• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:50 AM
JAMVI: Safari ya OKA, MKF imejaa visiki vingi

JAMVI: Safari ya OKA, MKF imejaa visiki vingi

Na CHARLES WASONGA

SIKU chache baada ya vinara wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA) kukutana na viongozi jopo la Mt Kenya Forum (MKF) kujadili mikakati ya kubuni muungano mkuu, kuna dalili kwamba huenda ndoto hiyo isitimie.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa na kisheria wanasema changamoto za kisheria na mivutano ndani ya OKA ni baadhi ya changamoto ambazo zinaweza kutibua mipango hiyo.Mnamo Jumatano wiki hii, vinara wa OKA; Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (Amani National Congress (ANC), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi walikutana na wanasiasa wa MKF wakiongozwa Martha Karua kujadili mipango ya kubuni mrengo wa tatu.

WANIA

Wanachama wengine kutoka Mlima Kenya waliohudhuria mkutano huo ni aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo, mbunge wa zamani wa Tetu Ndung’u Gethenji na mbunge wa zamani wa Mukurweini, miongoni mwa wengine. Pia alikuwepo Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi ambaye ametangaza kuwa atawania urais kwa tiketi ya chama cha Democratic Party (DP).

Akiongea na wanahabari baada ya mkutano huo katika mkahawa mmoja jijjini Nairobi, Bi Karua alisema wamekubaliana kuteua kamati maalum itakayojadili mikakati ya kubuniwa kwa muungano mkubwa.“Kamati hii itashirikisha wawakilishi wa vyama tanzu vinavyowakilishwa hapa leo.

Ni matumaini yetu kwamba baada ya muda wa mwezi mmoja kamati hiyo ya kiufundi itakuwa imeandaa mwongozo utakaosaidia kufanikisha ndoto yetu,” akasema Bi Karua ambaye ni kiongozi wa chama cha Narc Kenya.Akaongeza: “Sote tu Wakenya na hamna mmoja kati yetu ambaye anaweza kufaulu kivyake.

Hii ndio dhima kuu ya mkutano wa leo.”Bw Wetang’ula alisema mkutano wao ni kiashirio kwamba “siasa hubadilika kulingana na mahitaji ya nyakati.”“Sharti tuje pamoja, tuweke fikra zetu pamoja, tuzungumze pamoja na kutenda pamoja. Miungano ya OKA na Mt Kenya Forum imeanza safari ya kutembea pamoja.

Tulifanya mkutano wenye fanaka asubuhi ya leo, na mikutano mingine itafanyika siku zijazo. Tunawasihi Wakenya kuwa na subira,” akaeleza Bw Wetang’ula ambaye ni Seneta wa Bungoma.Bw Dismus Mokua ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa na uongozi anasema kuwa wanasiasa hao wamebuni fikra ya kuunda kwa mrengo wa tatu (Third Force), kuchelewa.

“Haitakuwa rahisi kwa wao kuelewana haswa kuhusu suala nyeti la nani kati yao atapeperusha bendera ya urais ya muungano huo ikizingatiwa kuwa OKA imejivuta kufikia uamuzi huo. Vile vile, Dkt Ruto na Bw Odinga wamepiga hatua kubwa zaidi kujinadi katika ngome za Mlima Kenya, Rift Valley na Magharibi mwa Kenya ambako baadhi ya wanasiasa hawa wanatoka,” akaongeza.

KUUZA SERA

Katika siku za hivi karibuni, Dkt Ruto na Bw Odinga wamekuwa wakiendesha kampeni katika maeneo ya Mlima Kenya na Magharibi mwa Kenya katika jitihada za kuuza sera zao.

Naibu Rais amekuwa akiuza sera zake zinazojikita katika mpango wa uimarishaji uchumi wa walalahoi, almaarufu “Bottom Up” huku Bw Odinga akiahidi kuwa atatoa ruzuku ya Sh6,000 kila mwezi kwa familia masikini chini ya kauli mbiu yake ya Azimio la Umoja.

