• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Mwisho wa lami kwa Sonko kisiasa

Mwisho wa lami kwa Sonko kisiasa

NA CHARLES WASONGA

CHAMA cha Wiper kimepata pigo kubwa baada ya Tume ya Uchaguzi (IEBC) kumzima aliyekuwa gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko kuwania kiti hicho katika Kaunti ya Mombasa.

Kwenye kikao na wanahabari katika ukumbi wa Bomas of Kenya, Nairobi, Jumamosi, mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati alisema Bw Sonko hajahitimu kuwania kiti chochote cha umma kwa msingi kuwa aliondolewa afisini 2020 kwa matumizi mabaya ya mamlaka, miongoni mwa maovu mengine.

“Kwa msingi wa kipengele cha 75 (3) cha Katiba, watu ambao waliondolewa mamlakani kwa kukiuka hitaji la Sura ya Sita ya Katiba kuhusu Maadili na Uongozi Bora, hawawezi kuruhusiwa kushikilia afisi ya umma kwa kuchaguliwa au kuteuliwa,” akasema.

Bw Sonko ni kati ya wawaniaji 241 ambao Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imependekeza kuwa wasiruhusiwe kuwania viti mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 kwa msingi wa kutohitimu kimaadili.

Mbali na Bw Sonko, Chitavi Antony Mkhala, ambaye pia alikuwa anawania ugavana wa Mombasa, na Karungo wa Thangwa anayewania useneta wa Kiambu, pia wamezimwa kushiriki uchaguzi mkuu ujao kwa msingi wa kufeli kutimiza matakwa ya Sura ya Sita ya Katiba.

Bw Chitavi alipata cheti cha chama cha United Democratic Party (UDP) kuwania ugavana wa Mombasa, hali Bw Wa Thang’wa alikuwa ameshinda tiketi ya chama cha UDA kupeperusha bandera yake katika kinyang’anyiro cha useneta, Kaunti ya Kiambu.

“Msimamo wa tume hii ni kwamba kipengele cha 75 cha Katiba kiko bayana na ni rahisi kutekelezwa. Hakina ibara nyingine ambayo inaweza kumwokoa mtu. Kwa hivyo, wawaniaji hao watatu walioondolewa afisini kwa kosa la matumizi mabaya ya mamlaka yao hawawezi kuruhusiwa kuwania viti vingine katika uchaguzi wowote nchini Kenya,” akasema Bw Chebukati.

Bw Sonko alitimuliwa afisini kama gavana wa Nairobi mnamo Desemba 20, 2020 na madiwani wa bunge la kaunti hiyo.

Alikabiliwa na makosa manne ya ukiukaji wa Katiba, matumizi mabaya ya mamlaka ya afisi yake, mienendo mibaya, ufisadi miongoni mwa makosa mengine.

Hatua hiyo baadaye iliidhinishwa na Seneti na kumfanya Bw Sonko kuwa gavana wa kwanza nchini kutimuliwa afisini tangu kuanzishwa kwa utawala wa ugatuzi mnamo 2013.

Mnamo Machi 16, chama cha Wiper kilimteua kuwa mgombea wake wa ugavana katika kaunti ya Mombasa.

Mbunge wa Kisauni, Ali Mbogo ambaye awali alikuwa akitaka kuwania kiti hicho kwa tiketi ya Wiper alishauriwa kuwa mgombea mwenza wa Bw Sonko. Alitii ushauri wa chama hicho kinachoongozwa na makamu wa rais wa zamani Kalonzo Musyoka.

  • Tags

You can share this post!

Mucheru adai Chebukati aibia Ruto siri

HUKU USWAHILINI: Riziki ni mafungu saba ila huku kwetu ni...

T L