• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 6:55 AM
IEBC: Kilio cha Raila kinampa Ruto maksi

IEBC: Kilio cha Raila kinampa Ruto maksi

NA LEONARD ONYANGO

MALALAMISHI ya mwaniaji wa urais wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga dhidi ya Tume ya Uchaguzi (IEBC) huenda yakampa nguvu mpinzani wake mkuu Naibu wa Rais William Ruto huku zikiwa zimesalia siku 29 kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Wadadisi wanaonya kuwa malalamishi ya mara kwa mara ya Bw Odinga kuhusu madai ya kuwepo njama ya mrengo wa Kenya Kwanza kuiba kura yatawakatisha tamaa wafuasi wake na kusababisha idadi ndogo kujitokeza Agosti 9.

Bw Odinga amekuwa akidai kuwa mrengo pinzani wa Kenya Kwanza unashirikiana na baadhi ya maafisa wa IEBC kuiba kura za urais.

Kulingana na muungano wa Azimio, hatua ya IEBC kutangaza kuwa itatumia mitambo ya kielektroniki kutambua wapigakura ni kati ya mbinu ambazo wapinzani wake wanatumia kuiba kura.

“Ni sharti IEBC itumie sajili iliyochapishwa na ile ya kielektroniki kutambua wapigakura Agosti 9. Bila kufanya hivyo, hakutakuwa na uchaguzi,” alifoka Bw Odinga alipokuwa akihutubia mkutano wa kisiasa katika eneo la Gatundu, Kaunti ya Kiambu, Jumatano.

Siku iliyofuatia alipokuwa katika Kaunti ya Kirinyaga, Bw Odinga aliendelea kuonya Bw Chebukati dhidi ya ‘kujaribu kuiba kura’.

Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohamed alidai kuwa muungano wa Kenya Kwanza ulishirikiana na IEBC kupitisha karatasi za kura nchini Uganda na kisha kuziingiza humu nchini kisiri.

“Hata tunajua kuwa kuna kamishna aliyenunuliwa nyumba Pwani na watu wa Kenya Kwanza. Tutawafichua,” akadai Bw Mohamed bila kutoa ushahidi.

Ajenti Mkuu wa Azimio, Saitabao Kanchory pia ameandikia barua IEBC akilalamika kuwa idadi kubwa ya maafisa wa kusimamia uchaguzi katika ngazi ya maeneobunge pamoja na manaibu wao, wanatoka katika eneo la Bonde la Ufa ambalo ni ngome ya Dkt Ruto.

Kulingana na Bw Kanchory, asilimia 17 ya maafisa wasimamizi wa uchaguzi katika ngazi ya maeneobunge, wanatoka Bonde la Ufa na wamepelekwa kusimamia kura katika eneo hilo.

“Hatua hiyo itatoa mwanya kwa mrengo wa Kenya Kwanza kutumia maafisa hao kuiba kura,” akasema Bw Kanchory kupitia barua yake kwa mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati.

Muungano wa Azimio pia unataka kujua majina ya maafisa watakaosimamia uchaguzi katika maeneobunge 21 ambayo yaliachwa wazi katika orodha ya wasimamizi iliyochapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali mnamo Aprili 2022.

Bw Kanchory alikuwa ametoa makataa ya hadi Alhamisi, Julai 7, 2022 kwa IEBC kushughulikia suala la ukabila miongoni mwa wasimamizi wa uchaguzi katika maeneobunge.

Lakini Jumamosi, Bw Kanchory aliambia ukumbi huu kuwa hajapokea ufafanuzi kutoka kwa IEBC.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa malalamishi hayo mengi ya Bw Odinga yatawakatisha tamaa wafuasi wake na huenda wakakosa kujitokeza kupiga kura Agosti 9 kutokana na imani kuwa uwezekano wa kushinda ni mfinyu.

“Tayari Ruto anatumia malalamishi hayo ya Bw Odinga kujipigia debe huku akisema kuwa hiyo ilikuwa ishara ya kuonyesha kuwa wamehisi kwamba watapoteza uchaguzi Agosti 9,” anasema Bw Javas Bigambo, mdadisi wa masuala ya kisiasa.

Kulingana na Bw Bigambo, malalamishi hayo ya Bw Odinga pia yanatoa taswira kuwa amelemewa maarifa na Dkt Ruto.

Prof Medo Misama anasema kuwa malalamishi hayo ya Bw Odinga kuhusu ukabila ndani ya IEBC pia yanamtia doa.

“Bw Odinga amekuwa akijigamba kwamba analenga kuunganisha nchi kupitia muungano wa Azimio. Hivyo, kuanza kulalamika kwamba jamii fulani ina watu wengi ndani ya IEBC inaonyesha taswira ya unafiki,” anasema Prof Misama ambaye pia anawania ubunge wa Suba Kusini kama mwaniaji huru.

Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya wapigakura waliojitokeza katika uchaguzi wa Agosti 8, 2017 katika ngome za Bw Odinga ilikuwa chini ikilinganishwa na 2013.

Ni kaunti nne pekee katika ngome ya Bw Odinga ambapo idadi ya wapigakura waliojitokeza 2017 walikuwa asilimia 80 na zaidi ya watu waliojisajili.

Wadadisi wanasema kuwa kuna uwezekano kwamba wafuasi wa Bw Odinga walikosa kujitokeza kupiga kura kutokana na imani kwamba ingekuwa vigumu kumshinda Rais Uhuru Kenyatta.

  • Tags

You can share this post!

HUKU USWAHILINI: Si ajabu mwanamume kutoroka kwake, kisa...

Viongozi duniani waomboleza Abe

T L