Kampeni za wawili hawa zimeonekana kukumbatiwa na idadi kubwa ya Wakenya kwani kutokana na matokeo ya kura ya maoni iliyoendeshwa na kampuni ya TIFA wao ndio wagombeaji urais wenye ushawishi mkubwa zaidi nchini.Hali hii imekoleza dhana kuwa kinyang’anyiro cha urais 2022 itakuwa mbio za farasi wawili; Dkt Ruto na Bw Odinga.

Martin Andati, ambaye pia ni mchanguzi wa kisias, hofu ya kupoteza katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa urais ndio imechangia vinara wa OKA na wanasiasa wa Mlima Kenya kutafakari kuhusu haja ya kubuni mrengo wa tatu wenye nguvu.

“Japo uwepo wa “Third Force” wenye nguvu za kutikisa Dkt Ruto na kiongozi na Raila kuna changamoto nyingi ambazo zichangia kutofikiwa kwa ndoto hii. Kwa mfano, wanasiasa wa ANC wametoa makataa ya kutaka OKA itangaza mgombeaji wake wa urais kabla ya Desemba 25.

Isitoshe, wanashikilia kuwa sharti mgombeaji huyo awe Bw Mudavadi wala sio mwingine,” anasema Bw Andati.Vile vile, anaongeza, kumekuwapo na hisia kwamba Seneta Moi ni kibaraka cha Rais Kenyatta na Bw Odinga, hali ambayo Seneta wa Kakamega Cleophas Malala adai itayumbisha ndoto za OKA.

“Kanu imegeuka na kuwa wasaliti ndani ya OKA. Mchana Gideon aka na sisi na usiku anakutana na Raila pamoja na Uhuru. Hii ndio maana juzi tulitangaza wazi kwamba iwapo OKA haitakuwa imetangaza mgombeaji urais kufikia Desemba 25 mwaka huu, sisi kama ANC tutajitoa na kupanga mikakati ya kumfikisha Musalia Ikulu kivyetu,” anaeleza seneta huyo wa Kakamega.L

icha ya kuwa mwanachama wa OKA, Seneta Moi amekuwa akisisitiza kuwa sharti muungano huo ufanye kazi na Bw Odinga pamoja na Rais Kenyatta ili uweze kufikia azma yake.“Ni muhimu kwetu kushirikishja Rais Kenyatta na Raila katika hesabu zetu za kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Hii ndio njia ya kipekee itakayotuwezesha kufikia lengo letu la kulikomboa taifa hili kutoka kwa wafisadi ambao lengo lao ni kuporomosha uchumi wetu,” Seneta Moi akasema wiki moja iliyopita baada ya kuhudhuria ibada ya Jumapili katika kanisa moja eneo la Kitengela, kaunti ya Kajiado.Mwanasheria Bobby Mkangi anasema juhudi za kuunda muungano wa mrengo wa tatu, utakaoshirikisha OKA na Mt Kenya Forum, pia utakabiliwa na changamoto za kisheria.

“Hii ni kwa sababu chama cha Kanu kingali katika muungano rasmi na chama tawala cha Jubilee. Chama cha Wiper, chake Kalonzo pia kina mkataba wa ushirikiano kati yake na chama hicho cha kinachoongozwa na Rais Kenya. Kwa hivyo, itabidi Kanu na Wiper zivunje mahusiano yao na Jubilee kabla ya kurasimisha nafasi yao katika OKA na muuungano mwengine ambao wanapanga kubuni,” anasema.

“Ilivyo sasa ni kwamba OKA haitambuliwa rasmi kama muungano kwani vyama tanzo hawatia saini mkataba wa kubuni muungano huo na kasha kuuwasilisha katika afisi ya Msaji wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu,” anaongeza mwanasheria huyo ambaye alishiriki katika mchakato wa kuandika katiba ya sasa.

You can share this post!

Suala la ardhi latumiwa kama chombo kumega kura za Pwani

Njaa yawakosesha wanafunzi 1,603 umakinifu Mbeere

T L