• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 8:09 PM
JAMVI LA SIASA: Uasi mpya watishia kuvuruga ODM

JAMVI LA SIASA: Uasi mpya watishia kuvuruga ODM

NA CHARLES WASONGA

MUSTAKABALI wa chama cha ODM kinachoongozwa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, uko hatarini kutokana na uasi ambao umechipuza miongoni mwa wabunge wake.

Baadhi ya wabunge kutoka ngome yake ya Luo Nyanza sasa wanataka wanasiasa ambao wameshikilia nyadhifa za juu katika chama hicho kwa muda mrefu wajiondoe ili kutoa nafasi kwa viongozi wapya ambao wanaweza kukipa chama hicho “nguvu mpya”.

Wakiongozwa na mbunge wa Gem Elisha Odhiambo, wabunge hao wanasema ODM inahitaji uongozi mpya ambao utaiwezesha kutamba katika uchaguzi mkuu wa 2027 na hata kushinda urais.

Walio katika kambi hii ni pamoja na Caroli Omondi (Suba Kusini) na Aduma Owuor (Nyakach), miongoni mwa wengine.

Lakini kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi amepuuzilia mbali wabunge hawa, akiwataja kama waliopoteza mwelekeo huku akiwataka kujizulu kutoka ODM badala ya kukipiga vita wakiwa ndani.

Bw Odhiambo anasema kuwa baadhi ya maafisa wa sasa wa ODM wamekuwa wakikihujumu chama kichinichini badala ya kukivumisha kiweze kupenya katika ngome za vyama vingine pinzani.

“Uongozi wa sasa wa ODM ni butu. Hauna msukumo, ilhamu na nguvu za kukiwezesha kutwaa mamlaka nchini. Badala ya kukiendeleza, baadhi ya maafisa hao ndio wamegeuka wasaliti wakubwa wa ODM,” mbunge huyo akasema bila kutaja majina ya maafisa hao.

Hata hivyo, mwezi Novemba, Bw Odhiambo, anayehudumu muhula wa pili bungeni, alinukuliwa akisema kuwa atawania kiti cha Katibu Mkuu wa ODM “uchaguzi wa chama utakapoitishwa.”

Wadhifa huo, wenye nguvu na usemi mkubwa chamani, sasa unashikiliwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna.

Hata hivyo, Bw Sifuna ametangaza kuwa yu tayari kupambana na Odhiambo wakati huo ukiwadia.

Kwa upande wake, Bw Odoyo amesema: “Tumegundua kuwa watu ambao wamekuwa wakiongoza ODM sasa wamechoka. Tunataka viongozi wapya ambao wataipa ODM sura mpya kabla ya uchaguzi mkuu ujao.”

Naye Bw Omondi, anayehudumu muhula wa kwanza kama mbunge wa Suba Kusini, amependekeza kutimuliwa kwa mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed.

Anamshutumu mbunge huyo ambaye ni kiranja wa wachache katika Bunge la Kitaifa kwa kuvuruga uchaguzi wa urais na kuchangia kushindwa kwa Bw Odinga na Rais William Ruto kwa kura 200,000.

Bw Omondi ndiye mbunge wa pekee wa ODM kutoka Luo Nyanza ambaye amekuwa akiandamana na Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na Uchumi wa Kidijitali Eliud Owalo katika shughuli zake za kugawa chakula cha msaada kwa wakazi wanaoathiriwa na njaa katika eneo hilo.

Lakini Bw Wandayi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Masuala ya Kisiasa katika ODM sasa anawataka wabunge waasi kugura chama hicho ili viti vyao vitangazwe wazi na uchaguzi mdogo uitishwe.

“Badala ya kumpiga vita Raila Amolo Odinga kwa kisingizio cha kuitisha mageuzi ndani ya ODM, nawapa wabunge hawa changamoto moja. Wajiuzulu na wahamie vyama wanavyojihusisha navyo. Watoe nafasi kwa wakazi wa maeneobunge yao kuwachagua wabunge wapya ambao watakuwa waaminifu kwa ODM,” akasema kwenye mahojiano na jarida hili kwa njia ya simu.

Hata hivyo, wachanganuzi wa siasa za Luo Nyanza wanasema kuwa tatizo kuu katika uongozi wa ODM, eneo hilo na hata kitaifa ni Bw Odinga mwenyewe.

“Odinga ambaye ameongoza ODM kwa miaka 18 tangu kilipobuniwa mnamo 2005 anaonekana kuwaamini zaidi baadhi ya viongozi ambao kwa kweli hawaleti manufaa yoyote katika chama hicho. Mabadiliko yataafikiwa katika ODM ikiwa Raila atakubali kwamba chimbuko la matatizo yanayokisibu ni baadhi ya maafisa wake anaowaamini kupita kiasi,” anasema Dkt David Ochieng’ ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Katika Bunge la sasa la 13, ODM ina wabunge 86 na maseneta 22. Katika ngazi za kaunti magavana 18 walichaguliwa kwa tiketi ya ODM.

Hii ni tofauti na katika Bunge la 12 ambapo ODM ilikuwa na wabunge 93, maseneta 25 na magavana 22.

  • Tags

You can share this post!

Mswada wa kusuluhisha mvutano kuhusu upande wa walio wengi...

Broadway yawapa wakongwe na watoto chakula wajienjoi

T L