• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:55 AM
Saini za Raila zitatoboa?

Saini za Raila zitatoboa?

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga anakabiliwa na vizingiti vingi katika juhudi zake za kumwondoa mamlakani Rais William Ruto kupitia ukusanyaji wa saini milioni 10 kutoka kwa Wakenya.

Ingawa Bw Odinga, na wenzake, wanashikilia kuwa mbinu hiyo imo katika kipengele cha kwanza cha Katiba kinachowapa wananchi nguvu za kuondoa mamlaka ya rais, ukusanyaji saini hautambuliwi na sheria hiyo kuu kama mojawapo ya njia za kumwondoa rais mamlakani.

Kulingana na kipengele cha 145 cha katiba rais anaweza kuondolewa mamlakani kupitia hoja inayowasilishwa na mbunge atakayeungwa mkono na angalau thuluthi moja ya wenzake wote.

Kipengele hicho cha katiba kinataja sababu za kumwondoa mamlakani rais kuwa; ukiukaji wa Katiba, rais akitenda uhalifu kinyume na sheria za kitaifa au kimataifa au akishiriki mienendo mibaya inayoshusha hadhi ya afisi hiyo.

Katika bunge la kitaifa, hoja ya kumwondoa mamlakani rais sharti iungwe na angalau thuluthi mbili ya idadi ya jumla ya wabunge.

Hii ni sawa na jumla ya wabunge 233 kati ya 349; idadi ambayo wakati huu ni vigumu kwa Azimio kupata ikizingatiwa kuwa baadhi ya wabunge wake wamebadili msimamo wa kisiasa na kuunga mkono mrengo tawala wa Kenya Kwanza (KKA).

Hali hii ilijidhihirisha juzi wakati wa upigaji kura kuhusu mapendekezo yenye utata kwenye Mswada wa Fedha (sasa sheria) baadhi ya wabunge wa Azimio walipokaidi msimamo wa vinara wao na kuungana na wenzao wa KKA kuyapitisha.

Endapo hoja ya kumng’oa mamlakani Rais itaungwa mkono na wabunge 233 katika bunge la kitaifa, spika atawasilisha hoja hiyo kwa mwenzake wa seneti ndani ya siku mbili.

Seneti itaunda kamati maalum ya wanachama 11 kuchunguza tuhuma dhidi ya Rais.Ili tuhuma hizo zithibitishwe, zitahitaji kuungwa mkono na angaa thuluthi mbili ya maseneta (maseneta 44 kati ya 67).

Ilivyo sasa, KKA inaungwa mkono na karibu wabunge 208 baada ya baadhi ya wabunge wa vyama vya Jubilee (26), UDM (8), PAA (2), MCC (1) na wabunge wanane wa ODM kuamua kushirikiana nayo.

Hali ni hiyo hiyo katika Seneti ambapo maseneta wa Azimio kama vile Margaret Kamar (seneta maalum), Fatuma Dullo (Jubilee) na Tom Ojienda (ODM) wameungana na maseneta 38 wa KKA kuunga mkono sera za Rais Ruto.

“Kwa kuwa Rais Ruto tayari ameonyesha kuwa ameteka mabunge yote mawili, hoja ya kumwondoa itazimwa kwa haraka zaidi,” anasema wakili Peter Wandiga.

“Hata mkondo huu wa ukusanyaji wa saini milioni 10 bado unakabiliwa na changamoto kwa sababu wakati huu, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ni kigae kisicho na mwenyekiti pamoja na makamishna sita.

“Hata kama Azimio itafaulu kukusanya saini hizo, sharti zipigwe msasa na IEBC kubaini kama wenyewe ni wapiga-kura waliosajiliwa. Kazi hiyo sharti iendeshwe chini ya usimamizi wa angalau makamishna watatu wa IEBC kulingana kipengele cha 88 cha Katiba,” anaeleza.

Lakini akiongea katika uwanja wa Kamukunji Ijumaa, Bw Odinga alishikilia kuwa “kufikia mwezi ujao tutakuwa tumefaulu kukusanya saini milioni 10 kuondoa mamlakani utawala huu dhalimu”.

“Wananchi ndio wenye mamlaka makuu kwa mujibu wa kipengele cha kwanza cha Katiba. Na wanaweza kumpokonya Ruto mamlaka hayo kwa sababu amekataa kutimiza matakwa yao kama vile kupunguza gharama ya maisha,” Bw Odinga akasema.

Mwanasheria Fred Ogolla anaunga mkono kauli ya Bw Odinga akisema Rais anaweza kuondolewa mamlakani hata bila kupitia bunge.

“Baada ya Azimio kukusanya saini milioni 10, mahakama inaweza kubuni jopo la kuthibitisha saini kisha kupendekeza kubuniwa kwa Baraza la Wawakilishi linaloweza kumwondoa Rais mamlakani,” akasema kwa njia ya simu. Prof Ogolla, aliye pia kiongozi wa vuguvugu la Operation Linda Ugatuzi aliongeza kuwa mbinu hiyo imewahi kutumika nchini Nigeria.

“Mahakama inaweza kusimamisha utekelezaji wa vipengele vyovyote vya Katiba kwa lengo la kutimizwa matakwa ya raia. Katiba iliundwa kuwatumikia rais na hivyo raia hawafai kuwa watumwa wa Katiba,” anasema.

Hata hivyo, mbinu hiyo ya kumwondoa Rais Ruto kupitia sahihi za Wakenya imesolewaa na wakili Ahmednassir Abdullahi akiutaja kama “mchezo wa bahati nasibu.

 

  • Tags

You can share this post!

Mbunge asema ilibidi atafute wafadhili kujaza kibaba cha...

Kidosho wa miaka 27 asema ataoleka baada ya kuwa milionea...

T L