• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 7:55 AM
KINAYA: Wenye hisa za Kenya wakate miti tusijinyonge!

KINAYA: Wenye hisa za Kenya wakate miti tusijinyonge!

NA DOUGLAS MUTUA

HIVI una hisa za kumiliki Kenya au unatoka kabila ‘sosa’?

Naambiwa umiliki wa nchi hii, ambayo inachukuliwa kama kampuni binafsi, unadhibitiwa na jamii mbili kubwa. Sijui tangu lini, ila nasikia wengine hatuna maana, nchi inaweza kuendelea, tuwepo tusiwepo. Na tukiungulika sana tujitie kitanzi eti. Hawatujali!

Hii inanikumbusha kauli iliyojaa maudhi, akipenda kuitumia sana yule ‘Mzee wa Nyororo’ Atwoli, wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2022: “Kateni miti!”

Alimaanisha watu wa Kijiji cha Sugoi wakate miti ili, iwapo mwanao maarufu angebwagwa na ‘Babaman’, asipate hata mti mmoja wa kujitilia kitanzi. Watu hawana huruma aisee!

Hata hivyo, nikitafakari sasa naona mzee huyo alikuwa muungwana kwa kiasi fulani; asiyekutakia mauti ni mtu na utu, hata ikiwa anakukejeli kwa masaibu yako.

Anakutaka humu duniani ili ushuhudie mbwembwe na madaha yake, na bado ukiungulika usijinyonge uzoee maudhi yake tu. Ajabu!

Katika muktadha wa siasa za Kenya wakati huu, basi nadhani jamii mbili kubwa ambazo zinaongoza nchi kama kampuni ya hisa zinapaswa kuwa na utu kidogo.

Hata zikitunyima kazi serikalini, yaani zitwae karibu asIlimia 60 na kutuachia asilimia 40, heri zisitutakie mauti.

Pamoja na kunyakua kazi zote zenye mishahara minono, jamii hizo zinaweza kufanya hisani ya kukata miti, hasa tunakoishi makabila ‘sosa’, ili tusipate kwa kujinyongea.

Zinatuhitaji humu ili angaa tuzisaidie kubeba mzigo mzito wa madeni na pia kuwalipa mishahara viongozi na wafanyikazi hao maalumu. Ama namna gani?

Si rahisi kutozwa ushuru, kusaidia wenye hisa kulipa madeni ya Uchina, lakini mwishowe unaambiwa hii si serikali au nchi yako. Inauma sana. Mbona watu hawana huruma?

Hii ni desturi gani ambayo imeanzishwa nchini Kenya, yaani wananchi kuambiwa si wenyeji, kana kwamba ni wakimbizi katika nchi yao? Huu ni ungwana kweli?

Hata kama tungetaka kupuuza kauli ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kwamba serikali ya Kenya ni kama kampuni ya hisa, dalili zote zinaonyesha kwamba huo ndio ukweli wa mambo.

Hata vitabu vitakatifu vinatwambia tutawajua watu kwa mienendo yao, si maneno pekee. Huhitaji kunitukana ndio nijue una hila. Matendo pekee yatanijulisha una nia gani.

Wakati huu ambapo matatizo ya uchumi yanasikiwa na kila kabwela, ukininyima kazi kisha unitoze hata ndururu, wewe ni ama kupe, funza, kiwavi au mseto wa vyote hivyo! Yaani mnyonyaji wa kutupwa! Unataka nife ule nini?

Watu wasiotaka ujivunie kuwa Mkenya, ila wanakutegemea kulipa madeni na hata kujilipa mishahara, wanapaswa kuwa werevu kiasi cha kukuzuia kujinyonga.

Wanapaswa kututunza sisi mitambo ya kuwaundia pesa, angalau wakate miti au wapige marufuku kamba, nyaya na nyuzi zote kama walivyofanya sandarusi za plastiki ili tukwame.

Hapo watakuwa wametumia akili, wakatuweka hai, watufyonze damu sisi wajinga hadi tutakapoerevuka na kuwaambia watukome! Hadi wakati huo, kaa vizuri unyonywe.

  • Tags

You can share this post!

Kuria akaangwa kwa kutaka ushuru wa mitumba upandishwe hadi...

HABARI YA KIPEKEE: Mwanamume aliyejiteketeza kwa mafuta ya...

T L