• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Kananu kaangukia minofu kweli

Kananu kaangukia minofu kweli

Na BENSON MATHEKA

GAVANA wa Nairobi Ann Kananu Mwenda anaweza kufananishwa na mtu aliyeangukia kiti hicho kwa kuwa ndiye gavana wa pekee ambaye hakushiriki uchaguzi mkuu wa 2012.

Magavana wengine walioingia mamlakani baada ya uchaguzi huo kama vile Mutahi Kahiga wa Nyeri, Hillary Barchok wa Bomet na James Nyoro wa Kiambu walikuwa wagombea wenza na manaibu gavana kabla ya kiti kubaki wazi kufuatia vifo au kuondolewa ofisini kwa wakubwa wao.

Hata hivyo, hakuna aliyemfahamu Bi Kananu kabla ya kupendekezwa na aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko kuwa Naibu wake Januari 2020.

Japo Kananu alikuwa afisa mkuu wa idara ya mikasa katika serikali ya kaunti ya Nairobi, hakuna aliyetarajia angependekezwa kujaza kiti kilichobaki wazi baada ya kujiuzulu kwa Polycarp Igathe ambaye alikuwa mgombea mwenza wa Bw Sonko kwenye uchaguzi mkuu wa 2017.

Wadadisi wa siasa wanasema Bw Sonko ambaye kwa takriban miaka mitatu alihudumu bila naibu hata baada ya seneti kupitisha sheria iliyoruhusu magavana kuteua manaibu viti hivyo vikibaki wazi, alipotoshwa au alijikaanga kwa kumpendekeza Bi Kananu kwa wadhifa huo.

“Sonko alipotoshwa kumteua Kananu akidhani alikuwa akizima shinikizo za kutaka ajaze kiti hicho. Hii iliharakisha kuondolewa kwake ofisini na alipogundua njama ya wapinzani wake, akajaribu kusitisha mchakato wa kumteua Kananu lakini akawa amechelewa,” asema mdadisi wa siasa za Nairobi Mike Oluoch.

Kulingana na Oluoch, Kananu alibadilika kuwa mradi wa serikali pale Bw Sonko alipotofautiana na serikali, akashtakiwa kwa ufisadi na akahamisha majukumu muhimu kwa serikali ya taifa.

“Kananu alibadilika kuwa mradi wa serikali na ikamsaidia kuteuliwa naibu gavana huku Bw Sonko, baada ya kugundua alijikaanga kwa kumpendekeza, akitumia mahakama kuchelewesha kuteuliwa kwake. Kananu alilazimika kusubiri Kwa miezi kumi kabla ya kuwa gavana wa tatu wa kaunti ya Nairobi asiyejua gharama ya uchaguzi,” asema Oluoch.

Kulingana na wadadisi, Bi Kananu alisaidiwa na serikali ya Jubilee kuwa gavana miezi mitatu kabla ya kipindi cha Idara ya Huduma ya Jiji la Nairobi (NMS) ambalo Rais Uhuru Kenyatta aliteua baada ya Sonko kuhamisha majukumu muhimu kwa serikali ya taifa kukamilika Februari 2022.

Muda wa NMS inayosimamiwa na Meja Jemedari Mohamed Badi unakamilika Februari 25 na kuna dalili kwamba huenda usiongezwe baada ya idara hiyo kukosa kutengewa pesa katika bajeti ya mwaka ujao wa kifedha.

Hata hivyo, wadadisi wanasema Bi Kananu akiwa mradi wa serikali, anaweza kudumisha idara hiyo na ifadhiliwe na serikali ya kaunti.

Katika hotuba yake baada ya kuapishwa kuwa gavana, Kananu aliahidi kushirikiana na NMS na Bunge la Kaunti ya Nairobi kuboresha huduma kwa wakazi wa Nairobi.

“Ikizingatiwa kwamba alibadilishwa au alikuwa mradi wa kumtimua Bw Sonko ambaye licha ya kutia saini mkataba wa kuhamisha majukumu alikataa kushirikiana na NMS, Bi Kananu atakuwa kibaraka wa serikali kwa miezi kumi ambayo atakuwa gavana wa Nairobi,” anasema mchanganuzi wa siasa Francis Kariuki.

Kulingana naye, Bi Kananu hakujiweka katika kiti cha gavana kaunti ya Nairobi na kwa hivyo hatakuwa na uhuru wa kufanya maamuzi.

“Ni wazi kuwa aliangukia minofu baada ya kutumiwa kuharakisha kuondolewa ofisini kwa Bw Sonko. Kwa msingi huu, hatakuwa na uhuru au uwezo wa kufanya maamuzi. Atatumiwa na waliomsaidia kutekeleza na kutimiza maslahi yao. Kwa mfano, mitaa kadhaa ya mabanda imeanza kubomolewa na maelfu ya watu kukosa makao akinyamaza kwa kuwa hakuomba kura,” asema Kariuki.

Mchanganuzi huyu anasema kuwa kiti cha ugavana kaunti ya Nairobi ni muhimu sio tu kwa serikali iliyo mamlakani bali pia kwa wafanyabiashara na wanasiasa wanaonufaika na minofu iliyoko jijini.

“Hii ndiyo kaunti iliyo na mapato mengi, kitovu cha biashara haramu na halali na makao makuu ya serikali ya kitaifa na kwa hivyo, lazima anayekuwa gavana ashirikiane na serikali. Bi Kananu alipata wadhifa huo kwa kuwa aliwekwa kwenye mizani na akapatikana kuwa asiye na misimamo mikali. Kumbuka hakuchaguliwa na wakazi kwa hivyo hawajibiki kwa wapiga kura kama watangulizi wake bali anawajibika kwa waliomuweka ofisini,” asema Kariuki.

You can share this post!

Filamu ya ‘Monica’ ilichangia ajiunge na...

Kocha Xavi ashinda mechi yake ya kwanza akidhibiti mikoba...

T L