• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:55 PM
HUKU USWAHILINI: Jamani ndoa zimekuwa ngumu huku kwetu, lalama kila mahali

HUKU USWAHILINI: Jamani ndoa zimekuwa ngumu huku kwetu, lalama kila mahali

NA SIZARINA HAMISI

HUKU kwetu idadi kubwa ya wanawake walio kwenye ndoa wanateseka na ndoa zao.

Wanaishi ili mradi siku ziende na wala sio kwa amani na furaha kama inavyotakiwa.

Wakati mwingine msituone tunacheka na kufurahi tunapokutana kijiweni, huwa tunayasikia mengi na ukweli ni kwamba wengi wanateseka kwenye ndoa zao huku wakitabasamu.

Kwenye haya mazungumzo yetu ya huku kwetu, nimeongea na wanawake kadha na walio wengi hawana raha ya ndoa au tuseme wanavumilia huku miaka inaenda wakiwa ndani ya mateso makali.

Wapo wale wanaolia kila siku, kwani wamebebeshwa jukumu la kulea na kutunza familia bila ya usaidizi wa waume zao, ambao hawachangii hata senti.

Na kama hiyo haitoshi, wanaume hawa wamekuwa wakatili na wenye roho za unyama kwani kuna mashoga zangu wanaojikuta wamefungiwa nje bila huruma na wengine hadi kufukuzwa kutoka kwenye nyumba zao, kutukanwa na kudharauliwa, kupigwa na hata kuachiwa ulemavu.

Wakati mwingine hawa wanaume wanapoona kwamba mke anakomaa na kuishi na mateso bila kulalamika ama kuonyesha dalili za kujali, basi wanaamua kutelekeza kabisa familia na kutokomea kusikojulikana.

Mwanaume anaweza akapotea kabisa nyumbani na baada ya miaka kumi hadi ishirini ndio anarudi na watoto wanamfurahia bila kuelewa jinsi mama alivyobeba jukumu lote la kulea na kutunza familia.

Wanaume hawa wapo huku kwetu Uswahilini na tunawaona kila siku, sema tunawasitiri sababu siri ya kata aijuaye ni mtungi.

Halafu wapo marafiki zangu ambao wanateseka na matukio ya hao waume zao, hawa wanaume zao wanahudumia familia bila shaka, isipokuwa wameamua kuwatesa kwa ukahaba, kwani wanakosa uaminifu katika ndoa zao na wakati mwingine wameishia kuwaambukiza wake zao magonjwa ya zinaa ukiwemo ukimwi na hata wanapotenda ukatili huo bado wanaendelea kuwatumikisha wake zao kama vile ni punda.

Hivyo huku kwetu kuna maibilisi wanaoishi katika miili ya binadamu kwa vitendo na matukio wanayowatendea wenzao na kupelekea wengine kuishi wakiwa na msongo wa akili na wengine kusinyaa na kukosa afya.

Hili jambo limeota mizizi huku kwetu ambapo wanawake wengi wamekuwa wanaonewa na waume zao bila kusema popote wakijua ndoa ni kuvumilia kumbe wanajiua taratibu pasipo kujua wanajikausha maisha yao sababu ya wale wanaoishi nao.

Hivyo wenzetu, msituone tunacheza kibao kata, taarab na wakati mwingine kusutana na matarumbeta, yanayojiri huku kwetu ni mengi sana.

  • Tags

You can share this post!

DINI: Mstari kati ya wema na ubaya ni mwembamba

Leicester wakataa Sh5.7 bilioni ambazo Newcastle wametoa...

T L