• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
MIZANI YA HOJA: Mafanikio katika maisha ni zao la jitihada za kila siku bila kukata tamaa

MIZANI YA HOJA: Mafanikio katika maisha ni zao la jitihada za kila siku bila kukata tamaa

NA WALLAH BIN WALLAH

KOSA kubwa ambalo usifanye maishani ni kukata tamaa!

Mafanikio hayaji ghafla kama mwangaza wa umeme gizani.

Mafanikio hutafutwa kwa bahati nasibu kama vile mtu anavyomtafuta paka mweusi katika chumba chenye giza totoro!

Siyo kwamba paka mwenyewe hayumo humo chumbani mwenye giza! La, hasha!

Yumo tu lakini haonekani kwa sababu ya giza! Si ajabu mtafutaji na paka watakuwa wakipishana mumo kwa humo gizani mpaka watakapogongana kwa tukizi tu!

Hivyo ndivyo watu wanaovumilia wanavyopata mafanikio kwa tukizi wakati wao unapowadia.

Kwani kila kitu kina wakati wake maishani. Bora subira! Safari ndefu ya kilomita elfu moja huanza kwa hatua moja tu.

Tujifunze kuvumilia pasipo kukata tamaa haraka haraka! Tuelewe kwamba mafanikio yapo tu duniani lakini hayapatikani kwa papara bila kufanya kazi ya kuyatafuta!

Mafanikio hayaitwi yakaja mbio kama kuku wanaoitiwa punje za mahindi! Aidha, mafanikio hayavutwi kwa kamba kama mbuzi apelekwaye mnadani kwa dalali kupigwa bei!

Ndugu wapenzi nimeileta hoja hii kwenye mizani kwa sababu maalumu kuwaasa na kuwanasihi watu wanaotafuta mafanikio lakini wana roho nyepesi za kukata tamaa haraka wakidhani hawawezi kufanikiwa maishani!

Kwa hakika mafanikio hutokana na juhudi ndogo ndogo zinazofanywa kila siku bila ya kukata tamaa! Vumilia! Ipo siku!!!!!!!!

  • Tags

You can share this post!

HADITHI FUPI: Usawiri wa wahusika katika hadithi...

NGUVU ZA HOJA: Kabianga kuwa mwenyeji wa Kongamano la 21 la...

T L