• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:22 PM
JUNGU KUU: Hatari ya magavana waliomaliza mihula yao kuwa maseneta

JUNGU KUU: Hatari ya magavana waliomaliza mihula yao kuwa maseneta

NA BENSON MATHEKA

HUENDA utawala wa magavana kadhaa ukakosa kupigwa darubini baada ya watangulizi wao kushinda useneta.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kwamba itakuwa vigumu kwa maseneta waliokuwa magavana kuwapiga darubini warithi wao au hata warithi hao kuwaandama wakigundua kwamba walitumia vibaya pesa za kaunti kwa miaka kumi ambayo wamekuwa uongozini.

“Kuna hatari katika kaunti ambazo magavana wamekuwa maseneta kwa sababu itakuwa vigumu kwa wakuu hao wa zamani wa kaunti kuchunguzwa na warithi wao. Hii ni kwa sababu waliwasaidia kuingia mamlakani kwa kuwapigia debe wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt Geff Kamwanah.

Kulingana naye, hali hii inazidishwa na ukweli kwamba magavana na maseneta hao wanatoka chama kimoja cha kisiasa.

“Chukua kwa mfano kaunti ya Uasin Gishu ambapo Bw Jackson Mandago alichaguliwa seneta ilhali alikuwa akimpigia debe mrithi wake Bw Jonathan Bii Koti Moja. Hautarajii Bw Bii kumchukulia hatua Bw Mandago akigundua alifanya makosa katika utawala wake wa miaka kumi au Bw Mandago afichue utendakazi duni wa mrithi anayemlinda,” asema Dkt Kamwanah.

Kulingana na Katiba, kazi ya seneti ni kutetea ugatuzi kwa kuhakikisha magavana wanatumia vyema pesa zinazotengewa kaunti zao.

Aidha, maseneta huwa wanatunga sheria zinazotia nguvu ugatuzi. Wachanganuzi wa siasa wanasema kwamba ingawa katiba haipingi marufuku magavana kugombea useneta au maseneta kugombea ugavana, kuna hatari ya kurudisha nyuma ugatuzi.

“Ugatuzi uko hatarini kwa kuwa magavana wanaokamilisha mihula miwili wanaweza kutawala seneti kwa lengo la kujikinga wasichukuliwe hatua kwa makosa wanayofamya wakiwa ofisini kama vile ubadhirifu wa pesa,” asema mchanganuzi wa siasa Wakili Ulbanus Kamau.

Baada ya kuhudumu kama gavana wa Mandera kwa mihula miwili, Bw Ali Roba alishinda useneta kaunti hiyo kwa tiketi ya chama cha United Democratic Movement (UDM) huku aliyekuwa spika wa Bunge la kaunti hiyo Adan Khalif akishinda ugavana kwa tikiti ya chama hicho.

Bw Kamau anasema mbali na kuwa wamekuwa wakishirikiana kwa muda, wawili hao wanatoka chama kimoja.

“Katika kaunti ya Mandera, Seneta Roba, akiwa kiongozi wa chama cha UDM anatarajiwa kumpiga darubini gavana wa chama chake, ambaye wamekuwa wakishirikiana katika bunge la kaunti,” asema Bw Kamau.

Anasema hali hii inashuhudiwa katika kaunti nyingi ambako gavana, seneta na wawakilishi wa wadi wanatoka chama kimoja.

“Katika kaunti nyingi, kulikuwa na kampeni ya kupiga kura kwa suti, kuhakikisha gavana, seneta na madiwani, mwakilishi wa wanawake na rais wanatoka chama kimoja. Hii inamaanisha kuwa katika mabunge ya kaunti, magavana wanaweza kushawishi madiwani walio wengi kuteua spika anayeweza kuwakilisha maslahi yao na hivyo basi kuzima juhudi zozote za kusukumwa kuwajibika,” akasema.

Kulingana na wadadisi, magavana wengi watachukua kila hatua kujikinga dhidi ya presha za madiwani na maseneta walio na nguvu za kuwatimua ofisini.

“Kulingana na hali ilivyo, magavana wengi wamejikinga kwa kuwa madiwani wengi na hata maseneta wanatoka vyama vyao vya kisiasa. Hivyo basi, kuna uwezekano wa wapigakura kukosa wa kuwatetea iwapo magavana watakosa kuwajibika au kutumia vibaya rasilmali za kaunti,” akasema Dkt Kamwanah.

  • Tags

You can share this post!

MIKIMBIO YA SIASA: Weta acheza pata potea

Haaland atambisha Man-City dhidi ya Crystal Palace katika...

T L