• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
MALEZI KIDIJITALI: Mafunzo ya malezi dijitali kwa wazazi yaja

MALEZI KIDIJITALI: Mafunzo ya malezi dijitali kwa wazazi yaja

JUHUDI za kuhakikisha kwamba wazazi nchini wamekumbatia malezi dijitali zimepigwa jeki baada ya wadau kuungana na kuzindua mpango wa kuwafunza wazazi na walezi.

Ili kufanikisha mpango huo wa mafunzo ambayo wataalamu wanasema hayaepukiki ikizingatiwa hatari inayokodolea watoto, Bodi ya Kutathmini Filamu ya Kenya (KFCB) imeshirikiana na Netflix, Google, TikTok na wadau wengine.

Mpango huo mpya unaofahamika kama Elimu ya Malezi Dijitali kwa wazazi (PaDiL) utawapa wazazi na walezi ujuzi unaohitajika kuwaongoza katika matumizi salama ya majukwaa ya dijitali.

Wataalamu wa malezi dijitali wanasema PaDiL utahamasisha wazazi na walezi kuhusu athari za maudhui na tekinolojia ibuka kwa watoto.

Kulingana na Katibu wa Idara ya Masuala ya Vijana na Sanaa, Bw Ismail Maalim Madey mpango huo utawezesha wazazi kulinda watoto mtandaoni na kuhakikisha usawazishaji kati ya biashara na usalama wa watoto katika tekinolojia ya dijitali.

“Huu ni mpango mzuri ikizingatiwa kwamba Kenya ina intaneti kote na ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa upatikanaji wa intaneti Afrika. Kutokana na hilo, matumizi ya ICT, ikiwemo mitandao ya kijamii, yamekuwa kote nchini hasa miongoni mwa vijana na watoto,” alisema.

Mpango huo ulizinduliwa wakati wa maadhimisho ya 10 ya Siku ya Usalama wa Intaneti.

Katibu Maalim anakubaliana na wataalamu kwamba usawazishaji ni muhimu katika matumizi ya mtandao ya watoto na vijana.Ingawa wataalamu wanatambua jukumu chanya la intaneti kwa watoto na nafasi inazotoa, wanasema intaneti pia inaweza kuletea watoto matatizo.

“Utafiti umeonyesha kuwa upatikanaji wa intaneti miongoni mwa watoto unawafaidi kimasomo. Katika kiwango kikubwa, upatikanaji wa intaneti ya kasi ya juu umegunduliwa kuchangia maendeleo ya uchumi na kuimarisha viwango vya maisha vya raia, wakiwemo watoto. Rasilmali hii pia inatoa nafasi nyingi kwa burudani na mawasiliano miongoni mwa vijana,” alisema.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa KFCB Christopher Wambua anasema kwamba wazazi na walezi ni muhimu kwa watoto na hivyo basi kuna haja ya kuwapa ujuzi wanaoweza kutumia kusaidia watoto wanaowalea kutumia dijitali salama.

  • Tags

You can share this post!

PENZI LA KIJANJA: Eti anataka umzalie kabla akuoe? Toroka!

HUKU USWAHILINI: Huku jina unalompa mtoto wako ndilo humkaa...

T L