• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 2:12 PM
HUKU USWAHILINI: Bwana, huwa tunajichosha huku sherehe hadi za talaka!

HUKU USWAHILINI: Bwana, huwa tunajichosha huku sherehe hadi za talaka!

NA SIZARINA HAMISI

WATU huku Uswahilini tumechoka.

Tumechoka na shughuli ambazo hazina tija na zinatuletea jakamoyo na wakati mwingine mvutano na wenzetu. Badala ya kupalilia utajiri kama wenzetu wa huko uzunguni, sisi tunamwagilia na kupalilia shida zinazodidimiza zaidi haya maisha yetu ambayo tayari yana changamoto nyingi.

Kawaida Uswahilini hakukosi shughuli. Huwa haipiti wiki kabla ya kusikia shughuli ikifanyika mahali fulani, zikiwemo harusi, kumtoa mwali ndani na wakati mwingine sherehe za talaka, yaani huku kwetu hadi watu wakiachana wanafanya sherehe.

Linalotuudhi ni jinsi shughuli hizi zinavyotukamua na kutuacha watupu na wakati mwingine tukiwa tumeharibu mahesabu ya mwezi mzima.

Kabla ya shughuli yenyewe kawaida watu huwa wanakutana kila juma tena katika maeneo ya baa ama starehe na huko kunahusisha kunywa hadi kusaza, wenyewe wakiita ni vikao vya maandalizi.

Vikao hivyo huchukua miezi miwili hadi mitatu.

Kwa shughuli hizi hutumia pesa nyingi, kwa jina la maandalizi.

Usipokuwa makini huku kwetu unaweza kujikuta unafanyia kazi harusi, na sherehe nyingine ambazo haziishi kila kutwa na zote utatakiwa utoe mchango wako.

Na ole wako pale utakapokataa kuchangia shughuli hizi, kwani utakuwa gumzo la mtaa. Utaimbiwa nyimbo zamafumbo na kuchambwa kila kona unayopita mtaani. Wakati mwingine hawa watu wa huku wanaweza wakususie hata pale unapopata shida ya matanga, bila kujali harusi huwa unajitayarisha lakini kifo huwa hakina hodi.

Ndiposa unapowadia muda wa hiyo harusi pamoja na mchango uliotoa, utatakiwa pia ununue sare za harusi na wakati mwingine ujumuishwe kuchangia zawadi ya wanandoa ama waliotalikiana.

Kabla ushangae kwamba talaka huku kwetu hushangiliwa, uelewe kwamba hata talaka pia ni hatua Uswahilini.

Hasa pale wanandoa wanapokuwa wamechokana baada ya mvutano na changamoto za muda mrefu, wengine wanapofikia tamati ya ndoa, huweka sherehe za kushangilia kuchomoka katika ndoa ambazo ni ndoano.

Tutaishi hivi hadi lini, hakuna anayejua, lakini haya ndio maisha yetu.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

MALEZI KIDIJITALI: Teknolojia inajenga na kuumbua familia...

DARUBINI YA WIKI: Toleo Nambari 08, Oktoba 23, 2022

T L