• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 3:19 PM
Mhudumu wa bucha Ruiru achoma kijana kwa supu moto

Mhudumu wa bucha Ruiru achoma kijana kwa supu moto

NA SAMMY WAWERU

MHUDUMU wa bucha eneo la Ruiru, Kiambu anaandamwa na mkono wa sheria baada ya kutumbukiza kijana kwenye sufuria ya supu inayochemka.

Mvulana huyo anayekisiwa kuwa chini ya umri wa miaka 20, inasemekana husambaza mifuko ya kupakia bidhaa kwa kutumia pikipiki.

Kulingana na walioshuhudia, alikuwa ameegesha pikipiki karibu na alikokuwa akipikia supu mshukiwa.

“Alikuwa katika harakati za kusambaza bidhaa anazochuuza,” akasema Grace Njeri, mmoja wa walioshuhudia.

Watu wakishuhudia kisa ambapo mhudumu wa bucha eneo la Kwa Kairu, Ruiru alichoma mfanyabiashara mchanga kwa supu moto. Picha|SAMMY WAWERU

Tukio hilo lilifanyika wikendi katika eneo la Kwa Kairu, Ruiru.

Inaarifiwa kwamba wawili hao walianza kurushiana maneno, mhudumu wa bucha akitaka mfanyabiashara huyo mchanga kuondoa pikipiki yake haraka iwezekanavyo.

Licha ya kijana huyo kumrai ampe muda mfupi, majibizano kati yao yaliishia jamaa kumnyanyua na kumtumbukiza kwenye sufuria kubwa iliyokuwa ikitokota supu.

Mwathiriwa aliuguza majeraha mabaya, walioshuhudia na wapitanjia wakitishia kutia adabu mwanabucha huyo.

Alijifungia kwenye mojawapo ya maduka ili kuokoa maisha yake.

Masalia ya supu iliyotumika kuchoma kijana eneo la Kwa Kairu, Ruiru. Picha|SAMMY WAWERU

Umma uliokuwa na ghadhabu nusra uvunje mlango wa duka hilo, ukiapa kumwadhibu.

“Huyu kijana ni sawa na mtoto wake. Ni unyama ulioje kumtendea ukatili wa aina hii kwa kumchoma kwa supu?” Ken Kamau mhudumu wa bodaboda eneo la Kwa Kairu alishangaa.

Mshukiwa aliokolewa na chifu eneo hilo, aliyerai watu kutochukua sheria mikononi mwao.

Hata licha ya mvulana huyo kuuguza majeraha mabaya, mamake alipofika alishangaza akidai hatamchukulia hatua kisheria ila Mungu atamwadhibu.

Hatua ya mhudumu wa bucha kuchoma kijana aliyekuwa akijitafutia riziki eneo la Kwa Kairu, Ruiru ilighadhabisha umma. Picha|SAMMY WAWERU

“Nimemwachia Mungu, atanilipizia kisasi,” mama huyo aliyelemewa na machozi alisema.

Taifa Leo Dijitali imebaini kuwa mhudumu huyo wa bucha amekuwa na visa kadhaa vya kuvamia watu hasa anaotofautiana nao.

“Si mara ya kwanza kuzua vita. Amekuwa na mazoea ya kupiga watu, hata wateja wake,” alisema mkazi aliyeomba kubana majina yake.

Cha kushangaza ni kwamba anaposhtakiwa kwa maafisa wa usalama, hakuna hatua inayochukuliwa.

  • Tags

You can share this post!

Kidosho wa miaka 27 asema ataoleka baada ya kuwa milionea...

Mume na mke watambuliwa kortini kama wavamizi wa mkurugenzi...

T L