• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:55 PM
HUKU USWAHILINI: Huku jina unalompa mtoto wako ndilo humkaa kabisa

HUKU USWAHILINI: Huku jina unalompa mtoto wako ndilo humkaa kabisa

NA SIZARINA HAMISI

WATOTO wetu huku Uswahilini huwa wanapitia masaibu mengi mno.

Na hata ukiona mtoto kalelewa hadi kuwa mtu mzima huku kwetu, nadhani kuna haja ya kumpa tuzo kwa kuweza kuhimili mikiki mikiki na patashika za maisha ya kila siku.

Hawa watoto changamoto zao huanza pale wanapozaliwa, kwani hata majina wanayopatiwa huwa yana mengi. Watoto wa huku kwetu hupatiwa majina kulingana na hali halisi ya maisha wakati wanapozaliwa, wapo wanaopewa majina ya Chausiku, wengine wanaitwa Shida, lakini pia wapo wale wanaoitwa Semeni, Sikudhani na hata Chuki.

Sambamba na majina wanayopatiwa, hawa watoto wa huku kwetu huandamwa na patashika na heka heka tangu wakiwa wadogo. Kwani maisha ya Uswahilini yanajulikana, ni yale yaliyojaa mbio za kutafuta na kuweza kukidhi mahitaji ya siku hadi siku. Napo katika harakati hizo wazazi huwa na muda mdogo wa kuonyesha mapenzi na ukaribu na watoto. Hivyo mzazi akivurugwa kwenye shughuli zake, hasira huishia kwa mtoto, hapo utasikia mtoto akiitwa majina ya wanyama wa aina zote kuanzia paka, mbwa, fisi na hata kuku.

Tunaona akina mama waliohangaishwa na waume zao wanavyomalizia machungu kwa watoto kupitia vipigo, maneno na hata masimango. Wapo wale ambao mume anapotoweka nyumbani kwa siku kadha, watoto huenda wasipikiwe chakula na wengine wakaamua kutembeza viboko kwa watoto bila sababu yoyote ya msingi.

Hawa watoto wetu pia wakija huku mtaani huwa wananyemelewa na binadamu wala watu, wale ambao wana sifa ya kuharibu watoto na kuharibu maisha yao, yaani wale wabakaji na wengine wanaodhulumu utoto wao.

Watoto hawa wa Uswahili wanapokuwa watu wazima ni wachache ambao wanaweza kumudu maisha na kuishi katika hali ya kawaida. Kwani kwa watoto wa kiume, wengine waliopitia maisha haya ya patashika, nao pia huendeleza patashika hizi katika familia zao. Ndiposa wanakuwa waliotawaliwa na hasira waliokosa upendo kwa wake zao na watoto pia na wengine wanakuwa ni wataalam wa kupiga wake na hata watoto wao.

Halafu wapo wale ambao wanakuwa hawana habari na majukumu ya familia, anajijali yeye na nafsi yake bila kujua watoto wanasoma vipi, wanakula nini, wanavaa nini na hata huduma za nyumbani zinapatikanaje.

Kuna kila sababu ya kuwapa tuzo wale waliolelewa Uswahilini na wakaweza kumudu maisha yao baadaye.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

MALEZI KIDIJITALI: Mafunzo ya malezi dijitali kwa wazazi...

Mbwa na punda kuchanjwa dhidi ya kichaa cha mbwa

T L