• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
HUKU USWAHILINI: Riziki ni mafungu saba ila huku kwetu ni robo fungu

HUKU USWAHILINI: Riziki ni mafungu saba ila huku kwetu ni robo fungu

NA SIZARINA HAMISI

IGAWA inajulikana kwamba riziki ni mafungu saba, huku kwetu Uswahilini riziki yetu ni robo fungu.

Kwamba pamoja na kuwepo njia na mbinu nyingi za kujipatia kipato na kuendesha maisha, huku kwetu njia zilizopo ni ngumu na zinatoa jasho.

Wapo akina dada ambao maisha yao ni magumu lakini kutwa kucha ni kujitunisha misuli vijiweni na kujidai mambo ni mazuri, wakati sote tunajua hata mlo mmoja ni mgogoro.

Hawa ni mafundi wa mashindano, katika harakati za kuonyesha kwamba wameyapatia maisha kumbe wanahemea masikioni kwa dhiki na changamoto za maisha.

Tunaoelewa maisha yetu huku huwa hatuwalaumu, bali tunaangalia uwezekano na nafasi ya kuwanyoosha na kuwarudisha kwenye uhalisia. Na ndio maana wale wanaokuja na kelele za kujisifu na kujikwaza, huwa tunawaangalia kwa jicho la tatu.

Wapo wale walio maarufu kwa kuazima nguo za kisasa kutoka kwa marafiki zao wa huko uzunguni na kuja kutuonyesha jinsi walivyoyapatia maisha.

Hapa utakuta msichana akihangaika kuzunguka mtaani kama kuku aliyekatwa kichwa ilimradi tu aonekane amevaa nguo ya aina fulani. Halikadhalika wapo wale ambao wanapotoka sokoni watahakikisha wanapita maeneo yote ya kijiweni wakiwa na kapu lililojaa bidhaa ilimradi waonekane kwamba hali yao ni shwari.

Tunawajua wote hawa na tunapopata nafasi huwa tunawachambua vilivyo na kuwaeleza ukweli wa maneno.

Hata hivyo wapo wengine ni wachapa kazi na haijalishi ni kazi gani ilimradi mkono uende kinywani.

Hawa ni wale na hata wakati mwingine akina kaka utakaowakuta wakipambana katika biashara ndogo, wengine wakisafisha mitaro ya maji machafu na wengine wakiponda kokoto ili kuingiza kipato cha kujikimu kimaisha.

Riziki yetu inakuja kwa juhudi za ziada na wakati mwingine hizo juhudi zinashindwa kuzaa matunda na sio ajabu ukipata tunasaidiana. Kwani tunaelewa shida na tunaiishi bila kinyongo wala hasira.

Hivyo wanapojitokeza wale wanaoishi maisha ya kuigiza huwa tunawatambua mara moja na sababu hatuna unafiki, tunawaeleza bayana pale nafasi inapopatikana.

Kuhusu yule jirani yetu muazima mavazi ya watu, juzi amejifunza somo kwa hii tabia yake, kwani huko alikoenda kuazima nguo walimchoka na mwenye mavazi yake akafika huku kwetu kumdai, tena bila kuficha na kumtangaza hadharani.

Leo ni wiki ya pili hatujamuona. Tunamngoja arudi, tumpe mbinu za kuishi maisha halisi.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mwisho wa lami kwa Sonko kisiasa

PENZI LA KIJANJA: Epusha mpenzi na marafiki mafisi vilabuni

T L