuishi na babu na nyanyake.

Akiwa katika darasa la tano, msiba ulibisha kwa mara ya pili. Babuye na nyanyake waliaga wakati mmoja. Ilimbidi Sabina agurie kwa mjombake Ombati. Huko ndiko ngomake ilifikia lele.

Yunuke, mkaza mjomba wake, alimgeuza Sabina kuwa mtumwa. Alitarajiwa kudamka kila siku na kutekeleza majukumu yake kabla ya kuenda shuleni.

Aliporejea kutoka shuleni jioni, alifanya kazi kabla ya kuandaa chajio. Alipokea matusi na vichapo wakati wowote Yunuke angehisi amekaidi maagizo. Alikosa muda wa kudurusu.

Sabina alikuwa na maono ya kupita mtihani wake wa darasa la nane na kupata ufadhili na kujiunga na shule ya upili ya hadhi nzuri.

Udhia wake ungeongezeka wakati binamuze walirejea nyumbani kwa likizo shule zilipofungwa.

Sabina alifanya kazi kuanzia macheo hadi machweo huku wao wakijistaheresha. Aliyekuwa tofauti nao ni Mike, rika la Sabina, aliyeandamana naye Sabina malishoni akiwa amebeba vitabu ili wadurusu.

Mtihani ulipowadia, Sabina alijipata matatani. Mwalimu mkuu aliwataarifu watahiniwa ya kwamba walitarajiwa kuwasili mapema kwa ajili ya mtihani. Yeyote angalichelewa angalinyimwa nafasi ya kuufanya mtihani.

Tangazo hili lilimtia shaka Sabina kwa kuwa bado alitarajiwa kutekeleza jukumu lake. Mwalimu mkuu alipodadisi kilichomtia kiwewe, Sabina alimsimulia yote yaliyomsibu. Mwalimu akabuni njia mbadala wa kuhakikisha ametimiza wajibu wake na kuufanya mtihani pia.

Ombati na Yunuke walikuwa na hakika Sabina angalianguka na Mike kufuzu vyema. Waliamua kumwoza kwa kijana mmoja mwendeshaji pikipiki. Ilisadifu siku waliofika kutoa mahari ndio siku matokeo ya mtihani yalitangazwa.

Umati ulipowasili kwake Ombati, alijifanya alikuwa ameandaa sherehe kwa ajili yake Sabina kuadhimisha ufanisi alioupata na kuibuka kati ya wanafunzi kumi bora nchini.

Ombati na Yunuke wakawa wanamwandama Sabina kila mahali. Sabina alifurahi kuwa maisha yake sasa yangebadilika kuwa mepesi.

Grace Ogoye

Kisumu Girls High School

  • Tags

You can share this post!

Jinsi programu ya ‘Ponea Patient’ inavyosaidia...

MIZANI YA HOJA: Mafanikio katika maisha ni zao la jitihada...

T L