• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 8:55 PM
JUNGU KUU: Gachagua atajiponza ‘akiupigania’ Mlima

JUNGU KUU: Gachagua atajiponza ‘akiupigania’ Mlima

NA WANDERI KAMAU

NAIBU Rais Rigathi Gachagua yuko katika hatari kujikwaa kisiasa katika juhudi za ‘kulitetea’ eneo la Mlima Kenya, kwani anaonekana kuyatenga maeneo mengine nchini.

‘Utetezi’ huo pia umezua hofu, kwani umeonekana kuingilia uhuru wa kimajukumu wa baadhi ya viongozi na maafisa wakuu serikalini.

Kwa mfano, kwenye hafla ya kutoa shukrani kutokana na uteuzi wa Bi Rebecca Miano kama Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maeneo Kame katika eneo la Shamata, eneobunge la Ndaragwa, Kaunti ya Nyandarua wiki iliyopita, Bw Gachagua alisema kuwa katika siku kadhaa zijazo, atahakikisha kuwa nafasi nyingi serikalini zinachukuliwa na watu kutoka ukanda wa Mlima Kenya.

“Ngonjeni. Mtaona tu. Katika siku chache zijazo, mtasikia orodha ya watu watakaokuwa katika Utumishi wa Umma. Wengi watatoka katika eneo hili. Kwani ni vibaya?” akauliza Bw Gachagua huku akishangiliwa na mamia ya wenyeji waliokuwa wamefika katika hafla hiyo.

Katika hafla iyo hiyo, Bw Gachagua alimwamuru Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu kuwapa kazi wanaume wawili waliojitokeza kwake kumrai awatafutie kazi.

Upeo wa ‘utetezi’ wa Bw Gachagua kwa wenyeji wa Mlima Kenya ulikuwa agizo lake kwa Gavana Johnson Sakaja wa Nairobi, kuhakikisha kuwa hayaondoi magari ya uchukuzi wa umma (matatu) kutoka katika eneo la katikati ya jiji la Nairobi.

Akihutubu Jumanne katika Kaunti ya Nyeri, Bw Gachagua alisema hatua hiyo itakuwa sawa na “kuwaumiza wafanyabiashara kutoka Mlima Kenya”.

Alisema Bw Sakaja anafaa kumwiga Gavana Susan Kihika wa Nakuru, aliyeruhusu matatu kurejea kati kati ya jiji hilo ili “kupata uungwaji mkono wa jamii ya Wakikuyu 2027”.

Kutokana na matamshi haya, wadadisi wanasema kuwa Bw Gachagua yuko katika hatari kubwa kujikwaa kisiasa, kwani mbali na kuwa na mazoea ya kutumia lugha yake asili katika majukwaa ya umma, maeneo mengine yanahisi kutengwa na mwelekeo wake.

“Gachagua anaonekana kusahau kuwa yeye ni Naibu Rais wala si kiongozi wa kisiasa wa Mlima Kenya pekee. Kuna hatari baadhi ya kauli zake zikaisawiri serikali ya Rais William Ruto kuwa ya watu kutoka maeneo machache nchini pekee,” asema Bw Oscar Plato, mchanganuzi wa siasa.

Wadadisi wanasema kwamba kuna hatari kubwa mwelekeo huo ukatia doa juhudi za Rais Ruto kuiunganisha nchi, hasa baada ya mgawanyiko mkubwa wa kisiasa uliotokea kutokana na uchaguzi wa Agosti.

“Rais Ruto amekuwa akijaribu kuiunganisha nchi ili kubuni mazingira bora ya kutimiza ahadi zake. Vile vile, lengo lake ni kuondoa mgawanyiko wa kisiasa ambao umekuwepo tangu uchaguzi wa Agosti, hasa kutoka kwa wafuasi wa kiongozi wa Azimio Bw Raila Odinga. Amekuwa akijaribu kuondoa dhana kuwa serikali yake itayahudumia maeneo yaliyompigia kura pekee,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Anasema kuwa ikizingatiwa kwamba Rais Ruto ni mwanasiasa anayelenga kuwania urais 2027, hatasita kumtenga Bw Gachagua ikiwa ataibuka kuwa kikwazo katika karata zake za kisiasa.

  • Tags

You can share this post!

Uwezo Fund: Vikundi 18 Mvita vyapokea Sh3 milioni kujikimu...

SOKOMOKO: Wivu wa mapenzi huenda utamvua Nyamu useneta

T L