• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:22 PM
MIKIMBIO YA SIASA: Weta acheza pata potea

MIKIMBIO YA SIASA: Weta acheza pata potea

NA CHARLES WASONGA

HUENDA Seneta Mteule wa Bungoma Moses Wetang’ula anacheza karata ya pata potea kufuatia uamuzi wake wa kujitosa katika kinyang’anyiro cha Uspika wa Bunge la Kitaifa.

Kisheria, kabla ya kiongozi huyo wa Ford Kenya kuwasilisha ombi la kuwania kiti hicho, sharti ajiuzulu wadhifa wake wa useneta.

Pili, sharti ajenge imani ya wabunge wote wa mrengo wa Kenya Kwanza (KKA) na baadhi ya wabunge waliochaguliwa kwa tiketi za vyama tanzu katika muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.

Wakati huu, mrengo wa Azimio una jumla ya wabunge 162 waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 huku mrengo wa KKA ukiwa na wabunge 159.

Lakini KKA, chini ya uongozi wa Rais Mteule William Ruto, imefaulu kuvutia wabunge 10 kati ya 12 waliochaguliwa kwa tiketi huru na baadhi ya wabunge waliochaguliwa kwa tiketi za vyama tanzu katika Azimio.

Kwa sababu hiyo, kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi juzi alidai kwa ujumla mrengo wa KKA unaungwa mkono na karibu wabunge 180.

“Kwa hivyo, tuko na imani kwamba ndugu yangu Moses Wetang’ula atatwaa wadhifa wa Uspika wa Bunge la Kitaifa kwa urahisi zaidi,” akasema.

Kulingana na mkataba wa maelewano uliobuni muungano na Kenya Kwanza, Bw Wetang’ula aliahidiwa kutunukiwa kiti hicho, endapo KKA itashinda uchaguzi wa urais.

Kwa upande wake, Bw Mudavadi aliahidiwa cheo cha Mkuu wa Mawaziri huku aliyekuwa gavana wa Kilifi Amason Kingi akiahidiwa wadhifa wa Upika wa Seneti.

Akiongea katika mkutano wa magavana, wabunge na maseneta waliochaguliwa kwa tiketi ya vyama vilivyoko ndani ya KKA wiki jana, Dkt Ruto alibainisha kuwa Mbw Wetang’ula na Mudavadi “watapewa viti walivyoahidiwa kwa sababu sisi ni watu wangwana wasiopenda kuvunja ahadi.”

Lakini sasa wadadisi wanasema kuwa huenda Bw Wetang’ula akapoteza viti hivyo viwili (useneta na uspika wa bunge la kitaifa) endapo, kwanza, muungano wa Azimio utamdhamini kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kwa wadhifa huo.

Pili, wanabashiri kuwa endapo Majaji wa Mahakama ya Juu watabatilisha ushindi wa Dkt Ruto huenda wabunge waliogura Azimio wakarejea.

Mgombea urais wa Azimio Raila Odinga na watu wengine waliwasilisha kesi katika mahakama hiyo kupinga uhalali wa ushindi wa Dkt Ruto uliotangazwa na mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati mnamo Agosti 15.

“Endapo Azimio itamwasilisha kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kwa kinyang’anyiro cha uspika wa bunge la kitaifa, haitakuwa rahisi kwake kushinda. Hii ni kwa sababu Kalonzo ana uwezo wa kushawishi wabunge wengi wa mrengo wa Kenya Kwanza wamuunge mkono,” anasema aliyekuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Amerika (USIU), tawi la Kenya, Profesa Macharia.

Duru zinasema kuwa kuna baadhi ya wabunge wa mrengo wa KKA, wameanza kuchukizwa na Bw Wetang’ula kutokana na kile wanachodai ni hatua yake ya “kujipiga kifua vijijini.”

Hii ni kutokana na kauli ambayo kiongozi huyo wa Ford Kenya alitoa alipohudhuria hafla ya mazishi katika kaunti ya Bungoma kwamba, “mimi ndiye kiongozi wa tatu mwenye mamlaka zaidi nchini kwa sababu nitatwaa kiti cha uspika wa bunge la kitaifa kwa urahisi,”

“Kwa kuwa uchaguzi wa Spika wa Bunge la Kitaifa huendeshwa kwa njia ya siri, huenda wabunge waliochukizwa na matamshi kama haya wakaamua kumwadhibu Wetang’ula kwa kumnyima kura. Hivyo, atakuwa amepoteza kuwili; kiti cha useneta na uspika, kwa mpigo,” Profesa Munene anaeleza.

  • Tags

You can share this post!

KIGODA CHA PWANI: Yaelekea PAA haijatosha kuwa sauti ya...

JUNGU KUU: Hatari ya magavana waliomaliza mihula yao kuwa...

T L