• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
HUKU USWAHILINI: Huku kwetu siku zote purukushani!

HUKU USWAHILINI: Huku kwetu siku zote purukushani!

NA SIZARINA HAMISI

MAISHA ya Uswahilini siku zote ni purukushani.

Kwani hata ukimsaidia jirani yako chakula, omba kisije kikamdhuru. Kwani kimkikataa tu, augue tumbo ama ugonjwa wowote kuhusiana na chakula ulichompa, utambue huo ni muziki utakaoucheza hadi asubuhi ama kwa siku kadha. Unaweza ukaitwa mchawi au una roho mbaya.

Halikadhalika kuna vituko vingine vinatokea na wengine hubaki tukitisa vichwa na sio kwa huzuni wala furaha bali kwa hisia mchanganyiko. Wapo majirani wengi, mmojawapo akiwa ni dada ambaye amepanga chumba kimoja na anaishi na mtoto wake. Huyu dada hafanyi kazi, na hata biashara ndogo hatujamuona akijishughulisha na huwa mara nyingi tunamuona mtaani, akiishi bila kikwazo wala changamoto yoyote.

Udadisi wetu ukabaini ana wanaume watatu wanaomhudumia bila kutambuana. Mmoja wao ni polisi, mwingine bodaboda na watatu ni mfanyabiashara. Mchanganyiko zaidi ni kwamba kati ya hao watatu, wawili ni waume za watu isipokuwa bodaboda ambaye hajaoa. Halafu wote hao watatu ni baba wa mtoto wake kwa nyakati tofauti.

Alijua kuwapanga hawa wanaume, kila mmoja kwa wakati wake na akitoa huduma kwa mtoto kwa nafasi yake. Lakini hizi harakati huwa zinafika ukingoni. Siku mtoto aliugua, aliwataarifu baba zake wote watatu. Yule mfanyabiashara akatuma pesa sababu alishindwa kuja. Naye polisi akamweleza angekuja kesho yake. Bodaboda akaahidi kufika baadae akipata nafasi ili ampeleke hospitali.

Siku ya pili, polisi akaja akaandaliwa chakula kwanza ale ili wampeleke mtoto hospitali. Wakati wakiwa wote ndani, bodaboda naye akaja kuangalia mwanae mgonjwa. Alipofungua mlango akamkuta polisi anajivinjari misosi huku mama mtoto na mtoto wamekaa pembeni yake.

Yule mama akashtuka na kusimama ghafla kama kaona jini. Akamkaribisha jamaa akaingia ndani akasalimiana na yule polisi bila kujua ni mume mwenzi. Bodaboda akamkaribisha polisi na kumtambulisha kwamba pale ni kwake na ile ni familia yake.

Polisi akabaki amepigwa na butwaa na kuuliza kulikoni. Kilichofuata ni vita vya ngumi baina ya wanaume wale wawili na yule mama akamchukua mtoto na kupiga kelele za kuomba usaidizi kwa majirani.

Mashuhuda tulikuwa wengi na habari ikawa ni ndefu. Majadiliano yaliyofuata baada ya hapo yaliwatambulisha baba hao wawili wa mtoto mmoja na kuwa mwisho wa uhusiano na huyu jirani yetu.

Utaniambiaje nihame huku kwetu, maisha yetu tunayajua wenyewe!

You can share this post!

Leads United yataka taji la Koth Biro

Wajackoyah aahidi kuhalalisha chang’aa akiwa rais

T L