• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
SOKOMOKO: Wivu wa mapenzi huenda utamvua Nyamu useneta

SOKOMOKO: Wivu wa mapenzi huenda utamvua Nyamu useneta

NA CHARLES WASONGA

WASWAHILI waligonga ndipo walipoamba kwamba; mapenzi ni kikohozi, hayafichiki.

Ukweli wa msemo huu ulidhihiri wiki moja iliyopita katika kilabu kimoja cha burudani Dubai, katika Umoja wa Milki za Kiarabu (UAE).

Hii ni baada ya Seneta Maalum Karen Nyamu kuzua sokomoko na sarakasi katika jitihada zake za kuonyesha kwamba bado anampenda mwanamuziki wa mtindo wa mugithi Samuel Muchoki, almaarufu, Samidoh.

Mapenzi yalimpofusha mheshimiwa huyu kiasi cha kutoweza kumwona wala kumtambua mkewe Samidoh, Edith Nderitu ambaye alikuwepo ukumbini humo.

Samidoh na Nyamu walikuwa wametengana lakini baada ya wao kujaaliwa watoto wawili, miale ya usuhuba ilikuwa bado inatoa mwangaza.

Sasa Seneta huyo amejipata pabaya kwani sarakasi zake zimekera uongozi wa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA), kilichomteua kuwa Seneta Maalum kuwakilisha masuala ya jinsia ya kike katika seneti.

UDA imesema kuwa mienendo ya Bi Nyamu, ambaye ni mwanasheria, imemharibia sifa na kuvuruga hadhi yake nchini na kimataifa.

Mnamo Ijumaa, Desemba 22, 2022, Seneta huyo alifika mbele ya Kamati ya Nidhamu ya UDA chini ya uenyekiti wa Charles Njenga katika makao makuu ya chama hicho katika jumba la Hustler Plaza, Nairobi.

“Katika kisa hicho, kilichonaswa kwenye kanda ya video na kusambazwa katika mitandao, mienendo yako imeleta aibu na kushusha hadhi ya chama kilichokuteua kuwa seneta maalum,” Bw Njenga akasema kwenye barua ya kumwamuru Bi Nyamu kufika mbele ya kamati yake.

Sasa miongoni mwa adhabu zinazomsubiri Bi Nyamu ni kuvuliwa wadhifa wa Seneta Maalum wa chama cha UDA, endapo kamati hiyo itampata na hatia.

  • Tags

You can share this post!

JUNGU KUU: Gachagua atajiponza ‘akiupigania’ Mlima

KIGODA CHA PWANI: Uchaguzi mkuu ulivyobadili mkondo wa...

T L