• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Kidosho wa miaka 27 asema ataoleka baada ya kuwa milionea kupitia kilimo cha mahindi

Kidosho wa miaka 27 asema ataoleka baada ya kuwa milionea kupitia kilimo cha mahindi

NA MWANGI MUIRURI

KUTANA na Grace Wangechi Kamande mwenye umri wa miaka 27, mzawa wa Kaunti ya Kirinyaga ambaye hushiriki kilimo cha mahindi.

Baada ya kujaribu kilimo hicho akitegemea mvua, alibadilisha mbinu na kukumbatia mfumo wa unyunyiziaji maji.

“Nilianza kilimo hiki mwaka wa 2020 maradhi ya Korona yaliponiondoa jijini Nairobi nilikokuwa nikisuka watu nywele,” anasema.

Anasema kwamba katika harakati zake za kuchumbiana, alikutana na mwanamume wa eneo la Nyanza ambaye alimpa mtaji wa kujipa riziki mashinani alikotorokea maradhi hayo.

“Kwa kuwa hatukuwa tumeafikiana kuoana, nilichukua mtaji huo wa Sh250, 000 na nikaingia katika shamba la babangu ambapo nilizindua kilimo hicho,” asema.

Bi Kamande anasema kwamba “msimu wa kwanza ulinipeleka visivyo kwa kuwa baada ya kulima shamba, gharama za fatalaiza na usaidizi wa vibarua na kisha nikanunua mbegu, nilipata faida ya Sh2, 000 pekee”.

Baada ya kungoja miezi mitatu ili mahindi yawe tayari kwa soko, alivuna takriban mabichi 10, 000 ambapo bei sokoni kwa kila hindi lilikuwa Sh8.

“Mtaji wangu uliteremka hadi Sh120, 000 na nilijua nilikuwa nakodolea macho kufilisika. Ndipo nilipata ushauri kutoka kwa wataalamu wa kutengeneza fatalaiza ya Yara na wakaniwezesha kuingia katika kilimo cha unyunyiziaji maji,” asema.

Kampuni ya Yara, asema, ilimpa ushauri kuhusu matumizi ya fatalaiza na pia ukadiriaji wa ubora na vipimo huku akipata pia uelekezi kuhusu mbegu.

Kupitia bidii yake, Bi Kamande aliweza kupanga ratiba ya kuwa na takriban mahindi mabichi 50, 000 sokoni kila mwezi.

Bi Grace Wangechi Kamande 27 achambua mahindi aliyovuna tayari kwa soko katika Kijiji cha Gatitika Kaunti ya Kirinyaga mnamo Julai 5, 2023. Picha|MWANGI MUIRURI

“Wakati wa kiangazi huwa ndio bora wa biashara hii kwa kuwa bei kwa kila hindi hupanda hadi Sh30 huku wakati wa mvua bei hiyo ikishuka hadi Sh5,” akaambia Taifa Leo Dijitali wakati wa mahojiano.

Lakini katika hali hizo zote, alisema usaidizi wa wataalamu umemwezesha kupunguza gharama ya uzalishaji hadi asilimia 45 kutoka 70 akianza harakati za upanzi wa mahindi.

“Leo hii, mahindi ndio riziki yangu na hivi karibuni natazamia kuibuka milionea wa kujijenga kupitia mahindi na pia niingilie kilimo cha uzalishaji maziwa na kuku wa nyama,” akasema.

Aliitaka serikali izidi kuteremshia wakulima gharama za uzalishaji ili viwango vya faida viongezeke.

Bi Kamande alisema kwamba “Kuna matumaini makuu kwamba sekta ya kilimo biashara ndiyo itazindua awamu mpya ya mamilionea katika miaka ya hivi karibuni”.

Akifanikiwa, asema ndio ataamua kuhusu ndoa na kupata watoto baada ya kujinunulia shamba lake ili azindue harakati za kilimo nje ya boma la baba yake.

 

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Saini za Raila zitatoboa?

Mhudumu wa bucha Ruiru achoma kijana kwa supu moto

T L